
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Mradi wa USAID AFYA YANGU kwenye
ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Mei 6, 2022. Wengine pichani kutoka
kushoto ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi
Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Kate
Somvongsiri, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Balozi wa Marekani nchini
Dkt. Donald Wright , Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka na kulia ni
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi
Maalum, Dkt. Zainab Chaula.

Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akionesha bango baada ya kuzindua Mradi wa USAID
AFYA YANGU kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Mei 6, 2022. Wengine
pichani kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Kate Somvongsiri,
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald
Wright na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka.

(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI
Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza rasilimali zote zinazotolewa kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya afya zitumike kwa uangalifu na
uaminifu ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanatekelezwa na kuleta
tija kwa wananchi.
Ametoa agizo hilo leo
(Ijumaa, Mei 6, 2022) wakati akizindua mradi wa USAID Afya Yangu ama
Comprehensive Client Centered Health Program (C3HP) unaotekelezwa na
Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Watu wa Marekani (USAID Tanzania).
“Mamlaka
za Serikali za Mitaa toeni ushirikiano wote utakaofanikisha utekelezaji
wa mradi huu kwa mafanikio. Watendaji wabadhirifu wasipewe nafasi
kuhujumu mradi huu. Viongozi, fuatilieni mara kwa mara ili kuhakikisha
malengo ya mradi yanatekelezwa na kuleta tija.”
Amesema
azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia
Suluhu Hassan ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya,
hivyo imeendelea kuweka kipaumbele katika sekta ya afya kwa kutekeleza
mikakati ya kuimarisha utoaji wa huduma. “Mojawapo ya vipaumbele ni
mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.”
Waziri Mkuu
amesema kuwa jitihada mbalimbali za Serikali pamoja na wadau zimeanza
kuzaa matunda, ambapo katika kutekeleza mkakati wa kupunguza maambukizi
ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa kiasi kikubwa kiwango cha
maambukizi kimeshuka kutoka asilimia 13.5 mwaka 2015 hadi asilimia saba
mwaka 2020.
Mheshimiwa Majaliwa amesema
Serikali imeweka kipaumbele katika kupambana na vifo vinavyotokana na
uzazi na watoto wachanga kwa kutekeleza Mpango wa Kuimarisha Afya ya
Msingi. “Mpango huu ulitutaka kuongeza vituo vya afya ili kila kata iwe
na kituo cha afya.”
“Hadi kufikia mwaka 2020
jumla ya vituo vya afya 487 na hospitali za wilaya 102 zimejengwa au
kukarabatiwa ili kutoa huduma za afya ya msingi ikiwemo ya upasuaji wa
kumtoa mtoto tumboni, haya ni mafanikio makubwa sana.”
Amesema
ongezeko la vituo hivyo linaifanya Tanzania kuwa kati ya nchi zilizo
chini ya Jangwa la Sahara ambazo zimefikia kwa kiasi kikubwa vigezo vya
Umoja wa Mataifa vya Utoaji Huduma za Dharura za Uzazi na Mtoto Mchanga.
Ametaja
vigezo hivyo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma za dharura kwa
kuzingatia idadi ya watu na jiografia ya maeneo, kiwango kikubwa cha
akinamama wanaojifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma na kiwango cha
kuridhisha cha wajawazito.
Akizungumzia kuhusu
mradi wa USAID Afya Yangu amesema amefurahishwa sana na mradi huo ambao
una nia ya kuongeza upatikanaji na matumizi ya huduma ya afya ya uzazi
hapa nchini ambao unalenga kumuwezesha mtu binafsi aweze kuimarisha
uwezo wake wa kuwa na tabia chanya katika kuzingatia mahitaji ya afya
yake.
Malengo mengine ni kumuwezesha mtu
kujihudumia mwenyewe pamoja na upatikanaji wa huduma ya afya ya uzazi na
mtoto kwa mtu binafsi. Pia, umelenga kuweka mazingira wezeshi ya
utoaji wa huduma bora za afya ya uzazi na mtoto.
Kwa
upande wake, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Serikali ya Watu wa
Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) imetoa
ufadhili wa miradi mitatu ya USAID Afya Yangu kwa Mashirika ya Elizabeth
Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF), Jhpiego, Deloitte kwa ajili
ya kutekeleza mradi huo wa Comprehensive Client Centered Health Program
(C3HP) unaotekelezwa katika mikoa 21 ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa
kipindi cha miaka mitano kuanzia Novemba 2021 hadi Oktoba 2027.
Pia,
Waziri Ummy ametumia fursa hiyo kulishukuru Shirika la Maendeleo ya
Kimataifa la Watu wa Marekani (USAID Tanzania) kwa kuunga mkono juhudi
za Serikali katika kuimarisha huduma za afya nchini.
Amesema
shirika hilo limekuwa likishirikiana na Serikali katika kutoa ufadhili
wa utekelezaji wa afua za VVU/UKIMWI, Kifua Kikuu, Uzazi wa Mpango,
pamoja na Afya ya Mama na Mtoto zitakazokuwa zinatekelezwa na miradi
hiyo ya USAID Afya Yangu ambayo wanufaika wa mwisho kabisa ni Watanzania
hasa wale walio maeneo ya pembezoni ya mikoa ambayo miradi hii
itatekelezwa.
Kwa upande wake Balozi wa
Marekani Nchini Tanzania Dkt. Donald Wright, amesema urafiki na
Ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani umeendelea kukua na kuimarika
siku hadi siku jambo ambalo linachangia Ushirikiano wa kimaendeleo baina
ya Nchi ya hizo.
“Marekani imeendelea kuwa
rafiki na mdau mkubwa wa maendeleo kwa Watanzania, uzinduzi wa mradi huu
ni kithibitisho cha namna ambavyo tumejikita katika kuhakikisha
tunashirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha tunaleta
mabadiliko chanya kwenye maisha ya Watanzania katika Sekta za Afya,
Miundombinu, na Uchumi.”
Awali, Mkurugenzi
Mkazi wa USAID, Kate Somvongsiri alisema USAID Afya Yangu ni programu ya
miaka mitano, inayojumuisha miradi itakayoshughulikia masuala ya VVU,
Kifua Kikuu, Uzazi wa Mpango, Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto na Vijana.
Alisema
takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ina takriban watu milioni 1.7
wanaoishi na VVU, inakabiliwa na changamoto za afya ya uzazi, watoto
wachanga na vijana na inaendelea kuwa na kesi za UVIKO-19 ambazo
zimeathiri makundi hatarishi kama vile akina mama wajawazito na watu
wanaoishi na VVU.
"Serikali ya Marekani
imedhamiria kushirikiana na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya
na Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika ngazi ya
Serikali kuu na mikoa kutoa huduma bora za kinga, matunzo na matibabu ya
VVU.
No comments:
Post a Comment