Jamii
 mkoani Njombe na Tanzania kwa ujumla wametakiwa kuwa na utamaduni wa 
kufanya vipimo vya hali ya lishe angalau mara mbili au tatu kwa mwaka 
ili kufahamu hali yake ya lishe na kumsaidia kufuata njia bora za lishe 
ili kuepuka utapiamlo.
Hayo yamebainishwa na Afisa Mtafiti 
Mwandamizi-Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) 
Bi.Maria Ngilisho kwenye mwendelezo wa maonesho ya Wiki ya Chakula 
Duniani iliyozinduliwa rasmi tarehe 10/10/2020 ambapo  Kitaifa 
maadhimisho haya yanafanyika Mkoani Njombe na yatahitimishwa 16/10/2020.
Bi.Ngilisho
 amesema, moja ya vipimo vinavyoweza kutoa tafsiri ya kuwa na hali nzuri
 ya lishe ni kipimo cha uwiano kati uzito na kimo/urefu ili kupata 
farihisi (Body Mass Index - BMI).
Amesema, kabla ya kufanya 
vipimo vya hali ya lishe katika banda lao, mteja anaeleweshwa namna ya 
kupanda kwenye mizani  (kuvua viatu, kutoa vitu mfukoni kama vile 
funguo, simu na vitu vingine ambayo vinaweza kuongeza uzito wake kama 
vile saa) na kusimama kwenye ubao wa kupimia kimo/urefu (kuvua viatu; 
mgongo kuwa sambamba na ubao; makalio, mabega na kisogo viguse ubao; 
kusimama wima na kuangalia mbele)", alisema Bi. Ngilisho.
Aliendelea
 kwa kusema, baada ya vipimo kuchukuliwa, vinaoanishwa kwa kutumia kadi 
ya farihisi ili kupata tafsiri ya hali yake ya lishe na kupewa ushauri 
stahiki kufuatana na matokeo ya vipimo vyake.
Aidha Bi. Ngilisho 
alisema, katika kurahisisha uelimishaji wa njia sahihi ya kupanga mlo 
kamili kwa jamii ni kutumia dhana ya pitamidi ya chakula (muundo wa 
kabati iliyotenganishwa katika vyumba vitano, chumba kikubwa kikiwa 
chini na kidogo kabisa kikiwa juu). Kila chumba katika piramidi hii kina
 wakilisha kundi moja la chakula, ili kupata/ kuandaa mlo kamilo 
inatakiwa kuchukua angalau chakula kimoja kutoka kwenye kila 
kundi/chumba.
"Kundi la kwanza lina  vyakula vya nafaka (mahindi,
 ngano, ulezi, mtama, uwele, nk.),  mizizi (mihigo, viazi vitamu, viazi 
mvitingo, magimbi, nk.) na ndizi (ndizi mbichi).Kundi la pili lina 
vyakula vya asili ya wanyama (nyama ya ng'ombe, kuku, mbuzi, nk., 
maziwa, mayai, dagaa, samaki na wadudu waliwao kama senene na 
kumbikumbi. Jamii ya mikunde ni kama maharage, njegere, mbaazi, kunde, 
choroko, soya, nk.). 
Kundi la tatu ni la mboga za majani (mchicha, 
spinachi, chinise, figiri, tembele, nk.) na mboga-mboga (pilipili hoho, 
karoti, vitunguu, nyanya, bamia, biringanya, nyanya chungu, matango, 
nk.), bila kusahau mboga za asili na porini. Kundi la nne ni la matunda 
ya aina mbalimbali kama machungwa, maembe, mananasi, ndizi mbivu, limao,
 fenesi, parachichi, machenza, nk., ukijumuisha pia matunda ya asili na 
matunda ya porini. Kundi la tano la tano linajumuisha vyakula kama 
sukari, mafuta, karanga, ufuta, korosho, mbegu mbalimbali kama vile 
mbegu za alizeti, maboga na nazi" Alisema Bi.Ngilisho.
Nae afisa 
lishe mtafiti kutoka taasisi hiyo, Elizabeth Lyimo, alielezea kuhusu 
mchezo wa karata za mlo kamili ambao lengo lake ni kuboresha uelewa wa 
wananchi kuhusu mlo kamili kwa njia shirikishi na ya kufurahisha ili 
kuvutia washiriki kujifunza.
"Mtu yeyote anaweza kucheza mchezo 
wa karata za mlo kamili. Masuala ya chakula katika ngazi ya kaya 
yanatekelezwa kwa asilimia kubwa na wanawake, wanaume wamekuwa 
wakishiriki kwa kiwango kidogo hivyo basi mchezo huu unawalenga zaidi 
wanaume wa rika zote ili wapate uelewaa wa kupanga mlo iwe katika 
kununua vyakula au kuandaa mlo kwa ajili ya familia. " Alisema 
Elizabeth.
Aidha Mteknolojia Mwandamizi wa Maabara kutoka taasisi ya chakula na lishe Juvenary Mushumbusi alisema taasisi ina Maabara
mahususi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa
kimaabara ili kuiwezesha Taasisi kutekeleza na kufanikisha majukumu yake.
Maabara hii ina vitengo vitatu, ambayo ni;
• Mabara ya Kemia ya Chakula (Food Chemistry
 Laboratory)
 Kazi kuu ya maabara hii ni kufanya uchunguzi wa
 sampuli za chakula ili kubaini uwepo na wingi wa viinilishe
 kama
 vile, protini, wanga, mafuta, vitamini, madini na phytochemicals. Pia 
kitengo hiki hufanya uchunguzi wa kubaini ubora na usalama wa chakula 
Kama vile uwepo na wingi wa  sumukuvu, madini tembo, sumu kwenye
 mihogo (cyanide) na vikolezo (food additives)
• Maabara ya Baiokemia (Biochemistry
 Laboratory)
 Kazi
 kuu ya maabara hii ni kufanya uchunguzi wa  sampuli zinazochukuliwa 
kutoka kwenye mwili wa  binadamu ili kubaini viwango vya virutubishi au 
 viashiria lishe mwilini (Nutritional Biomarkers) mwilini; kwa mfano, 
vitamin, madini na elementi mbalimbali, mafuta na wingi wa damu
• Maabara ya Maikrobiolojia (Microbiology
 Laboratory)
 Kazi
 kubwa ya maabara hii ni kufanya vipimo maalumu vya kilishe Kama vile 
folate na amino asidi kwa kutumia mbinu za maikrobiolojia.
Pia 
maabara hii hupima vimelea vinavyo patikana kwenye chakula ili kubaini 
usalama na ubora wake kimikrobiolojia km vile uwepo wa vijidudu 
vinavyosabisha magonjwa kwa mtumiaji wa chakula au vile vinavyoashiria 
kuharibika kwa chakula au vinavyoashiria hali ya usa lama wa 
 maeneo/mazingira yanayuhusika na  utayarishaji/usindikaji wa chakula 
husika. Baadhi ya vimelea hivi ni kama Salmonella, E-coli,Shigella na 
S.aureus
Juvenali Msumbusi ni mtekinolojia mwandamizi wa maabara 
kutoka taasisi ya chakula na lishe taifa,amesema kulingana na maeneo ya 
nyanda za juu kusini mimea kukosa virutubishi,serikali imekuja na mpango
 wa kuongezea virutubishi kwenye chakula.
"Serikali saizi imekuja
 na mpango mwingine wa kuongezea virubishi kwenye vyakula kama unga wa 
mahindi na ngano na virutubishi hivi havibadilishi rangi wala radha na 
kwenye upande wa vitamini A tunaongeza virubishi kwenye mafuta ya 
kura"alisema Juvenali Msumbusi 
Aidha amewata wananchi kufika na 
kupata elimu katika taasisi hiyo licha ya wao kutumia njia mbali mbali 
ili kumalizana na tatizo la udumavu ikiwemo kwa watoto wadogo.
 



 
 
 
 
No comments:
Post a Comment