Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka akiongea na kamati iliyoundwa kwa ajili ya mapendekezo ya namna bora ya kudhibiti makorongo.
Sehemu ya wajumbe wa kamati iliyoundwa kushughulikia mapendekezo ya namna bora ya kudhibiti makorongo kwenye kikao cha pamoja kujadili njia bora zinazotakiwa kufuatwa kwa mujibu wa sheria kudhibiti makorongo.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka akitoa Elimu kuhusu ufukiaji wa makorongo kwa kutumia taka ngumu kwa mujibu wa sheria ya mazingira.
Eneo lililofukiwa kwa kutumia taka ngumu na udongo kwenye Mtaa wa Kunguru Goba jijini Dar es Salaam.
………………………………………………………………..
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka amewataka wanao ongoa ardhi kwenye makorongo kufuata taratibu za kisheria ili kulinda mazingira yetu na kuhakikisha yako salama.
Ameyasema hayo wakati wa kikao kilichohusisha Watalaamu wa mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC, Wakurugenzi na Maafisa Mazingira wa Manispaa na Jiji wa Mkoa wa Dar es Salaam, wataalamu wa mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shirika la Umeme Tanzania Tanesco na Wananchi wa Goba Mtaa wa Kunguru. Hatua hii ilifikiwa baada ya Wananchi wa Mtaa wa Kunguru Goba Jijini Dar es Salaam kutumia taka ngumu kufukia makorongo bila kufunya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM).
Dkt. Gwamaka amesema taratibu za kisheria zinapaswa kuchukuliwa ili kulinda rasilimali afya za wanadamu na viumbe hai wote.
“Watu wa Jiji na Manispaa wanapaswa kusimamia makorongo yote kwenye maeneo yao, endapo wanataka kuyadhibiti wanatakiwa kufanya tathmini ya Kitaalamu yaani Tathmini ya Athari kwa Mazingira na kushirikisha Wananchi kisha waandae andiko watakalo liwasilisha Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira.
Dkt. Samuel ameongeza kuwa Manispaa inayosimamia zoezi la kufukia makorongo kwenye eneo lake itakuwa na wajibu wa kusimamia shughuli zote zinazofanyika kwenye eneo husika, na wanatakiwa kuanzisha eneo maalumu kwa ajili ya kuchambua taka Vile vile wanapaswa kuweka mfumo maalumu wa ukusanyaji wa taka maji.
Mkuu wa Idara ya Mazingira Manispaa ya Kinondoni Bw. Juvinice Mahuna amesema taka ni fursa ambayo ikitumiwa vizuri inaleta faida kwenye mazingira, mfano ni namna taka ngumu zinavyotumika kudhibiti mmomonyoko kwenye makorongo.
Angela Kabalo ni mhanga wa mmomonyoko wa udongo kwenye korongo la Mtaa wa Kunguru ameishukuru NEMC na Serikali kwa ujumla kwa kutoa Elimu ya taratibu za kufuata kisheria ili mazingira yawe salama na mali za Wananchi kama nyumba zisiathirike na mmomonyoko wa udongo kwenye makorongo.
No comments:
Post a Comment