HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 14, 2019

MKUU WA WILAYA KOROGWE AHIMIZA WANANCHI KULIPA KODI KWA WAKATI

Na Veronica Kazimoto
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Kissa Kasongwa amewahimiza wananchi kulipa kodi kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za jamii kwa lengo la kuleta maendeleo nchini.   

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi inayofanyika wilayani humo, Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuna miradi ya huduma za jamii inayojengwa katika Wilaya ya Korogwe ikiwemo Hospitali ya Wilaya, miradi ya barabara, maji, umeme na elimu ambayo yote inategemea kodi ili iweze kukamilika.

“Bado Korogwe kiwango chetu cha kulipa kodi ni kidogo kwani kati ya wananchi 303,000 wa wilaya hii, ni wananchi 2,800 ndiyo wanalipa kodi na tumeshaelekeza kwamba wale wasiokuwemo kwenye mfumo wa TRA ambao mauzo ghafi yao ni chini ya sh. 4,000,000 wanatakiwa kuwa na vitambulisho vya wajasiriamali.

“Sote tunatakiwa tutambue kwamba, tusipolipa kodi, tunajidhoofisha wenyewe kimaendeleo. Hivyo, tujitahidi kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati ili tuweze kutekeleza miradi inayoendelea hapa wilayani kwetu,” alisema Kasongwa.

Naye Mkurugenzi wa Sheria wa Sekretariati ya Bodi na Huduma za Kisheria wa TRA Makao Makuu Salim Beleko, amesema kuwa kodi ni sawa na damu kwenye mwili wa binadamu, hivyo kama Serikali itashindwa kupata kodi itashindwa kufanya jambo lolote la maendeleo kwa wananchi wake.

Aidha, Beleko ameongeza kuwa wananchi hawatakiwi kulalamika kwasababu wanayo fursa ya kukata rufaa endapo hawataridhika na makadirio ya kodi waliyokadiriwa na malalamiko yao tatafanyiwa kazi Mamlaka ya Mapato Tanzania huku akisisitiza kuwa Tanzania ni moja ya nchi chache ambazo wananchi wake wanalipa kodi kwa hiari tofauti na nyingine ambapo wanalipa kwa nguvu.

Kwa upande wa Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga Lucas Kaigarula amesema lengo la wiki hiyo ya huduma na elimu kwa mlipakodi ni kutoa elimu ya kodi, kusikiliza malalamiko, changamoto pamoja na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa walipakodi.

Wiki ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi inafanyika nchi nzima ambapo kwa Mkoa wa Tanga inafanyika wilayani Korogwe. Wiki hii ya elimu kwa mlipakodi imeanza tarehe 13 na itamalizika tarehe 17 Mei, 2019 ikiongozwa na kaulimbiu isemayo “Karibu tukuhudumie na tukuelimishe”.
 Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Kissa Kasongwa akizungumza kwenye ufunguzi wa Wiki ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi katika Mkoa wa Tanga inayofanyika katika Stendi ya zamani ya mabasi, Manundu. Wengine ni Mkurugenzi wa Sheria wa Sekretariati ya Bodi na Huduma za Kisheria wa TRA Makao Makuu Salim Beleko (kulia) na Kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Korogwe Rehema Bwasi
 Mkurugenzi wa Sheria wa Sekretariati ya Bodi na Huduma za Kisheria wa TRA Makao Makuu Salim Beleko akizungumza kwenye ufunguzi wa Wiki ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi inayofanyika katika Stendi ya zamani ya mabasi, Manundu mkoani Tanga. Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Kissa Kasongwa (kushoto) na Kulia ni Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga Lucas Kaigarula.
 Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Kissa Kasongwa (wa kwanza kushoto) akimsikiliza Ofisa wa Elimu kwa Mlipakodi Mkoa wa Tanga Salim Bakari (kulia) kwenye ufunguzi wa Wiki ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi inayofanyika katika Stendi ya zamani ya mabasi, Manundu mkoani Tanga. (Picha na mpigapicha wetu).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad