HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 14, 2019

WAZIRI MKUU AWASIMAMISHA KAZI WAKURUGENZI SABA TUME YA UMWAGILIAJI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi Wakurugenzi saba wa Tume ya Umwagiliaji akiwemo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazowakabili.

“CAG afanye haraka uchunguzi wa kina, tunataka kujua ni nani alikuwa mlango wa ubadhirifu huu. Hatutamuonea mtu, wote watakaothibitika kuhusika na matumizi mabaya ya fedha watachukuliwa hatua.”

Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo leo (Jumanne, Mei 14, 2019) wakati wa kikao na viongozi wa tume hiyo kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Mawaziri, Manaibu Waziri na Makatibu Wakuu. 

Mbali na kuwasimamisha kazi wakurugenzi hao, pia Waziri Mkuu ameagiza watumishi wengine 21 wa tume hiyo wachukuliwe hatua za kinidhamu kutokana na utendaji usioridhisha kwenye miradi mbalimbali inayosimamiwa na tume hiyo.

Waziri Mkuu amesema Serikali imechukua hatua hiyo kutokana na udhaifu wa kiutendaji ndani ya tume hiyo ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za miradi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, upendeleo na kukosa umakini. “Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya ubadhirifu uliofanyika katika miradi ya umwagiliaji.”

Amesema hali ya kilimo cha umwagiliaji nchini hairidhishi na Serikali haijafurahishwa na utendaji wa Tume ya Umwagiliaji licha ya kuwekeza nguvu kubwa, hivyo inataka kuona mabadiliko.

“Miradi mingi inayotekelezwa na Tume ya Umwagiliaji nayo ina hali mbaya zaidi. Miradi mingi ya tume hiyo imejikita katika mafunzo, semina na warsha badala ya kujenga na kuendeleza skimu za umwagiliaji.”

Waziri Mkuu amesema tume hiyo imeshindwa kusimamia miradi takribani 10 katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha sekta ya umwagiliaji kushindwa kupata mafanikio yaliyotarajiwa kutokana na ubadhirifu.

Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na mradi wa umwagiliaji wa Luiche unaokadiriwa kumwagilia hekta 3,000 ambao upo katika hatua za awali za utekelezaji lakini tayari pamekuwepo na matumizi mabaya ya fedha za mradi.

“Kaimu Mkurugenzi Mkuu alitoa kibali na kulipa fedha taslimu masurufu ya jumla ya sh. milioni 100.7 kwa Wahandisi wa Makao Makuu, Maafisa wa Idara ya Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji kwenda kufanya ukaguzi badala ya kujenga. Mkaguzi wa nje alihoji uhalali wa malipo hayo na hajapata majibu hadi leo.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akamilishe mchakato wa kuwapata wajumbe wa bodi wa tume hiyo ambayo imemaliza muda wake.

Pia amemtaka Waziri huyo ahakikishe Wizara ya Kilimo inaisimamia tume kukamilisha ujenzi wa skimu zote za umwagiliaji zilizoanza kujengwa miaka ya nyuma zikiwemo za wakulima wadogo.

Kadhalika, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Kilimo afanye mabadiliko ya muundo wa tume hiyo na kuwa na maafisa wa umwagiliaji katika ngazi za mikoa na wilaya ili kusogeza huduma kwa wananchi.

Awali, Waziri wa Kilimo alisema skimu zinazofanya kazi hazizidi 10 kati ya 2,678 hali iliyosababishwa na kuwepo kwa dosari katika usimamizi na pia matumizi ya fedha za miradi katika Tume ya Umwagiliaji si mazuri.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa alisema miradi mingi ya umwagiliaji ilifeli kwa sababu ya ilijengwa chini ya kiwango hususani mabwawa na pia haikuwa ikilingana na kiasi cha fedha kilichokuwa kinatolewa. “Mradi wa kutumia sh. bilioni mbili wanatumia sh. bilioni nne.”

Kikao hicho kimehudhuriwa na Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, Naibu Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Mwita Waitara, Naibu Waziri wa Kilimo, Omar Mgumba, Naibu Waziri wa Kilimo Innocent Bashungwa, Makatibu Wakuu wa Wizara hizo pamoja na maofisa wengine wa Serikali.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Watendaji wa Tume ya Umwagiliaji kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Mei 14, 2019. Kushoto ni Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga na wa tatu kulia ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa. Wa pili Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Umwagiliaji, Eliakim Chitutu. (PIcha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Baadhi ya Watendaji wa Tume ya Umwagiliaji wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Mei 14, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga mara baada ya kumaliza kuongea na  watendaji wa Tume ya Umwagiliaji kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Mei 14, 2019.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad