BAADHI YA WAISLAMU WAMEASWA KUACHA KULALAMIKA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 2, 2021

BAADHI YA WAISLAMU WAMEASWA KUACHA KULALAMIKA

NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza ,limewataka waumini wa dini ya Kiislamu kuacha kulalamika na kuilaumu serikali, wafanye shughuli za maendeleo,wasisumbuliwe na vyeo (madaraka).

Pia limewataka kusomesha watoto wao na kufanya mambo ya maendeleo badala ya kusubiri hisani ya serikali kwa kuwa yanayofanywa na BAKWATA, madhehebu mengine yametangulia,hivyo wakipuuza watabaki nyuma. 

Rai hiyo ilitolewa jana na Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke, alipozungumza na waumini wa Msikiti wa Jihad Nyabusalu, Kiseke katika Wilaya ya Ilemela,kwenye Sherehe ya Maulidi ya Mtume Muhammad S.A.W.

Alisema Waislamu wanapaswa kujitambua kwa kuchangia na kufanya maendeleo kwa maslahi yao badala ya kulalamika na kuilaumu serikali.

“Hatuwezi kuwa watu wa kulalamika tu,tufanye maendeleo ya waislamu, haiwezekani serikali ichukue sh. milioni 4 itupe tu, za nini? Tuseme ukweli, serikali itatuunga mkono kama kuna jambo la maendeleo,hivyo tufute mambo ya kulalamika,”alisema Sheikhe Kabeke.

Alitahadharisha Mwanza kuna tatizo kubwa la ushirikiano kwenye elimu bado hawajaitumika vizuri na kusistiza ujenzi wa vituo vya afya unaoendelea,waendeleze mshikamano na kusameheana kwani hakuna mkamilifu,”alishauri.

Naye Sheikhe wa Wilaya ya Tabora, Sheikhe Ramadhan Rashid, alimmwagia sifa Sheikhe Kabeke kwa anayoyafanya ni makubwa ili kuchochea maendeleo, hafanyi ili kulinda nafasi yake bali maslahi ya waislamu na kwa jinsi hiyo Mwanza itabadilika na itaendelea kwa sababu hafanyi maigizo kuhamasisha maendeleo.

Mgeni rasmi kwenye maulidi hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Massala, alisema lipo jambo la kujifunza kwa Sheikhe Kabeke,amekuwa mwanaharakati wa maendeleo na dini hata serikali inapokwama amekuwa kinara wa kuikwamua kwenye changamoto zinazoikabili likiwemo suala la chanjo ya Uviko-19.

Alisema jamii kupitia kwa kiongozi huyo wa kiroho ilihamasika kuchanja baada ya upotoshaji uliofanywa na watu wasioitakia mema nchi yetu na kuwaomba viongozi wengine wa dini na kisiasa kuendelea kuhamasisha chanjo ya kujikinga na ugonjwa huo na kuwataka waislamu waitumie tunu hiyo, wasiyaone mapungufu bali mazuri yake kwa maslahi mapana ya uislamu.

“Sheikhe Kabeke umefanya kazi kubwa ya kuhamasisha ujenzi wa vituo vya afya,unahisi unawajengea waislamu tu bali Watanzania wote na serikali hatutakuacha pekee yako, tutakuunga mkono kutafuta matofali ya ujenzi huo,binafsi nitakuunga mkono kwenye jambo hili la heri, pia ” alisema Massala.
Aliongeza kuwa “waislamu tusione shida kwenye suala la maendeleo,waliofanikiwa walijitoa kwa fedha na nguvu zao (kusomba maji ama kufyatua matofali), tusilalamike,tunapoteza muda mwingi na hakuna mtu anatuonea kwani zipo shule nyingi za dini na haya yanayofanyika yawe chachu ili mwisho tusikwame kwenye maendeleo.”

Aidha alisema ujenzi wa vituo vya afya vya waislamu unaunga mkono jitihada za serikali ambapo imetoa sh. milioni 250 za tozo kujenga kituo kama hicho Kayenze, hivyo wamwombee Rais Samia Suluhu Hassan afya njema kwani anayoyafanya yanagusa maisha ya Watanzania.
Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke, akizungumza jana na waumini wa dini ya Kiislamu wakati wa maulidi na harambee ya kuchangia ununuzi wa kiwanja cha upanuzi wa Msikiti wa Jihad, Nyabusalu, Kiseke wilayani Ilemela.
Sheikhe Mohamed Mbega , kutoka kushoto wa tatu akizungumza jana kwenye eneo la ujenzi wa kituo cha afya Kiseke,wilayani Ilemela, kinachojengwa kwa nguvu na michango ya Waislamu.Wa nne kutoka kushoto ni Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad