HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 15, 2018

ASILIMIA 13-17 YA WATOTO WOTE WANAOZALIWA NCHINI HUZALIWA NJITI


Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
CHAMA cha Madaktari bingwa wa watoto nchini kimefanya kongamano lake la kwanza la kisayansi kwa watoto wachanga likiwa na kauli mbiu ya "Kila pumzi ni ya thamani" likiwa na malengo ya kufundisha watumishi wa afya jinsi ya kuwahudumia watoto wachanga ili kupunguza vifo vya watoto walio chini ya mwezi mmoja.

Akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa. Lawrence Museru amesema kuwa Tanzania inakabiliwa na tatizo kubwa la vifo vya watoto wachanga chini ya mwezi mmoja na asilimia kubwa ya watoto hao huwa  ni njiti na takwimu zinaonesha kuwa asilimia 13-17 ya watoto wanaozaliwa nchini huwa njiti.

Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imekuwa ikiripoti programu mbalimbali ambazo lengo lake ni kupunguza vifo vya watoto wachanga na wale walio chini ya miaka 5, programu hizo ni pamoja na zile za kumsaidia mtoto kupumua baada ya kuzaliwa pamoja na kupanua huduma za watoto wachanga kwa kujenga wodi za watoto wachanga katika hospitali za Wilaya na Halmashauri pamoja na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya kuhusiana na namna ya kuwahudumia watoto wachanga na programu hizo zimesaidia sana katika kupunguza vifo vya watoto wachanga.

Aidha amesema kuwa kuanzishwa kwa wodi za watoto wachanga itasaidia pia kutatua changamoto ya matibabu kwa watoto hao na maboresho yanayoendelea kufanyika yatasaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga na kuhakikisha watoto wachanga hasa njiti wanapata huduma bora zinazostahili.

Pia amewapongeza washiriki wa kongamono hilo ambao wametoka katika mikoa yote nchini na Zanzibar na kuwashauri kuwa watumie vizuri maarifa hayo katika kuboresha huduma kwa watoto katika maeneo waliyotoka na amewapongeza wanachama wa Chama cha Madaktari wa watoto nchini na hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuandaa mafunzo hayo na kuyafanya yawe endelevu ili kuweza kufikia malengo mkakati ya mwaka 2030 ya kuendelea kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa ujumla.

Kwa upande wake Rais wa chama cha Madaktari bingwa wa watoto nchini Dkt. Sekela Mwakyusa ameishukuru Serikali hasa kwa kuhakikisha kuwa kila hospitali inakuwa na wodi kwa ajili ya watoto wachanga licha ya kuwepo kwa changamoto za vifaa, madawa na mafunzo kwa wahudumu wa afya.

Dkt. Sekela amesema kuwa kwa wadau wa afya na taasisi binafsi zinakaribishwa katika kuunga mkono jitihada hizo za kuokoa maisha ya watoto wachanga nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad