HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, December 21, 2018

MKOA WA ARUSHA WAPATA ENEO LA UJENZI WA KITUO KIKUU CHA MABASI

Na Ahmed Mahmoud, Arusha
Mkoa wa Arusha unakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na kituo cha mabasi chenye hadhi ya kisasa,kwani kilichopo sasa kinakabiliwa na ufinyu hali iliyoilazimu  Halmashauri ya Jiji la Arusha kuja na mkakati wa kujenga kituo kikubwa cha mabasi chenye hadhi ya Kimataifa,kinachotarajiwa kujengwa katika Kata ya Olasiti iliyopo nje kidogo ya jiji hilo .

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo alipotembelea Eneo litakapojengwa Kituo hicho ambapo amewataka viongozi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa kila mwananchi aliepisha eneo lake kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho analipwa fidia inayokadiriwa ni ni zaidi ya shilingi bilioni 1.7.

Gambo amesema kuwa mkoa wa arusha hauna standi inayoendana na hadhi ya jiji hilo na kuweza kufanya tathmini upya ya eneo hilo ili kuanza mchakato wa kuwalipa wale wanaostahili ili kuondoa sintofahamu ya kuwalipa watu wasio husika hali ambayoimekuwa ikisababisha malalamiko na migogoro mingi isiyo na tija kati ya wananchi na serikali yao.

“Hakikisheni mnapitia upya mchakato wa kuwalipa wananchi na ikiwezekana kila moja asimame kwenye eneo lake ili kuhakikisha mnamlipa mtu anayestahili kulipwa na sivinginevyo ili kuepusha migogoro isiyo na tija kati ya serikali na wananchi”alisisitiza mkuu huyo wa mkoa.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt.Maulid Madeni amesema kuwa pindi kituo hicho cha mabasi kinachojengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa hekari 29.5 kitakapokamilika Halmashauri hiyo itaongeza wigo katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na wananchi wa jiji la Arusha kunufaika na uwepo wa kituo hicho.

Amesema kuwa mchakato wa awali wa jiji ulikuwa kujenga vituo viwili vya kisasa katika maeneo  ya Kata ya Moshono na Olasiti ila kutokana na mgogoro wa kimipaka kati ya Halmashauri jirani ya Arusha na jiji ndio maana wataanza na ujenzi katika eneo la Olasiti kwa kuwa hakuna mgogoro na pindi watakapomaliza mgogoro na Halmashauri ya Arusha wataanza ujenzi katika Eneo la Moshono.

Katika ziara hiyo ambayo Mkuu wa mkoa aliongozana na kamati yake ya ulinzi na usalama ya mkoa na viongozi wa jiji la Arusha pamoja na meneja wa Tanesco na wawakilishi wa AUWSA na TARURA walipata fursa ya kutembelea na kukagua eneo litakapojengwa kituo hicho cha kisasa kukagua mradi wa umeme vijijini ikiwemo miradi ya Afya na Barabara ilikuweza kujionea changamoto mbali mbali wanazokutana nazo wananchi.

Nae Diwani wa kata ya Olasiti Alex Martini ameishukuru serikali ya awamu ya Tano kwa kupeleka miradi hiyo mikubwa katika kata hiyo jambo ambalo litakuwa chachu ya kukuza maendeleo katika eneo hilo.

Akaitaka serikali kuhakikisha inaondoa baadhi ya kero kwa wananchi wa kata hiyo ikiwemo suala zima la ubovu wa barabara jambo ambalo limekuwa ni kero kubwa hususani kipindi hicho cha mvua, sanjari na Kero ya maji ambayo imeonekana kuwa kubwa katika kata hiyo ikiwa ni kuharakisha mradi wa umeme vijijini Rea awamu ya Tatu.
Viongozi wa mkoa wakiongozwa na mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo walipotembelea eneo litakapojengwa Kituo kikuu cha mabasi mkoani hapa eneo la Olasiti nje kidogo ya jiji la Arusha (Picha na a Ahmed Mahmoud  Arusha)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad