WAZIRI MHAGAMA AZINDUA MPANGO KAZI WA KUSIKILIZA NA KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO YA WADAU KATIKA SEKTA YA KAZI NA AJIRA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, January 30, 2021

WAZIRI MHAGAMA AZINDUA MPANGO KAZI WA KUSIKILIZA NA KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO YA WADAU KATIKA SEKTA YA KAZI NA AJIRA

 

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.  Jenista Mhagama akikata utepe ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kusikiliza na Kushughulikia Malalamiko ya Wadau katika sekta ya kazi na ajira uliofanyika ukumbi wa mikutano wa NSSF mkoani Morogoro Januari 29, 2021, kulia kwake ni rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, Tumaini Nyamhokya, kushoto kwake ni Mwakilishi wa ILO Bw. Maridadi Phanuel, wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Loata Sanare, wa pili kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Bw. Andrew Massawe na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Dkt. Aggrey Mlimuka.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.  Jenista Mhagama akihutubia wakati wa uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kusikiliza na Kushughulikia Malalamiko ya Wadau katika sekta ya kazi na ajira uliofanyika mkoani Morogoro, Januari 29, 2021.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.  Jenista Mhagama akikabidhi Mpango Kazi wa Kusikiliza na Kushughulikia Malalamiko ya Wadau katika sekta ya kazi na ajira kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Sanare mara baada ya kuuzindua rasmi mpango huo.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Sanare akitoa salamu za mkoa wake wakati wa uzinduzi huo.

Bw.Tumaini Nyamhokya rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi akizungumza masuala ya vyama vya wafanyakazi wakati wa uzinduzi huo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.  Jenista Mhagama akiteta jambo na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, wakati wa hafla ya uzinduzi huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri (ATE) Dkt. Aggrey Mlimuka akitoa salamu wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kusikiliza na Kushughulikia Malalamiko ya Wadau katika sekta ya kazi na ajira.

Mwakilishi kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO) Bw. Maridadi Phanuel akizungumza wakati wa uzinduzi huo.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda akieleza masuala ya Afya na Usalama Mahala Pa Kazi wakati wa uzinduzi wa Mpango huo.

Sehemu ya wadau walioshiriki katika hafla ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kusikiliza na Kushughulikia Malalamiko ya Wadau katika sekta ya kazi na ajira wakifuatilia mkutano huo.

Sehemu ya wadau walioshiriki katika hafla ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kusikiliza na Kushughulikia Malalamiko ya Wadau katika sekta ya kazi na ajira wakifuatilia mkutano huo.

Kamishna wa Kazi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Brigedia Jenerali Francis Mbindi akichangia jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kusikiliza na Kushughulikia Malalamiko ya Wadau katika sekta ya kazi na ajira.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Masha Mshomba akichangia jambo wakati wa hafla hiyo

Mkurugenzi wa uendeshaji kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Bw. Mbaruku Magawa akichangia jambo wakati wa hafla hiyo.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

**********************************************

Na.Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Wazri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.  Jenista Mhagama amezindua Mpango Kazi wa Kusikiliza na Kushughulikia Malalamiko ya Wadau na Kikosi Kazi cha kufanya ukaguzi maalum katika sekta ya kazi na ajira wenye lengo la kutatua changamoto wanazokabiliana nazo na kuhakikisha kunakuwa na mazingira rafiki kwa wafanyakazi, waajiri na wadau wengine wanaohudumiwa na Ofisi yake.

Uzinduzi huo umefanyika tarehe 29 Januari, 2021 katika Ukumbi wa Mikutano wa NSSF uliopo Mkoani Morogoro na kuhudhuriwa na viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loate Sanare, Mkurugenzi wa shirika la Kazi Duniani (ILO),Wakuu wa Taasisi zilizochini ya ofisi hiyo ikiwemo;WCF, NSSF, PSSSF, OSHA na CMA, Viongozi wa vyama vya waajiri, pamoja na Watendaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Wenye ulemavu).

Akizungmza wakati wa uzinduzi huo Waziri amesema uwepo wa mpango huo utasaidia Wafanyakazi, Waajiri na Wananchi kufahamu mamlaka sahihi ya kuwasilisha malalamiko yanayohusu sekta ya kazi na ajira, uwepo wa njia nyepesi ya kushughulikia malalamiko na kero za wadau na kuweka utaratibu rahisi wa kutoa ushauri na elimu.

Mpango unalenga pia, kuwepo kwa njia nyepesi ya utoaji wa ushauri na elimu ya Sheria za Kazi, mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Masuala ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi pamoja na kuisaidia Serikali kuwa karibu na Waajiri na Wafanyakazi.

Aidha alibainisha kuwa, uwepo wa mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025, kwani inaelekeza kuwa Chama kitaisimamia Serikali kuhakikisha inazingatia haki na wajibu wa wafanyakazi na waajiri na kuimarisha taasisi za hifadhi ya jamii.

Waziri Mhagama alieleza kuwa kila mdau katika eneo lake aone umuhimu na tija kubwa katika kuhakikisha wanatatua malalamiko ya wafanyakazi na waajiri kwa wakati na kupunguza gharama zisizo za lazima katika utoaji wa huduma.

“Mpango utasaidia katika kupunguza gharama na muda unaotumika na wadau katika kushughulikia na kufutlia malalamiko yao na hii itarahisisha uwepo wa muda wa kutosha katika kuendelea na kazi za kujenga uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja,”Alisisitiza

Alisema kuwa, kupitia Mpango huu, malalamiko na kero za wafanyakazi na waajiri zitapokelewa kila siku ya Ijumaa ya mwisho wa mwezi katika kituo/ofisi katika kila Mkoa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana kisha Idara ya kazi, mifuko ya Hifadhi ya jamii, Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi pamoja na vyama vya wafanyakazi na waajiri vitatoa majibu na kushauri hatua za kuchukua kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.

Sambamba na hilo, Waziri aliwataka Watendaji wa Ofisi yake kuhakikisha Mpango Kazi huo unatekelezwa ipasavyo kwa kuzingatia umuhimu wake.

“Kila Ofisi itekeleze majukumu yake kwa ufanisi ili kuwaondolea wadau wa sekta ya kazi na ajira changamoto ambazo zilikuwa zikiwakabili katika maeneo yao bila kupotea muda na rasilimali fedha kuzunguka nchi nzima kutafuta haki,”alisisitiza Waziri

Waziri alitumia fursa hiyo pia kuzindua rasmi Mpango wa Ukaguzi Maalum nchini ambao utatekelezwa na kikosi kazi maalum ambacho kitakuwa jumuishi katika kuimarisha utekelezaji wa Sheria za Kazi (Labour Law Compliance) na maeneo watakayokagua ni pamoja na  vibali vya kazi vya raia wa kigeni, vibali vya kazi vya Watanzania katika miradi ya kimkakati kwa lengo la kuhakikisha vibali vinatolewa kwa kada au ujuzi ambao ni adimu katika soko la ndani la ajira na tulionao.

“Hatua hii itawezesha kulinda ajira za Watanzania na kurithisha ujuzi walionao raia wa kigeni kwa wazawa na kuhakikisha mapato ya kodi yanapatikana,”alieleza

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO) Bw. Maridadi Phanuel aliipongeza Serikali kuona haja ya kuwa na mpango huo na kuahidi kuendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa kuzingatia malengo chanya yaliyobeba dhana ya uanzishwaji wake.

Aliongezea kuwa, ILO itaendelea kushirikiana na Serikali na vyama vya waajiri na wafanyakazi kwa kutoa misaada mbalimbali ambayo inasaidia katika mikutano ya Utatu yenye lengo la kutatua changamoto zinazohusu sekta ya kazi na ajira.

“Ni vyema kuwa na mpango huu ambao utasaidiia kuendeleza jitihada za utatuzi wa migogooro mahali pa kazi ili kuendelea na uzalishaji kisha kuleta tija ambayo itachochea uwepo wa maendeleo katika Nyanja mablimbali nchini,”alisema Maridadi

Aliongezea kuwa, ni vyema malalamiko sehemu za kazi yakaendelea kushughulikiwa kwa kuzingatia ni njia bora ya kuwepo kwa mahusiano mazuri ya wafanyakazi na waajiri na ni hatua nzuri yenye nia njema itakayochochea maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad