HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 7, 2019

MAPINDUZI YA KIJESHI YAHOFIWA KUTEKELEZWA NCHINI GABON

Na Leandra Gabriel, Blogu ya Jamii

JESHI la wananchi nchini Gabon limeshikilia kituo cha redio cha taifa nchini humo na kutangaza kutoridhishwa na hali ya kiafya na Rais wa nchi hiyo Ali Bongo Ondimba anayetibiwa nchini Morocco akisumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi huku amri ya kutotoka nje ikitolewa. Luteni kanali Ondo Obiang kiongozi wa kundi la harakati za ulinzi na usalama wa vikosi vya Gabon amesema kuwa ujumbe wa mwaka mpya uliotolewa na Rais Bongo umezidi kuwapa nguvu ya kutoamini uwezo wake katika kuendelea na utekelezaji wa majukumu yake ya kiuongozi.

Katika hotuba yake ya kutoa salamu za mwaka mpya Rais Bongo alisema kuwa hali yake si ya kuridhisha ila anaendelea kupata matibabu na kupata afueni. Shirika la AFP limesema kuwa milio ya risasi imesikika katika mji mkuu wa nchi hiyo Libreville na karibu na kituo hicho cha redio ya taifa tangu majira ya saa 10 alfajiri  huku ikisemekana mapinduzi hayo yanatekelezwa na kikundi kidogo cha askari.

Bongo (59) alilazwa nchini Saud Arabia Oktoba 28 mwaka jana akipatiwa matibabu mara baada ya kupata kiharusi na baadaye Novemba  kwenda nchini Moroco ambako bado anaendelea na matibabu zaidi. Ali Bongo Ondimba alizaliwa Februari 9, 1959 ambapo alimrithi baba yake Omar Bongo aliyetawala tangu mwaka 1967 hadi kifo chake mwaka 2009 na katika utawala wa baba yake Ali Bongo aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Waziri wa mambo ya nje kwa miaka kadhaa.

Inasemekana kuwa utawala wa muda mrefu wa familia hiyo ndio unapelekea mapinduzi haya na taarifa kuhusiana na hali hiyo itatolewa na msemaji wa Rais muda mfupi ujao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad