HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 20, 2021

Idadi kubwa ya watu sio kigezo cha kuwa na uchumi imara

 

Mkurugenzi wa Tanzanian Men As Equal Partiners in Delvelomepment(TMEPiD) Dkt.Cuthbert Maendaenda akizungumza na waandishi wa habari na Wahariri kuhusiana Masoko Jumuishi ya Uzazi wa Mpango mara baada ya kuwajengea uwezo katika Mkutano uliofanyika Morogoro.
Meneja wa Utetezi wa Shirika la Tanzania Communication and Development Centre (TCDC), James Mlali akizungumza na waandishi habari kuhusiana uzazi wa mpango katika semina iliyoandaliwa na TMEPiD kwa ufadhili wa UNFPA  iliyofanyika mkoani Morogoro.
Baadhi ya Wahariri na Waandishi wa Habari wakiwa katika mkutano.
Picha ya pamoja ya waandishi wa habari na wahariri mara baada ya kupata mafunzo ya juu hali ya uzazi wa mpango nchini.

*Tafiti zinaonyesha uzazi wa mpango ukitumika vizuri vifo vya mama na mtoto vitapungua.
*TMEPiD yaja na ushauri wa masoko jumuishi ya upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango.

Na Chalila Kibuda ,Michuzi TV
IDADI ya watu kuwa kubwa sio kigezo cha kuwa na maendeleo kwani baadhi ya nchi zimekuwa na idadi ndogo za watu lakini hazijaweza kupata maendeleo .

Suala la uzazi wa  mpango haliko kwa ajili ya kufanya  idadi ya watu kuwa ndogo bali ni kufanya kuwepo kwa idadi ambayo serikali inaweza kupanga bajeti pamoja na kuwa na idadi kubwa ya watu wenaozalisha huku  idadi ndogo ikiwa tegemezi.

Uzazi wa mpango ni hiari ya mtu kuamua muda gani wa kuweza kupata mtoto na mtu huyo kuamua ni mtu gani wa kuamua kupata naye mtoto kwa ajili ya kuweza mtoto huo kupata huduma zote katika ukuaji na kulinda afya ya mama.


Meneja wa Utetezi wa Shirika la Tanzania Communication and Development Centre (TCDC), James Mlali anasema huduma za uzazi wa mpango ni muhimu zaidi katika kuboresha afya ya mama, afya ya mtoto ikiwemo kuleta maendeleo kwa ujumla kwa kusaidia serikali kupanga bajeti ambayo inaweza kutusheleza.

Meneja wa Utetezi wa Shirika la Tanzania Communication and Development Centre (TCDC), James Mlali akizungumza na waandishi habari kuhusiana uzazi wa mpango katika semina iliyoandaliwa na TMEPiD kwa ufadhili wa UNFPA  iliyofanyika mkoani Morogoro

Mlali anasema, umuhimu huo, juhudi zinapaswa kufanywa ili kuongeza huduma hizo nchini kuanzia maeneo yote ya vijijini na mijini pamoja na kuruhusu sekta binafsi kushiriki katika kutoa huduma jumuishi ya soko la huduma za mpango.

Mlali aliyasema hayo katika Semina juu ya Mbinu Jumuishi za Soko la Huduma za Uzazi wa Mpango zinazoweza kupatikana kiurahisi kwa kila anayehitaji na kuwa endelevu kuliko ilivyo sasa.

Semina hiyo ya Desemba 14 hadi 16, 2021 ambayo iliwakutanisha pamoja wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini ilifanyika mjini Morogoro ambapo iliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali ambalo limejikita katika kukuza ushiriki wa wanaume katika Afya na Haki za Ujinsia na Uzazi , afya ya mama na mtoto pamoja na kukuza usawa wa kijinsia katika shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi la Tanzania Men as Equal Partners in Development (TMEPiD) na kufadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshugulikia Idadi ya Watu (UNFPA) pamoja na wengine katika utetezi wa uzazi afua za uzazi wa mpango nchini.

Amesema huduma za uzazi wa mpango nchini bado kuna haja ya kufanya kazi zaidi,ili tuweze kupiga hatua, kulingana na taarifa rasmi za afya na idadi ya watu za mwaka 2015 hadi 2016 ya Tanzania Demographic and Health Survey, tunaona kuwa watumiaji wa huduma za uzazi wa mpango walifikia asilimia 32 katika kila asilimia 100, ambacho ni kiwango kidogo, hawajafikia hata theluthi.

Amesema matumizi ya kila mwaka zinaonyesha kuwa, kufikia mwaka 2020 idadi hiyo ilikuwa imefikia asilimia 41 ambapo malengo yake ni kuhakikisha watumiaji hao wanafikia asilimia 47 mwaka 2023.

Amesema kuweza kufikia asilimia 47 jitihada zinahitajika kwa serikali kufanya zaidi kwa kushirikisha wadau kufanya kazi zaidi ili watumiaji wa huduma za uzazi wa mpango waweze kuongezeka nchini ikiwa pamoja na kusogeza huduma kila sehemu ambapo huduma hizo zinaweza kukaa ikiwemo Famasi na Maduka ya Dawa Muhimu kama iliyo kwa kwa huduma za Kondomu.

"Lengo sio kuwa na idadi kubwa ya watumiaji, bali ni kufanya kuongezeka kwa huduma za uzazi wa mpango kurahisisha watu kuzifikia na kuweza kutoa mchango mkubwa sana katika afya ya mama, afya ya mtoto na maendeleo kwa ujumla,"amesema Mlali.

Amesema kuwa kutokana na huduma hizo kupatikana kidogo karibu ya mimba zote zinazotungwa baadhi ya mimba ambazo hazikutarajiwa kuwa wanapanga kuwa wazae, wengine wana mtoto mdogo, wengine umri umeenda sana, hana malengo ya kuzaa, lakini baada ya kushiriki tendo wanajikuta wamepata mtoto.

"Tafiti Ulimwengunj zinaonyesha kuwa matumizi ya huduma za uzazi wa mpango zikifanyika vizuri, vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi vinaweza kupungua kwa asilimia 44,na vifo vya watoto vinaweza kupungua kwa asilimia 35.

"Taifa linahitaji nguvu kazi kubwa, linahitaji wanawake wenye afya njema, linahitaji watoto wakue vizuri, wasikatishwe au maisha yao yasikatishwe, katika umri mdogo waweze kukuwa ili waweze kuwa sehemu ya nguvu kazi ya Taifa.

Amesema huduma za uzazi wa mpango zina mchango mkubwa katika maendeleo kwa sababu ndizo ambazo zinasaidia familia, au watu binafsi kuamua idadi ya watoto ambao wanataka kuzaa, wawazae kwa wakati gani, wawaachanishe kwa umri gani kati ya mtoto na mtoto na hizo ndiyo kanuni bora kwa ajili ya afya mama na mtoto kwa maendeleo ya nchi.

Mlali anasema kuwa, Serikali inapaswa kuelekeza bajeti ya kutosha kwenye masuala yahusuyo uzazi wa mpango na inapaswa kupewa kipaumbele kikubwa, pia jamii ambazo zina fikira potofu kuhusu uzazi wa mpango zinapaswa kuachana nazo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TMEPiD, Dkt.Cuthbert Maendaenda katika semina hiyo amesema kuwa, kila mtu ana haki ya kuamua ni wakati gani wa kuzaa na wakati gani si wa kuzaa kutokana mipango katika familia.

Amesema taasisi yaob inahusika na utetezi na kuimarisha elimu afya ya uzazi katika jamii hasa ikiwalenga wanaume, kwa nini tunawalenga wanaume? Kwa sababu mbalimbali za kijamii, walikuwa ni kundi ambalo limewekwa pembeni katika masuala ya haki ya uzazi pamoja na uzazi wa mpango

"Ukitamka sema uzazi wa mpango moja kwa moja zinawalenga wanawake, njia za uzazi wa mpango nyingi zinawalenga wanawake, huduma zinazotolewa mahali zinawalenga mama na mtoto, hivyo wanaume walikuwa wanakaa pembeni.Tukiangalia kimila, wanaume ndiyo wafanya maamuzi,kama ni mzazi mtoto apatikane lini, wapatikane watoto wangapi, maamuzi mara nyingi yanategemea wanaume, mila zimewapa hiyo nguvu au upendeleo.

"Kwa hiyo, kwa sasa Taasisi tumejikita katika kujiimarisha kwenye utetezi wa afya ya uzazi wa mpango, tukisaidiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu hapa Tanzania (UNFPA)na kwa sababu tayari Serikali imeshajiwekea malengo, Malengo ya Uzazi wa Mpango 2030, Serikali imepania kupanua matumizi ya huduma za uzazi wa mpango.

Dk.Maendaenda amesema  kupanua wigo wa wananchi kuweza kupata huduma za uzazi wa mpango, sasa katika kufanya hivyo, tukajikuta miaka mingi mtu akitaka kupata huduma ya uzazi wa mpango alipaswa kwenda kiliniki, usipokwenda kiliniki hauwezi kupata huduma,lakini pia kuna watu wengine wanapata changamoto  ya kupata huduma, ukienda kiliniki au zahanati huduma hamna, kwenye jamii zingine ambapo vijana ambao ndiyo wapo kwa wingi zaidi, suala la uhusiano wamekuwa wakishindwa kufikia hizo huduma kwa sababu ya hofu ya wazazi wao, ndugu zao kuwa wanaweza kukutana nao na kuaza kuhojiana juu ya kilichowapeleka .
"Tumekuja na masoko jumuishi (TMA) katika hili tunachotaka ni huduma ya uzazi wa mpango zipatikane kila mahali, na kupitia wadau si kwenda kliniki, tukiangalia huko miaka ya nyuma hata kupata huduma ya baba, mpira wa kiume au kondomu ilikuwa lazima uende kliniki, lakini kwa sasa ukitaka kondomu inapatikana kila mahali ikiwemo katika maduka ya rejareja.

"Mtu hawezi kuacha kutumia kondomu, kwa sababu inapatikana kila mahali, na kwa sababu tunataka huduma nyingine zipatikane kila mahali za uzazi wa mpango ikiwemo katika famasi na maeneo mengine ili ziweze kupatikana kwa wingi hususani mashirika yanayotoa huduma hizo. Kwa hiyo mtu hawezi kuacha kutumia kondomu,"amesema Dkt.Maendaenda.

Amesema Taifa litapata faida nyingi kupitia upangaji salama wa uzazi wa mpango na hakutakuwa na kisingizio cha mtu kushindwa kuitumia huduma hiyo kutokana na kuweza mazingira mazuri ya huduma hizo.

"Tunataka huduma za uzazi wa mpango zipatikane kila mahali wakati wowote, kwa mfano katika maduka ya kutolea huduma za dawa kwa kuwapa mafunzo,mashirika kama TMARK,PSI ambao wapo mitaani, kwa hiyo, mwanamke au mwanaume akitaka huduma asilazimishwe, kama tumeweza kuzileta kondomu zikajaa, basi itafutwe njia nyingine ya kuhakikisha huduma zingine za uzazi wa mpango zinasambaa kila mahali.

Aidha amesema kuwa, idadi kubwa ya watu wanaoishi mijini wana uwezo hivyo inawezekana wakawa wanapatiwa huduma hizo kwa kugharamia ili kipato kitakachopatikana kiweze kupeleka huduma hiyo kwa wingi huko vijijini.

"Hii ni faida kubwa ya kuhakikisha maeneo ya vijijini huduma zinajaa, lakini pia tunatetea kwamba haya mashirika ya Bima na wenyewe katika huduma wanazotoa waweke suala la uzazi wa mpango ili kama huduma hiyo inatolewa katika vituo binafsi, waweze kufanya maamuzi ya kwenda kutumia huduma anapotaka,

"Pia itaweza kusaidia kuongeza usiri, kwa mtu ambaye anataka huduma hiyo,anaweza kuipata sehemu yoyote bila kukaa foleni,kwa hiyo unajua mimi ninatumia huduma fulani unaenda kwenye duka la dawa kupata huduma, hivyo kama mwingine anatumia kitanzi badala ya kwenda kliniki na kuambiwa kuwa havipo, ataweza kwenda kununua na kuja kuwekewa katika kituo cha afya.

"Pia itatoa nafasi kwa watumiaji wa huduma ya uzazi wa mpango mfano wanaume kupata nafasi ya kukaa na wahudumu kupata ushauri kabla ya kufanya maamuzi,"amesema.

Dkt.Maendaenda amesema kuwa, pia elimu kuhusu huduma za uzazi wa mpango iendelee kutolewa katika maeneo yote nchini ili kupunguza changamoto kwa baadhi ya makundi hususani vijana.

Amebainisha sasa huduma za uzazi wa mpango ni bure na zinatolewa na Serikali, lakini wakati mwingine bajeti ya Serikali inakuwa haitoshelezi soko la wahitaji.

Amesema tafiti zinaonesha kuwa, kuna njia nyingi za uzazi wa mpango ambazo zinaweza kutumiwa na mtu au wenza waweze kusubiri,kuchelewesha au kupunguza idadi ya watoto watakaowazaa. Miongoni mwa njia hizo kuna njia za muda mfupi, muda mrefu na za kudumu.

Amesema njia za kisasa za uzazi wa mpango ambazo unaweza kuzibadilisha, unaweza kupata ujauzito pindi utakapoacha kuzitumia.

Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa, njia hizi ni nzuri kwa mama anayetaka kupata ujauzito baada ya miaka miwili baada ya kujifungua na miongoni mwa njia hizo ni vichecheo ambavyo ni sawa na vichocheo vya kawaida

vilivyomo kwenye mwili wa mwanamke, njia ya vidonge ambavyo hutumiwa na wanawake kila siku.

Njia ya nyingine ni ya sindano ambapo mama huchoma sindano kila baada ya miezi mitatu,njia ya dharura ya vidonge vya uzazi wa mpango ambavyo huwa vinamezwa na mama ili kuzuia kupata mimba kwa mama anayeshiriki tendo la ndoa au ngono bila kutumia kinga yeyote.




Hivi vinaweza kuzuia mimba hadi siku tano baada ya kujamiana, kondomu za kike na kiume nazo ni muhimu kutumia ipasavyo kila unapofanya tendo la ndoa au ngono. Hii ni njia ya pekee ambayo pia inazuia maambukizi ya VVU na magonjwa ya zinaa.

Dk.Maendaenda inawezekana ikiwa mama anaufahamu mzunguko mzima wa siku zake za hedhi na kujua ni zipi siku za hatari za kushika mimba hiyi mama na mwenza wake wanatakiwa kuacha kabisa kufanya tendo la ndoa au ngono siku hizo za hatari.

Pia kufunga kizazi kwa mwanaume ambapo njia hii inahusisha upasuaji mdogo ambapo mirija ya uzazi ya mwanaume ukatwa au kufungwa hivyo kuzuia yai kusafiri na kukutana na shahawa ambapo licha ya kufanya hivyo mwanaume anaendelea kuwa na hamu ya kujamiiana na kutoa mbegu, lakini mbegu zake hazitaweza kutunga mimba.

Kufunga kizazi kwa mwanamke ni njia inahusisha upasuaji mdogo inafanyika kwa kuziba au kukata mirija ya kizazi kuzuia yai kukutana na mbegu, mwanamke ataendelea kuwa na hamu ya kujamiiana na kuona siku zake za hedhi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad