DROO ya Makundi ya CRDB Bank Taifa Cup 2021 yapangwa - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 29, 2021

DROO ya Makundi ya CRDB Bank Taifa Cup 2021 yapangwa

 
Meneja Uhusiano wa Benki ya CRDB, Kilo Mgaya akionyesha moja ya timu zitakazoshiriki Mashindano ya CRDB Bank Taifa Cup 2021 wakati wa droo ya kuzipanga timu hizo kwa makundi, iliyofanyika kwenye studio za Azam Tv, Tabata jijini Dar es salaam. Wengine pichani kutoka kulia ni Mkuu wa Vipindi vya Michezo wa Azam TV, Michael Maluwe, Kamishna wa Wanawake wa Shikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Agnela Semwaiku pamoja na Mchezaji wa zamani wa Mpira wa Kikapu, Rwehabura Barongo. 

=========   =======   ========

Dar es Salaam 29 Oktoba 2021 – DROO ya makundi ya michuano CRDB Bank Taifa Cup imepangwa ambapo timu 32 zinatarajiwa kupambana katika kinyang'anyiro hicho kinachotarajiwa kuanza tarehe 5 hadi 14 Novemba katika viwanja vya Chinangali, Dodoma.

Akitangaza makundi hayo katika hafla ya kupanga droo hiyo iliyofanyika “MUBASHARA” kupitia channel ya Azam Sports HD 2, Meneja Uhusiano Benki ya CRDB, Kilo Mgaya amesema kwa upande wa timu za wanaume kutakuwa na makundi manne kila kundi likiwa na timu tano hivyo kufanya jumla ya timu 20.

Bingwa mtetezi wa CRDB Bank Taifa Cup kwa upande wa wanaume mwaka jana timu ya mkoa wa Mbeya imepangwa kundi C ikiwa pamoja na timu za CRDB Bank Youth, Iringa, Tabora na Manyara; kundi A zimepangwa timu za Mwanza, Mtwara, Rukwa, Kilimanjaro na Unguja; kundi B zimepangwa timu za Dar es Salaam, Pemba, Shinyanga, Pwani na Kigoma; wakati kundi D, zimepangwa timu za; Dodoma, Simiyu, Tanga, Arusha na Morogoro.

Kwa upande wa wanawake, makundi yalitangazwa na Kamishna wa Wanawake Shirikisho la Mpira wa Kikapu (TBF), Agnela Semwaiko ambaye alisema kwa mwaka huu zimepatikana timu 12 tu za mikoa ambazo zitamegawanywa katika makundi matatu. Semwaiko alisema mwaka huu timu za wanawake zimeongezeka timu 4 kulinganisha na mwaka jana ambapo timu za wanawake zilikuwa 8.
 
Bingwa mtetezi wa CRDB Bank Taifa Cup kwa upande wa wanawake mwaka jana timu ya mkoa wa Dar es Salaam imepangwa kundi B ikiwa pamoja na timu za Mwanza, Arusha na CRDB Bank Youth; kundi A zipo timu za Dodoma, Mtwara, Unguja na Iringa; wakati kundi C, zimepangwa timu za Pemba, Tanga, Mbeya na Pwani.

Akizungumzia kuhusu maandilizi ya CRDB Bank Taifa Cup, Mgaya alisema mpaka sasa hivi tayari kamati ya maandalizi imefikia asilimia 90 na kuahidi kuwa mashindano ya mwaka huu yatakwenda kuandika historia kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika ambapo Benki ya CRDB imetoa udhamini wa Sh. Milioni 300.

“Maandalizi tayari yameshaanza kufanyika katika viwanja vya Chinangali, kuanzia tarehe 3 Novemba 2021 tunatarajia kuanza kupokea timu Dodoma kwa ajili ya kuanza mashindano tarehe 5. Mwaka huu ushindani utakuwa mkubwa sana kwani timu zimejipanga vilivyo,” alisema Mgaya huku akibainisha kuwa jumla ya zawadi ya Sh. Milioni 40 zimetengwa kwa ajili ya washindi katika mashindano ikiwamo zawadi za ufadhili wa masomo “scholarships.”

Naye Msimamizi wa vipindi vya michezo Azam TV, Michael Maluwe amewataka Watanzania kuanza kufuatilia CRDB Bank Taifa Cup 2021 kupitia chaneli ya michezo ya Azam Sports 2, ambapo kimeanzishwa kipindi maalum kuelekea mashindano hayo ya mpira wa kikapu kiitwacho Mchomo. “Azam TV itaweka kambi Dodoma kuwaletea burudani Watanzania wote kuelekea mashindano haya, niwakaribishe Watanzania tujiunge na Azam TV ili kuwashangilia vijana wetu,” alisema Maluwe.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad