HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 18, 2019

Mawaziri wakutana na Watanzania waishio Namibia

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.), akiambatana na Waziri Ofisi ya Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Issa Haji Ussi Gavu; Waziri wa Viwanda na Biashara, George Kakunda (Mb.) na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) tarehe 17 Machi, 2019, wamepata fursa ya kukutana na jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Namibia na kujadiliana nao masuala mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa vitambulisho vya taifa na hati za kusafiria, maendeleo na hali ya siasa nchini, biashara kwa ujumla na mkakati wa serikali katika kunufaika uanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Miongoni mwa masuala mengine, mawaziri hao wamewataarifu Watanzania hao kuhusu juhudi mbalimbali zinazotekelezwa na serikali ya awamu ya tano katika kuleta maendeleo ambazo ni pamoja na kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa uvujaji wa mapato; ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa mazao na bidhaa; ukuaji katika sekta ya viwanda; ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika Korongo la Stiglers;kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za kijamii zikiwemo afya na elimu bure na mkakati wa Tanzania kujitanua kibiashara katika eneo la SADC.

Prof. Kabudi amewataka Watanzania hao kuacha kuamini dhana kuwa, chema chajiuza na kibaya chajitembeza na kuanza kuyasemea masuala mbalimbali mazuri ya Tanzania. Ametolea mfano uwepo wa uhitaji mkubwa wa vitu vyenye ubora vinavyozalishwa nchini kama vigae, nepi za watoto, korosho na mvinyo na kuwataka Watanzania hao kuitumia fursa hiyo kuwa mawakala wa bidhaa hizo nje ya nchi.Suala hilo limeungwa mkono na Watanzania hao ambao wameiomba Wizara ya Viwanda na Biashara kuwapa taarifa sahihi za kibiashara na kwa wakati. 

Kuhusu suala la kila Mtanzania kuwa na hati mpya ya kielektronikia ya kusafiria ifikapo mwaka 2020, Prof. Kabudi amewataarifu Watanzania hao kuwa, serikali inaziboresha hati za sasa za kusafiria kwa mujibu wa makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Hivyo, ameitaka jumuiya ya Watanzania wanaoishi nje ya Tanzania kuhakikisha wanakuwa na vitambulisho vya kitaifa ambavyo ni moja ya vielelezo muhimu katika kuomba hati hizo mpya za kusafiria.

Prof. Kabudi amewahakikishia Watanzania hao kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kitengo cha Diaspora, kipo wazi muda wote ili kuwasaidia Watanzania wanaoishi nje ya nchi ili kuhakikisha wanapata vitambulisho hivyo vya taifa kwa wakati.

Mawaziri hao wapo nchini Namibia kwa lengo la kuhudhuria mkutano wa Baraza la Mawaziri la SADC ambao umefanyika kuanzia tarehe 15 hadi 17 Machi, 2019. 

Wajumbe walioshiriki katika mkutano huo wakifungua mkutano kwa kuimba wimbo wa taifa.
Kaimu Balozi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ambao pia unawakilisha nchini Namibia, Richard Lupembe, akimkaribisha Prof. Kabudi kwa ajili ya kufungua mkutano huo.
Sehemu ya Watanzania waishio nchini Namibia wakifuatilia mkutano huo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, akifurahia jambo wakati wa mkutano huo.Pembeni yake ni baadhi ya Watanzania waishio Namibia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad