Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema
Wananchi wanapaswa kujua Historia yao katika dhana nzima ya kuendelea
kulinda Uhuru wao, Heshima, Utamaduni na hata mazingira yao
yanayowazunguuka ya kila siku.
Alisema Binaadamu asiyejua Historia yake kamwe anakuwa Mtumwa wakati
wote akiendelea kutawaliwa kifikra jambo ambalo ni hatari katika
maisha yake yanayomuhusu.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo alipofanya ziara fupi ya kuyakagua
Mahandaki Mawili ya Mangapwani yaliyokuwa yakitumika kuhifadhia
Watumwa ambayo kwa sasa yamekuwa sehemu muhimu ya kujifunza Historia
ya Biashara hiyo iliyopigwa marufuku tokea Karne ya 18.
Alisema Zanzibar ilikuwa kituo muhimu cha Historia iliyounganisha
sehemu nyingi Duniani historia ambayo Taasisi inayosimamia masuala
hayo ambayo ni Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale ina jukumu la
kusimamia vyema maeneo yote muhimu ili Wageni pamoja na Wananchi
wapate fursa ya kujifunza zaidi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pia aliwakumbusha Vijana
wanaosimamia maeneo hayo kufanya jitihada ya kujifunza Historia kamili
ili kuepuka tabia ya kutoa Taarifa zisizo na uhakika wa Historia ya
maeneo wanayofanyia kazi.
Akitoa ufafanuzi Msimamizi wa Mahandaki ya Mangapwani Makame Omar Said
alisema maumbile ya eneo hilo muda wote yamekuwa ya kujificha kutokana
na hali halisi ya biashara yenyewe ya Utumwa ilivyokuwa ikifanywa kwa
kujificha.
Makame alisema utafiti unaonyesha wazi kwamba bado idadi ya Wazawa
kufika eneo hilo kwa ajili ya kujifunza Historia yake ni ndogo
ikilinganishwa na Wageni pamoja na Wasomi wa fani za Kihistoria.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale
anayesimamia Utalii na Mambo ya Kale Dr. Amina Ameir Issa alimueleza
Balozi Seif kwamba Idara ya Mambo ya Kale ilianzishwa Mnamo
Mwaka1920.
Dr. Amina alisema hatua hiyo ilifuatiwa na kutungwa kwa Sheria ya
Mambo ya Kale Mnamo Mwaka 1941 ikiwa chini ya uangalizi wa Idara ya
Mambo ya Kale ikiwa na lengo la kusimamia maeneo Saba ya Kihistoria
hapa Zanzibar.
Aliyataja baadhi ya Maeneo hayo kuwa ni pamoja na Mahandaki ya
Mangapwani,Msikiti Mkongwe wa Kizimkazi, Mji wa Makutani uliopo katika
Kisiwa cha Tumbatu pamoja na Mji wa Mwinyimkuu uliopo Dunga.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale
anayesimamia Utalii na Mambo ya Kale alifahamisha kwamba Mahandaki ya
Mangapwani yana bahati kubwa ya kutembelewa na Wageni wengi, Watalii,
Wanafunzo pamoja na Watafiti ikilinganishwa na sehemu nyengine za
Kihistoria zilizopo Zanzibar.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale
Bibi Khadija Bakari Juma alisema Wizara hiyo kwa sasa tayari
imeshaandaa mpango maalum wa kushajiisha Utalii wa ndani ili
kuimarisha zaidi mapato ya Taifa.
Bibi Khadija alisema mpango huo umeaanza kufanya kazi kwa kuwahusisha
watendaji wa Wizara hiyo kama muelekeo wa ushajiishaji ili kuungwa
mkono ya Wizara nyengine na baadae Wananchi hapa Nchini.
Katibu Mkuu Habari ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
uamuzi wake wa kutenga Bajeti Maalum kila Mwaka inayolenga kuhudumia
Uhifadhi wa Maeneo ya Kihistoria hapa Nchini jambo ambalo limeleta
matokeo mazuri katika usimamizi wa maeneo hayo muhimu.
Akielezea changamoto zinayoyakabili maeneo mengi ya Kihistoria Nchini
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Rajab Ali Rajab alimueleza Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba uhaba wa wafanyakazi ni tatizo
kubwa linalofaa kuangaliwa na Serikali pamoja na Taasisi inayosimamia
maeneo hayo.
Nd. Rajab alisema ufinyu huo wakati mwengine hutoa mwanya kwa wahalifu
kufanya hujuma katika maeneo hayo ambayo kwa namna yoyote ile
yanapaswa kuheshimiwa na kuenziwa kwa vizazi vya sasa na vile vijavyo.
“ Yapo matendo mabaya wakati mwengine hufanyika ya uharibifu a maeneo
ya Hifadhi kama uchafuzi wa mazingira kutokana na kukosa usimamizi
imara wa Watendaji”. Alisisitiza Mkuu huyo wa Wilaya ya Kaskazini “B”.
Zanzibar iliyokuwa Kituo cha Biashara ya Utumwa katika Mwambao wa
Afrika Mashariki ilisimamisha Biashara hiyo chini ya Utawala wa
Uingereza Mnamo Mwaka 1873 licha ya baadhi ya Wafanyabiashara
kuendelea kufanya biashara hiyo kwa siri.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifanya ziara ya
kukagua Mahandaki Mawili ya Mangapwani yaliyokuwa yakitumika kuhifadhia
Watumwa ambayo kwa sasa yamekuwa sehemu muhimu ya kujifunza Historia ya
Biashara hiyo iliyopigwa marufuku tokea Karne ya 18.
Balozi
Seif Ali Iddi akipewa maelezo ya Biashara ya Utumwa ilivyokuwa
ikufanyika katika Mahandaki ya Mangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale anayesimamia
Utalii na Mambo ya Kale Dr. Amina Ameir Issa akielezea jitihada
zinazochukuliwa na Wizara kuyasimaia vyema Mahandaki ya Mangapwani.
Balozi Seif akiuagiza uongozi wa Wizara ya Habari,
Utalii na Mambo ya Kale pamoja na ule wa Wilaya kuendelea kuyahifadhi
Mahandaki ya Mangapwani ili yaendelee kutoa huduma za Kihistoria.
Picha na – OMPR – ZNZ.
No comments:
Post a Comment