HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, 5 October 2019

ZANTEL KUSHIRIKIANA NA BENKI YA POSTA KUTOA HUDUMA ZA KIFEDHA KUPITIA SIMU ZA MKONONI

 Mkuu wa Masoko na Huduma ya Fedha wa Zantel, Sakyi Opoku, (wa pili kutoka kushoto) akipeana mkono na Mkuu wa TEHAMA na Uendeshaji wa Benki ya TPB, Jema Msuya,mjini Zanzibar, kuashiria uzinduzi wa ushirikiano utakaowezesha watumiaji wa huduma ya EzyPesa ya Zantel kupata huduma za kibenki za benki hiyo. Wengine pichani ni Wengine pichani ni Mkuu wa Zantel Zanzibar, Mohamed Khamis Mussa (kushoto) na Mkurugenzi wa Masoko na Uendelezaji wa Biashara wa TPB, Deo Kwiyukwa ( Kulia).
Meneja wa Huduma za EzyPesa wa Zantel, Leonard Kameta, akifanya mhamala wa malipo kutoka akaunti ya EzyPesa kwenda kwenye akaunti ya benki ya TPB, wakati wa uzinduzi wa ushirikiano wa Zantel kupitia huduma ya Ezypesa na TPB ambao unawezesha wateja wa Zantel kufanya mihamala ya kibenki katika Benki ya TPB, Anayeangalia ni Mkuu wa Zantel Zanzibar Mohammed Khamis Mussa (kushoto), Mkuu wa Masoko na Huduma ya Fedha wa Zantel, Sakyi Opoku,(wa pili kutoka kushoto),wengine ni Mtaalamu wa TEHAMA wa TPB,Melleji Mollel (Kulia), Mkuu wa TEHAMA na Uendeshaji wa Benki ya TPB, Jema Msuya na Mkurugenzi wa Masoko na Uendelezaji wa Biashara wa TPB, Deo Kwiyukwa ( wa kwanza kutoka kulia).

Na Mwandishi Wetu.

Wakati matumizi ya huduma za kifedha kupitia simu za mkononi yanaongezeka kwa kasi kubwa, huduma ya fedha ya mtandao wa Zantel ya EzyPesa, imeunganishwa na Benki ya TPB, kuwawezesha wateja kufanya mihamala ya fedha ya kibenki kupitia simu zao za mkononi.

Ushirikiano huu umeiwezesha kampuni ya Zantel kufikisha idadi ya taasisi za fedha inazoshirikiana nazo kufikia 12, lengo kubwa likiwa ni kurahisisha maisha kupitia huduma ya EzyPesa.

“Sekta yetu imekuwa na mabadiliko kwa kasi kubwa kiteknolojia, ambayo yanatufanya kwenda nayo sambamba ili kuhakikisha wateja wetu wanaotumia huduma yetu ya fedha kuendelea kupata huduma bora kupitia kuingia ushirikiano wa kutoa huduma na taasisi nyinginezo,” alisema Mkuu wa Zantel Zanzibar, Mohammed Khamis Mussa.

Aliongeza kuwa ushirikiano huu uliozinduliwa, wateja wa Zantel wanaweza kupata huduma za kibenki za TPB kupitia Ezypesa, wataweza kufanya mihamala kwa kuingia katika menu ya Ezypesa kwenye simu zao za mkononi”.

“Huduma za kifedha kupitia simu ya mkononi zinazidi kurahisishwa kwa wateja wetu kwa kuingia ushirikiano na TPB na tunayo furaha kuingia katika ushirikiano huu ambao tuna imani utazidi kuwarahisishia wateja kupata huduma za kibenki kwa urahisi zaidi na mkakati wetu ni kuendelea kushirikiana na taasisi nyinginezo zaidi ili kukidhi matakwa ya wateja wetu wote” alisema Mussa.

Kwa upande wake Mkuu wa Masoko na Huduma za Kifedha wa Zantel, Sakyi Opoku,alisema huduma ya EzyPesa na TPB POPOTE inatoa fursa kwa Zantel, kupanua huduma zake na kuboresha maisha ya watu. “Dhamira yetu ni kuendelea kuwezesha wananchi kuingia katika mfumo rasmi wa huduma za kifedha nchini kwa kuwawezesha kupata huduma za kibenki kupitia simu zao za mkononi hususani wateja wetu ambao walikuwa hawawezi kuzipata kwa urahisi”.

Mkurugenzi wa Masoko na Uendelezaji Biashara wa TPB,Deo Kwiyukwa, alisema Benki ya TPB, inazo huduma mbalimbali zinazokidhi mahitaji ya watanzania wote, hivyo anaamini Zantel ni mshirika wake mzuri kibiashara kwa kuwa taasisi zote hizi mbili zina lengo la kutoa huduma bora kwa wateja . “Tunayo furaha kuingia katika ushirikiano huu na Zantel, kwa kuwa tunazidi kufanikisha dhamira yetu ya kupanua huduma za kifedha ili ziwafikie wananchi wengi sambamba na kutoa fursa kwa watumiaji wa mtandao wa Zantel kupata huduma mbalimbali za benki yetu”, alisema.

Kwiyukwa,aliongeza kusema kuwa mtumiaji wa Huduma ya kifedha ya EzyPesa na TPB POPOTE ataweza kupata huduma mbalimbali za Benki ya posta kama vile kuulizia salio katika akaunti yake,taarifa ya mihamala katika akaunti yake kwa urahisi akiwa mahali popote,saa yoyoye na katika siku zote za wiki.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad