HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, February 8, 2022

JAJI MAHAKAMA KUU YA TANZANIA AHIMIZA MAHAKIMU KUAMUA MASHAURI BILA WOGA, UPENDELEO

 Na Faustine Kapama – Mahakama, Lushoto

JAJI wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Edwin Kakolaki amewahimiza Mahakimu kuutumia vizuri uhuru walionao katika kuamua mashauri yanayoletwa mbele yao bila woga wala kuegemea upande wowote ili kuleta amani, upendo, matumaini na faraja kwa watu nje na ndani ya Mahakama.

Mhe. Kakolaki ametoa wito huo leo tarehe 7 Februari, 2022 alipokuwa akifungua mafunzo ya uendeshaji wa mashauri ya rushwa na urejeshaji mali kwa Mahakimu Wakazi 200 yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA). Mafunzo hayo ya siku tano yanadhaminiwa na serikali kupitia Programu ya Kitaifa ya Kuzijengea Uwezo Taasisi za Umma Zinazohusika na Kuzuia na Kupambana na Rushwa (BSAAT).

“Utekelezaji wa majukumu yote yanayosaidia katika utoaji haki umo mikononi mwenu. Nawasihi kuutumia vizuri uhuru wenu kama Mahakimu na uhuru wa Mahakama katika kuamua shauri lililopo mbele yenu bila woga na kutoegemea upande wowote. Mkiwa imara na madhubuti katika kazi zenu, mtakuwa mmetimiza malengo ya Mahakama na ya nchi. Nitumie fursa hii kusisitiza kwamba muwe mstari wa mbele katika kuleta amani, upendo, matumaini na faraja kwa watu mahakamani na nje ya Mahakama,” amesema.

Jaji Kakolaki, ambaye alikuwa mgeni rasmi amebainisha kuwa Mahakama imekabidhiwa dhamana na jukumu zito la kuhakikisha kuwa jamii inapata huduma iliyokusudiwa, hivyo Mahakimu kama watumishi wake wanatakiwa kuzingatia sheria, kanuni, na miongozo mbalimbali inayosimamia uwajibikaji wakati wa kutekeleza majukumu yao kikazi.

“Ni jukumu lenu kufuata kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya kiutumishi kuhusu maadili mema. Kazi yenu ya kutoa haki iende sambamba na uwepo wa maadili mema. Katika maisha yenu ya utendaji kazi, muendelee kuwa kioo na kielelezo cha maadili mema, hofu ya Mungu na kutotengeneza mazingira ya kuwa na tabia zisizofaa katika utumishi wa umma,” amesema.

Jaji Kakolaki amebainisha kuwa kesi za rushwa na utakatishaji fedha zipo katika maeneo mengi ikiwemo uchumi na elimu, hivyo Mahakimu Wakazi hawana budi kuwa na uelewa, maarifa na uwezo wa kukabiliana nazo, hasa kwenye suala la kusikiliza na kufikia uamuzi.

“Miongoni mwa madhara yanayoweza kusababishwa na rushwa pamoja na utakatishaji fedha ni kuzuia ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja, jamii na taifa zima kwa ujumla. Kwa kuzingatia uwepo wa vitendo vya rushwa na utakatishaji fedha katika Idara na Taasisi mbalimbali za umma na binafsi, Serikali imeweka mfumo wa kuzuia na kupambana na vitendo hivyo ili kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa zinafikia malengo ya kuwahudumia Watanzania kwa haki na usawa,” amesema.

Akitoa neno la utangulizi katika mafunzo hayo, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma aliwakumbusha Mahakamu hao kuwa kazi ya kutoa haki ni kazi ya Mungu na kwa kuwa yeye ni mtakatifu ni lazima kuifanya kwa uadilifu na utakatifu wake.

“Hoja hii ndiyo imelazimu uongozi wa Mahakama kutoa kibali ili mafunzo haya yafanyike. Kwa msingi huo, kupambana na rushwa, utakatishaji fedha na uhujumu uchumi kwa ujumla, si tu unataka weledi wa hali ya juu, lakini pia unahitaji ujuzi na uelewa wa kutosha wa sheria na kanuni zinazohusika na masuala haya,” amesema.

Kwa mujibu wa Mhe. Chuma, rushwa, uhujumu uchumi na utakatishaji fedha ni hatarishi kwenye jamii pamoja na maendeleo ya taifa kwa ujumla, hivyo washiriki hawana budi kusikiliza kwa makini na kushiriki kikamilifu wakati wote wa mafunzo ili kuungana na jitihada zinazoendelea za Mahakama ya Tanzania za kujenga imani na kuwa karibu zaidi na wananchi.

“Ni dhahiri kwamba kila mmoja wetu akiwa na utamaduni wa uadilifu, uchumi wetu utakua, sekta ya umma itakuwa bora na kustawi na taasisi zetu zitaaminika zaidi. Vilevile jamii zetu zitafaidi matokeo ya ukuaji wa uchumi. Zaidi, ustawi wa watu wetu unategemea sana uadilifu wetu na wa viongozi wenzetu. Kwa ufupi uadilifu utaboresha maisha ya watu,” amesema.

Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha aliwapitisha washiriki wa mafunzo hayo katika maelezo mafupi juu ya Programu ya BSAAT ambayo imejikita katika kujenga mfumo endelevu wa mapambano dhidi ya rushwa unaofadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia Ofisi ya “Foreign Commonwealth Development (FCDO)” kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya na hapa nchini kuratibiwa na Ofisi ya Rais, IKULU.

“Programu hii ni ya miaka mitano na imeanza kutekelezwa mwaka 2018/2019 – 2022/2023 kwa kunufaisha taasisi na wizara mbalimbali, ambapo Mahakama ya Tanzania wakiwa ni moja wapo. Programu hii inatekeleza malengo yake makuu, ikiwemo kupunguza vitendo vya rushwa kama kikwazo cha kupunguza kiwango cha umasikini kwa Watanzania, kuboresha uadilifu, kuboresha uwezo na uratibu wa mfumo wa haki jinai katika vita dhidi ya vitendo vya rushwa na kuongeza imani kwa umma juu ya utendaji kazi wa Mahakama,” amesema.

Kwa mujibu wa Bw. Magoha, tangu program hiyo ianze kutekelezwa, kumekuwa na viashiria mbalimbali vya mafanikio ambavyo vimeonekana katika maeneo mbalimbali kama kuongezeka kwa utoaji wa taarifa za ubadhirifu au vitendo vya rushwa kwenye mamlaka husika, kupunguza muda wa usikilizwaji wa mashauri ya rushwa na urejeshaji wa mali.

Wakati wote wa mafunzo, washiriki watapitishwa katika mada mbambali zilizoandaliwa na Wawezeshaji mahiri katika maeneo juu ya Rushwa, Utakatishaji Fedha na Urejeshaji Mali. Wawezeshaji hao ni pamoja na Mhe. Kakolaki na Majaji wengine wawili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt Zainab Mango na Mhe. Awamu Mbagwa pamoja na Naibu Msajili, Mhe. Godfrey Isaya, ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma akitoa neno la utangulizi katika mafunzo hayo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Edwin Kakolaki akisisitiza jambo alipokuwa akifungua mafunzo leo tarehe 7 Februari, 2022 juu ya uendeshaji wa mashauri ya rushwa na urejeshaji mali kwa Mahakimu Wakazi 200 yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha akitoa maelezo mafupi juu ya Programu ya Kitaifa ya Kuzijengea Uwezo Taasisi za Umma Zinazohusika na Kuzuia na Kupambana na Rushwa (BSAAT) kwa Mahakimu wanaoshiriki mafunzo hayo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Edwin Kakolaki akisisitiza jambo alipokuwa akiwasilisha mada kwenye mafunzo leo tarehe 7 Februari, 2022.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt Zainab Mango akiwapitisha washiriki wa mafunzo kwenye mada mojawapo zilizowasilishwa juu ya Utawala wa Kisheria wa Kimataifa juu ya Rushwa.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Awamu Mbagwa akifafanua jambo wakati wa uwasilishaji wa mada mbalimbali kwenye mafunzo hayo.
Naibu Msajili, Mhe. Godfrey Isaya, ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akiwasilisha mada kwenye mafunzo.
Mratibu wa mafunzo, Mhe. Victor Bigambo akieleza jambo kabla ya kumkaribisha mmoja wa Wawezeshaji ili kutoa mada katika mafunzo hayo.


Meza kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Zainab Mongo (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Sekretarieti (waliosimama nyuma) wanaoratibu mafunzo hayo.

Wawezeshaji wa mafunzo wakichambua na kufuatilia hoja mbalimbali.
Sehemu ya Mahakimu Wakazi (juu na chini) wanaoshiriki mafunzo hayo.

Meza kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Zainab Mongo (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Mahakimu Wakazi (juu na picha mbili chini) wanaoshiriki katika mafunzo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad