HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 6 February 2019

Wakimbizi kupewa Vitambulisho

Serikali imelitaka Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani(UNHCR) kusaidia katika utoaji wa vitambulisho kwa  wakimbizi wote walioko katika makambi  pamoja na kusaidia uanzishwaji wa kanzidata ya wakimbizi nchini itakayomilikiwa  na serikali.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhnadisi Hamad Masauni wakati akizungumza katika kikao cha ndani na Ujumbe ulioongozwa na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani(UNHCR) Fillippo Grandi,ambaye yuko nchini kwa ziara ya kikazi.

Naibu Waziri Masauni alisema Serikali ya Tanzania imekua na historia ndefu katika jukumu la kuhifadhi wakimbizi wanaokimbia machafuko katika nchi zao lakini wakimbizi hao wanatakiwa kutokua sehemu ya watu wanaovunja sheria pindi wawepo makambini.

“Ni muhimu sasa UNHCR wakasaidiana na serikali katika kuboresha  orodha ya wakimbizi walioko nchini sambamba na ugawaji wa vitambulisho kwa wakimbizi watakaothibitika kisheria kuwa ni wakimbizi huku ikisaidia katika kupokea wakimbizi halali na sio wahamiaji haramu” Alisema Masauni

Akizungumza katika kikao hicho Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani(UNHCR) Fillippo Grandi aliishukuru serikali ya Tanzania kwa kupokea wakimbizi kwa muda mrefu na akiweka wazi  lengo lao la kushirikiana  na nchi zinazopokea wakimbizi    katika kusimamia zoezi la urejeshwaji wa wakimbizi wanaotaka kurudi kwao kwa hiyari

“Tutahakikisha tunasimamia wakimbizi kutii sheria za nchi husika  ikiwemo uhifadhi wa mazingira katika makambi na kusaidia urejeshwaji wa wakimbizi walio tayari kurejea katika nchi zao baada ya kurejea kwa amani” alisema Filippo

Tanzania inahifadhi zaidi ya wakimbizi Laki Tatu katika kambi za Nyarugusu, Nduta na Mtendeli zilizopo mkoani Kigoma.  
 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni (katikati), akiongozana na   Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Fillippo Grandi baada ya kumaliza kikao cha ndani ambacho mambo mbalimbali kuhusiana na wakimbizi yalijadiliwa. Kulia  ni Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu.Kikao hicho kimefanyika leo katika Ofisi Ndogo ya wizara jijini Dar es Salaam.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni, akiagana na    Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Fillippo Grandi (kushoto) baada ya kumaliza kikao cha ndani ambacho mambo mbalimbali kuhusiana na wakimbizi yalijadiliwa. Katikati   ni Katibu wa Naibu Waziri, George Mwansasu.Kikao hicho kimefanyika leo katika Ofisi Ndogo ya wizara jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad