HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, August 21, 2020

WANAFUNZI MASONYA SEKONDARI WAPONGEZA MPANGO WA UCHUNGUZI WA KIFUA KIKUU

 


Na Mwandishi wetu Tunduru
WANAFUNZI wa shule za sekondari wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wameipongeza Hospitali ya wilaya kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma kutoa elimu na kufanya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa wanafunzi wa Bweni kwani hatua hiyo itasaidia wanafunzi kufahamu na kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugunjwa huo.
Wakiongea kwa nyakati tofauti wakati wakati wa uhamasishaji kampeni na uchunguzi kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Masonya, baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wamesema, mpango huo wa Hospitali ya wilaya utawezesha wanafunzi kufahamu madhara ya ugonjwa huo.
Wamesema, wanafunzi wengi hawakufahamu kwa undani ugonjwa wa kifua kikuu, hivyo kutokana na elimu iliyotolewa na wataalam kutoka kitengo cha kifua kikuu Hospitali ya wilaya ya Tunduru.
Aziza Ridhiwan amesema, kutokana na elimu waliyopata wataweza kujilinda na kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo unaotajwa kati ya magonjwa 10 yanayoongoza kupoteza maisha ya watu wengi hasa kutika nchi za Dunia ya tatu.
Ameiomba Serikali kupitia wizara ya afya kuhakikisha inaendelea kutoa elimu ya ugonjwa wa kifua kikuu katika shule zote za msingi na sekondari na jamii, kwani bado kuna wanafunzi wengi na hata watu wazima hawajafikiwa na elimu na huduma ya kifua kikuu hasa wanaoishi maeneo ya vijijini.
Maria Marwa wa kidato cha sita amesema,elimu waliyoipata ni mwanzo mzuri kwao kama wanafunzi wa bweni, na watatumia elimu hiyo kama mabalozi kwa wazazi na jamii inayowazunguka.
Alisema, kabla ya kupatiwa kwa elimu hiyo hapo mwanzo hawakujua chanzo na madhara ya ugonjwa wa kifua kikuu lakini kwa sasa wanafahamu hivyo itakuwa rahisi kwao kujikinga na ugonjwa wa kifua kikuu kwani moja ya makundi yaliyopo katika hatari ya kupata ugonjwa huo ni wanafunzi wanaokaa bweni.
Kwa upande wake mratibu wa kitengo cha cha kifua kikuu na ukoma katika Hospitali ya wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema, Hospitali ya wilaya inaendelea na mpango wa kupima ugonjwa wa kifua kikuu wanafunzi wote wa shule za sekondari wanaokaa bweni na wale wa kutwa.
Alisema, mpango huo unalenga kuwajengea uelewa wanafunzi juu ya ugonjwa wa kifua kikuu na kuwanusuru na maambukizi ya ugonjwa huo ambapo wale wanaobainika kuwa na ugonjwa huo wanaanzishiwa dawa.
Alisema, lengo ni kuhakikisha wanawafikia wanafunzi wote na umeanza kwa wanaoishi bweni na baadaye watakwenda katika shule mbalimbali za kutwa kabla ya kuanza kampeni hiyo kwa shule za msingi.
Kwa mujibu wa Kihongole,mpango wa uchunguzi wa kifua kikuu tangu ulipozinduliwa mwezi Machi mwaka huu umeleta mafaniko makubwa na wanafurahi kuona idadi ya wagonjwa wa kifua kikuu wanaofika katika vituo vya kutolea huduma wameongezeka ikilinganisha na siku za nyuma.
Alisema, hali hiyo inatokana na elimu inayotolewa na kampeni za uchunguzi zinazofanyika mara kwa mara na kitengo cha kifua kikuu na ukoma ambapo ametoa wito kwa jamii kuhakikisha pale wanapoisi dalili za kifua kikuu ni vizuri kuwahi hospitali kwa ajili ya uchunguzi badala ya kusubiri hadi pale tatizo linapokuwa kubwa.
Alisema, ugonjwa wa kifua kikuu unazuilika kwa mgonjwa kupata chanjo sahihi,kula chakula bora,kuishi kwenye makazi bora na matibabu yake yanatolewa bure katika vituo vyote vya serikali na vinavyomilikiwa na taasisi za dini hapa nchini.
Mratibu wa ugonjwa wa kifua kikuu na Ukoma wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Mkasange Kihongole kulia,akimsikiliza mwanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya sekondari Masonya wilayani humo Maria Marwa aliyetaka kufahamu zaidi chanzo cha ugonjwa wa kifua kikuu na athari zake wakati wa zoezi la uhamasishaji na uchunguzi wa ugonjwa huo kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Masonya wilayani Tunduru wakiwa katika mstari kwa ajili ya kujaza fomu maalum kabla ya kuanza kwa zooezi la uchunguzi na upimaji wa ugonjwa wa kifua kikuu lililofanywa na kitengo cha kifua kikuu na ukoma Hospitali ya wilaya Tunduru kwa wanafunzi wa shule hiyo. Picha zote na Mpiga Picha Wetu,

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad