HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, February 28, 2019

DKT. KIJAJI ASHITUKIA GHARAMA ZA MRADI WA UKARABATI WA SHULE YA SEKONDARI MZUMBE MKOANI MOROGORO

Na Peter Haule, WFM, Morogoro
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amuagiza uongozi wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro kuuchunguza mkataba wa ukarabati wa shule kongwe ya Sekondari ya Wavulana-Mzumbe, ulioingiwa kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Shirika la Nyumba la Taifa-NHC ili kujiridhisha kuhusu gharama halisi za mradi baada ya kubaini kiasi kinachodaiwa kutumika kukarabati shule hiyo kinatofautiana na fedha halisi zilizotolewa na Serikali

Dkt. Kijaji, ametoa maagizo hayo alipotembelea na kufanya ukaguzi wa ukarabati wa shule kongwe ya Sekondari ya wavulana ya Mzumbe iliyopo Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro na kuelezwa na viongozi wa wilaya hiyo akiwemoo Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kutokuwa na taarifa zozote kuhusu mradi huo.

Dkt. Kijaji alishangazwa na utofauti wa kiwango cha fedha kilichoainishwa katika taarifa ya gharama ya ukarabati wa shule hiyo kwamba ilikuwa shilingi milioni 999.7 wakati kiasi cha fedha kilichotolewa na Serikali ni zaidi ya shilingi bilioni 1.

Alitoa wito kwa wakuu wa wilaya kote nchini kufuatilia kwa karibu miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ili kujiridhisha kuhusu fedha zinazotumika kwenye miradi hiyo, kukagua thamani ya fedha kwenye miadi husika, pamoja na mikataba yote inayohusika ili kujua mawanda (scope) ya miradi hiyo

"Kila anayekuja kutekeleza miradi katika Wilaya ni vema akaulizwa amekuja kufanya nini na kwa namna gani kwa kuwa lengo ni kuwasaidia wananchi wa maeneo husika na Taifa kwa ujumla na hakuna siri kwenye miradi hiyo kwa hiyo ni lazima muijue kwa undani" alisema Dkt. Kijaji

Alisema kuwa,  Shule Kongwe ya Mzumbe imekarabatiwa na mabadiliko yanaonekana lakini ni vigumu kujua ilitakiwa kukarabatiwa kwa kiwango kipi na maeneo gani kwa kuwa wahusika wakiwemo Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na Mkuu wa Shule hiyo hawafahamu mawanda ya mradi huo.

"Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mvomero hakikisheni mnapata mkataba wa ukarabati wa shule hii ili kupata uhakika wa nini kilitakiwa kifanyike kwa kuwa bado maeneo mengi hayajakarabatiwa na Mkandarasi ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa lakini tayari amekabidhi kazi" alisisitiza Dkt Kijaji.

“Dhamana ya Wizara ya Fedha na Mipango ni kutafuta fedha, kupeleka maeneo husika kwa ajili kubadili maisha ya watanzania na kukagua matumizi yake, hivyo hali hiyo iliyojitokeza inaenda kufanyiwa kazi kwa lengo la kuongeza ushirikiano”, alieleza Dkt. Kijaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bw. Florent Kyombo, aliishauri Serikali kuona namna bora ya kuboresha ushirikiano wakati wa utekelezaji wa miradi kama hiyo kuanzia kwenye upembuzi yakinifu wa majengo yanayokarabatiwa, nini kikarabatiwe, wakati gani, na kuwahusisha wataalam wa wilaya wakati wa kukagua na kutathimini kazi iliyofanyika kabla ya mkandarasi kulipwa

Naye Mkuu wa Shule hiyo Kongwe ya Mzumbe Bw.Wal Kihongosi, aliishukuru Serikali kwa hatua yake ya kuboresha shule hiyo ya vipaji maalum kwa kuwa hapo awali mazingira yake yalikua hayasadifu hadhi ya kuwa na wanafunzi wenye vipaji.

Pia akaiomba Serikali kusaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi, kuongeza vifaa vya maabara kwa kuwa havitoshi, kujengewa jengo moja jipya kwa ajili ya ofisi ya taaluma pamoja na idara zake tisa  na pia kuongeza idadi ya watumishi wakiwemo wapishi na walinzi walioajiriwa wa muda mrefu badala ya waliopo ambao ni wa mkataba wa mda mfupi ambao udhibiti wake kulingana na unyeti wa kazi hizo ni mgumu.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro Bw. Mohamed Utaly, alipotembelea na kukagua ukarabati wa Shule Kongwe ya Sekondari ya Wavulana ya Mzumbe.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akihoji baadhi ya maeneo ya ukarabati wa Shule Kongwe ya Sekondari ya Wavulana Mzumbe, alipotembelea na kukagua ukarabati wa Shule hiyo Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro.
 Mkurugenzi wa Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro Bw. Florent Kyombo, akiiomba Serikali kushirikisha uongozi wa Wilaya katika hatua za awali za utekelezaji wa miradi, wakati Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (hayupo pichani) alipotembelea na kukagua ukarabati wa Shule Kongwe ya Sekondari ya Mzumbe.
 Mkuu wa Shule Kongwe ya Wavulana ya  Mzumbe Bw. Wal Kihongosi, akitoa maelezo ya maeneo yaliyokarabatiwa huku wadau wengine wakitazama picha za majengo hayo, wakati Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (hayupo pichani) alipotembelea na kukagua ukarabati wa Shule hiyo.
 Mkuu wa Shule Kongwe ya Wavulana ya  Mzumbe Bw. Wal Kihongosi, akisoma kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya ukarabati wa Shule yake ambacho kilikua kinatofautiana na kiasi alichowasilisha cha kutekeleza maboresho hayo. Kushoto ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb).
 Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro Bw. Mohamed Utaly, akiuliza jambo wakati Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kulia), alipotembelea majiko ya Gesi yaliyo karabatiwa katika Shule Kongwe ya Wavulana Mzumbe, Mkoani Morogoro .
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wa pili kulia), akiongozwa na Mkuu wa Shule Kongwe ya Wavulana Mzumbe, Bw. Wal Kihongosi (kulia) kukagua ukarabati wa shule yake.
Muonekano wamajengo ya Shule Kongwe ya Wavulana ya  Mzumbe, yaliyokarabatiwa na kubadilisha mandhari ya shule hiyo yenye wanafunzi wenye vipaji.

(Picha na Peter Haule, Wizara ya Fedha na Mipango)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad