HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, October 20, 2018

Benki ya Biashara ya Mkombozi yazindua Tawi la Morogoro

Benki ya Biashara Mkombozi imezindua rasmi Tawi la Morogoro ambalo limepandishwa hadhi kutoka kituo cha huduma za kifedha na sasa kuwa tawi kamili.

Zoezi hili linafanyika wiki moja tu baada ya Benki ya Biashara Mkombozi kuzindua Tawi la Tegeta ambalo pia lilikuwa kituo cha cha huduma za kifedha hapo awali.

 Ufunguzi wa Tawi hilo ulifanywa na Katibu Tawala Wilaya ya Morogoro Bi. Ruth John akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa,  wadau mbalimbali, wafanyakazi, wafanyabiashara na wateja wa Benki ya Biashara Mkombozi.

 Akizindua tawi hilo jipya, mgeni rasmi aliipongeza Benki ya Biashara Mkombozi kwa hatua iliyofikia na kusema uzoefu kutoka nchi nyingine unaonyesha kuwa wafanya biashara wadogo na wale wakati ni wadau muhimu sana katika kukuza uchumi na kuondoa umasikini.

“Hivyo napenda kuwapongeza benki ya Biashara Mkombozi kwa kuamua kuwafikia wadau hawa muhimu ambao baadhi ya taasisi za kifedha zinawatizama kama ni soko hatarishi katika biashara ya kukopesha,” alisema.

Mgeni rasmi pia aliipongeza Benki ya Biashara Mkombozi kwa kutoa huduma za kibenki kwa watanzania wote bila ubaguzi wa rangi, ukabila, dini, dhehebu tofauti na baadhi ya watu wanavyotafsiri kuwa ni benki ya kanisa tu.

 “Natambua kuwa bado tuna changamoto kubwa ya kuwafikia na kuwashawishi watanzania walio wengi kutumia huduma za fedha za kibenki. Rai yangu kwenu Uongozi na Wafanyakazi wa Benki ya Biashara Mkombozi ni kwamba, mjikite zaidi katika ubunifu ili kuweza kuwavutia kundi hili ambalo linahitaji huduma zenu lakini labda utambuzi bayana bado haujakuwepo,” alisema.

Alitoa wito kwa Benki ya Mkombozi pia ijitahidi kufahamu mahitaji halisi ya soko na hivyo kuboresha huduma zake na bidhaa ili ziendane na mahitaji. “Elimu juu ya fedha kwa wananchi (yaani Financial literacy) ni muhimu sana, naomba pia muweke nguvu zenu katika hili,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Benki ya Biashara Mkombozi Bw. Sylivester Kasikila akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo alisema Benki ya Biashara Mkombozi ilianzishwa miaka tisa iliyopita huku ikijipambanua kuwa ni benki yenye uadilifu (Bank with Integrity) ikibeba dira ya benki ambayo itatoa huduma za kibenki zenye suluhisho sahihi kiuchumi kwa jamii pana hapa nchini, yaani wateja wadogo, wa kati na wakubwa kwa maana ya kuwezesha jitihada zao anuai za kiuchumi.

“Leo benki inafungua Tawi hili likiwa ni tawi na nane (8) ikiwa ni juma moja kamili limepita baada ya shughuli kama hii kufanyika huko Dar Es Salaam ambapo Benki ilizindua Tawi la Tegeta,” alisema.

 Alisema Benki ilifungua Kituo cha Huduma za kifedha Morogoro tarehe Julai 23, 2016 na imepata mafanikio ya kuridhisha katika kipindi kifupi, mafanikio ambayo yamechochea maamuzi sahihi ya Benki kuomba kibali Benki Kuu ili kupandisha hadhi Kituo cha Huduma kiwe Tawi kamili. “Benki imepokelewa vema na wananchi wa kada zote ambao wameendelea kujipatia huduma za kibenki toka viunga vyote vya Mji wa Morogoro ikiwepo Wilaya za Mkoa huu pamoja na maeneo mengine jirani,” alisema Bw. Kasikila

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mjumbe wa Bodi ya Benki ya Biashara Mkombozi, Bw. Marcellino Kayombo akimwakilisha Mwenyekiti wa bodi hiyo alisema tangu kufunguliwa kwake benki imetoa fursa mbalimbali kwa jamii na taifa kwa ujumla.

 “Kwanza benki imetoa ajira kwa Watanzania na pili serikali nayo imefaidika na kodi mbalimbali zinazotokana na utendaji wa benki. Kwa sasa benki hii ina wafanyakazi 135 ikijumuisha hawa wa kituo chetu cha Morogoro ambacho leo hii kinakuwa tawi kamili, alisema.

Mkombozi Commercial Bank Plc ilianzishwa mwaka 2009 na kanisa la Katoliki Tanzania na taasisi zake kwa madhumuni ya kusaidia wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa kupata huduma za kifedha. 

Ili kutanua wigo zaidi, waanzilishi wa benki hiyo walitoa nafasi kwa watanzania wengine wakiwemo wafanyabiashara na wawekezaji na kuifanya Benki ya Biashara Mkombozi kuwa iliyo orodheshwa kwenye soko la hisa na mitaji.
 Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro, Ruth John  (wa tatu kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Tawi jipya la Morogoro la Benki ya Biashara ya Mkombozi  huku viongozi na wageni waalikwa wakishuhudia tukio hilo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro, Ruth John akijaza fomu ya kufungua akaunti katika Benki ya Biashara ya Mkombozi baada ya kuzindua tawi jipya la Morogoro. 

Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya Biashara ya Mkombozi Tawi la Morogoro wakifuatilia matukio ya uzinduzi wa tawi hilo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad