HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, December 7, 2022

MAVUNDE AKABIDHI WAKULIMA NYENZO AKIHIMIZA KILIMO CHA TIJA, MATUMIZI YA TEKNOLOJIA

 

Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde akikata utepe kuashiria ugawaji wa zana za kilimo na vyombo vya usafiri kwa wakulima wadogo na maofisa ugani wa Mradi wa Beyond Cotton,hafla iliyofanyika wilayani Misungwi.
Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde (mwenye kofia) akiendesha moja ya mashine ya kulimia (rotary machine) kabla ya kukabidhi nyenzo hizo kwa wakulima wadogo wa Mradi wa Beyond Cotton wilayani Misungwi,wanaoshuhudia kutoka kulia ni Katibu Tawala Msaidizi (Kilimo) Mkoa wa Mwanza, Emil Kasagara na Mratibu wa mradi huo,Dk. Paul Saidia (mwenye koti jeusi).Picha zote na Baltazar Mashaka.

NA BALTAZAR MASHAKA, MISUNGWI
NAIBU Waziri wa Kilimo,Anthony Mavunde amewataka wakulima wa Pamba na mazao ya mengine kutumia teknolojia,kanuni na zana bora za kilimo kuongeza tija,thamani, usalama wa chakula na lishe.

Amesema kilimo hakiwezi kuendelea bila utafiti, hivyo watafiti waendelee kufanya utafiti,kubuni mbinu na kuja na teknolojia mbalimbali ili kukuza sekta ya kilimo nchini.

Amesema katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Ukiriguru,wilayani Misungwi,mkoani Mwanza, wakati akikabidhi zana za kilimo na vyombo vya usafiri kwa baadhi ya wakulima wadogo na maofisa ugani wa Mradi wa Uzalishaji Pamba kwa Tija na Usalama wa Chakula ‘Beyond Cotton’.

Amesema kilimo kina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi yetu ana akawasihi wakulima wa zao la pamba na mengine ya chakula lishe wafuate kanuni sahihi,watumie zana na teknolojia vizuri kuongeza tija na ufanisi katika kazi,pia pikipiki zitumike kupeleka elimu iliyokusudiwa kwa wakulima.

“Wakulima wengi wa pamba ni changamoto kubwa hawalimi kwa tija na mradi huu wa Beyond Cotton ni wenye manufaa kwa maendeleo ya wakulima wetu,ukisimamiwa vizuri utaleta tija,hivyo TARI endeleeni kutafuta miradi yenye tija ya aina hiyo na ninatamani kuona nini kitafanyika na matokeo yanayoshikika”amesema Mavunde.

Naibu waziri huyo ameongeza kuwa mradi wa Beyond Cotton umegusa kila eneo ikiwemo miundombinu,uzalishaji wa mbegu bora,kuongeza thamani, kusaidia usalama wa chakula na lishe bora kwa wakulima.

Kwa mujibu wa Mavunde vifaa vilivyokabidhiwa ni pikipiki tatu,zana za kulimia (rotary mashine) moja,za kupandia 200 na ya kupalilia (weeder) moja kila wilaya,pia mashine rahisi moja ya kutengeneza nguo na ya kutengeneza mkaa mbadala kwa kutumia miti ya mabaki ya pamba.
Aidha ameeleza kuwa utafiti ni moyo wa kilimo na ili kiwanufaishe wakulima na kukuza sekta hiyo,watafiti waendelee kufanya utafiti wabuni mbinu waje na teknolojia ya kisasa kusaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kipato.

Naye Katibu Tawala Msadizi (Kilimo) Mkoa wa Mwanza,Emil Kasagara,ameishukuru serikali kuleta mradi wa kuendeleza zao la pamba (tija na thamani)chakula na lishe,pia mradi kutoa vitendea kazi vitakavyowasaidia wataalamu kuwafikia wakulima na kutoa huduma za ugani kwa wakati na zana zitakazo warahisishia kilimo cha mazao.

Amesema Mkoa wa Mwanza msimu huu unalenga kuongeza uzalishaji wa pamba kutoka kilo 500 hadi 600,bila vitendea kazi vya uhakika na zana bora uzalishaji huo hauwezi kufikiwa na kuahidi kufuatilia ili kuhakikisha malengo ya serikali na mradi yanafikiwa.

Awali Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Ukiriguru na Mratibu wa Zao la Pamba nchini,Dk.Paul Saidia, amesema mradi wa Beyond Cotton utawajengea wakulima uwezo katika kuongeza tija na thamani ya zao la pamba na mazao mengine yanayolimwa na wakulima wa pamba,pia utachangia usalama wa chakula na lishe.

Amesema mradi huo wa uzalishaji zao la Pamba kwa tija na usalama wa chakula unafadhiliwa na Serikali ya Brazil kwa USD 629,000,utatekelezwa katika wilaya tatu za Magu,Misungwi na Kwimba,utawafikia wakulima wadogo 9000, mbali na vitendea kazi utatoa elimu ya nadhalia na vitendo kwa wakulima.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad