HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 30, 2022

RUWASA KUWATEMA WAKANDARASI WABOVU NA WABABAISHAJI

 Na Muhidin Amri, Mufindi

WAKALA wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) imesema, haitarudia kosa la kuwapa kazi wakandarasi wenye rekodi ya kufanya vibaya na wasiokuwa na uwezo katika kutekeleza ujenzi wa miradi ya maji hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo,mara baada ya kukagua mradi mkubwa wa maji unaojengwa katika kijiji cha Mkalala Halmashauri ya wilaya Mufindi mkoani Iringa kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 3.2.

Kivegalo,amewataka wakandarasi na mafundi wadogo wanaopewa kazi ya kujenga miradi ya maji hapa nchini,kutanguliza uzalendo na kujenga miradi kwa ubora wa hali ya juu ili kuisaidia serikali yao kutimiza lengo la kupeleka na kuboresha huduma ya maji kwa wananchi kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95.

Alisema, kwa sasa Ruwasa imetengeza mifumo maalum ambayo wakandarasi wabovu watajiondoa wenyewe kuomba kazi, ikiwamo kutoa cheti cha umahili wa kukamilisha mradi kwa kila mkandarasi atakayemaliza kazi ambacho kitatumika kama sifa mojawapo(CV) pale anapoomba kazi nyingine.

Kivegalo,amempongeza mkandarasi kampuni ya Gnms Contructions Co Ltd ya Iringa kwa kazi nzuri katika kutekeleza mradi huo ambayo sehemu kubwa ya kazi hiyo ambayo hadi sasa imefikia asilimia 60 ya utekelezaji wake ametumia fedha zake na Ruwasa imemlipa asilimia 15 tu ya gharama.

Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa ,amefurahishwa na kazi za mkandarasi na kuhaidi kumlipa kiasi cha fedha kilichobaki baada ya muda mfupi na pia kuendelea kumtumia kwenye ujenzi wa miradi maji katika maeneo mengine hapa nchini.

Alisema,siku za nyuma changamoto kubwa la wakandarasi wengi ni pale waliposhindwa kukamilisha kazi wanazopewa huku fedha nyingi za serikali zikiwa zimeshatumika,jambo lililo sababisha fedha za umma kushindwa tija na kumaliza changamoto ya maji kwa wananchi.

Kwa upande wake Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mufindi Happy Mrisho alisema, mradi ulianza kutekelezwa mwezi April na ulitarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu na muda wa utekelezaji ni miezi sita.

Hata hivyo alieleza kuwa, kutokana na changamoto mbalimbali Mkandarasi ameongezewa muda na sasa kazi zote za ujenzi zitakamalika mwezi Februari mwaka 2023.

Alisema,mradi huo utakapokamilika utamaliza changamoto ya huduma ya maji kwa wakazi zaidi ya 19,850 wa vijiji vitatu vya Ikwega,Mkalala na Igowole ambao kwa sasa wanalazimika kutumia vyanzo vingine ili kupata huduma ya maji.

Mrisho alitaja gharama za mradi huo ni Sh.bilioni 3,242,561,649.15 na mkandarasi ameshalipwa kiasi cha Sh.milioni 486,384,247.37 fedha zilizotolewa na serikali kupitia mfuko wa maji.

Mkazi wa kijiji cha Mkalala kata ya Mninga Asia Chelesi,ameiomba serikali kuwa karibu na mkandarasi ili aweze kukamilisha ujenzi wa mradi huo haraka kwa kuwa wamechoka kuendelea kutembea umbali mrefu na makazi yao kwenda kutafuta maji.

Kaimu Afisa Mtendaji wa kata ya Mninga Octova Malangalila alisema,mradi huo una manufaa makubwa kwa wananchi wa vijiji vinavyounda kata hiyo ndiyo, maana hadi sasa hakuna matukio ya wizi na uharibifu wa vifaa.

Malangalila,ameishukuru serikali kuanza kutekeleza mradi huo kwani utamaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji iliyokuwepo muda mrefu ambayo imesababisha hata baadhi ya shughuli za maendeleo kusua sua.
shehena ya mabomba yatakayotumika katika mradi wa maji katika kijiji cha Mkalala wilayani Mufindi.
 Tenki la maji lenye uwezo wa kuchukua lita linalojengwa katika mradi wa maji kijiji cha Mkalala wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira(Ruwasa)Mhandisi Clement Kivegalo katikati na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ruwasa Mhandisi Ndele Mengo kulia wakikagua sehemu ya mabomba ya maji yatakayotumika kwenye ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Mkalala wilayani Mufindi, wa kwanza kushoto meneja wa Ruwasa mkoa wa Iringa Mhandisi
Joyce Bahati.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad