HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 6 September 2018

Madereva wasio na vyeti waaswa kuchangamkia fursa za mafunzo VETA

Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii
KAMANDA wa kikosi cha Usalama Barabarani Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Fortunatus Musilimu amewataka madereva nchini kuchangamkia fursa za mafunzo ya udereva bora katika vyuo mbalimbali ikiwemo vyuo vya VETA.

Akizungumza wakati wa mahafali ya mafunzo ya muda mfupi katika Chuo cha VETA Dar es Salaam Kamanda Musilimu alisema zoezi la ukaguzi wa vyeti kwa madereva litafanyika kama ilivyopangwa ambapo baada ya miezi mitano iliyotolewa na Jeshi la Polisi kwa madereva kurudi shuleni na kupata vyeti kumalizika, hakutakuwa na mjadala tena bali hatua stahiki zitachukuliwa.

“Nawakumbusha madereva kuwa mwezi mmoja umeisha katika ile miezi mitano iliyotolewa…. Nawasihi tena kutumia vizuri muda uliobaki wakasome…”Alisema

Alisema vyeti vyote vitatakiwa kuwa na sahihi ya Wakuu wa Usalama Barabarani wa Mikoa ili kuhakikisha hakuna udanganyifu katika upatikanaji wa vyeti hivyo.

Kamanda Musilimu aliwaasa vijana waliohitimu mafunzo katika chuo cha VETA kuhakikisha wanatumia vyema ujuzi walioupata kuanzisha shughuli zao za kujiingizia kipato kulingana na fani walizosoma.

Naye Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA Stella Ndimubenya aliwataka vijana kutumia vyema fursa zinazopatikana katika Halmashauri zao kuwa kuna fungu maalum kwa ajili ya kuwawezesha vijana kufanya shughuli za ujasiriamali wakiwa kwenye vikundi.

Awali, Mkuu wa Chuo hicho Douglas Kipokola alisema chuo chake kwa kushirikiana na chuo cha VETA Kihonda wamejipanga vyema kutoa mafunzo ya udereva bora kwa madereva wote wataohitaji kupata mafunzo hayo.

Alisema hivi karibuni chuo hicho kimeanza kutoa mafunzo kwa madereva wa magari makubwa/malori yanayobeba mizigo na kwamba mtaala wake umeshapitishwa ambapo mafunzo hayo yameanza kutolewa tarehe 3 Septemba mwaka huu huku kukiwa na madereva 30 wanaopata mafunzo kwa wamu ya kwanza.

Kipokola alisema katika mahafali hayo,jumla ya wanafunzi 1125 wamehitimu mafunzo ya muda mfupi na katika fani mbalimbali ikiwepo Udereva, Uendeshaji wa hiteli, uhazili, umeme, compyuta, mapishi, Nywele na urembo na ufundi wa magari.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani , Fortunatus Muslimu akizungumza katika mahafali ya Chuo cha Veta Changombe yaliyofanyika Chuoni hapo Jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA Stella Ndimubenya akizungumza katika mahali ya Chuo cha VETA Changombe kuhusiana na VETA katika uimarishaji katika utoaji wa Mafunzo ya Ufundi Stadi.

Mkuu wa Chuo VETA Chang’ombe Douglas Kipokola akitoa historia ya chuo katika uandaji wa nguvu kazi ya taifa yenye ujuzi.
 Sehemu ya wanafunzi wanaohitimu katika Chuo cha Veta Changombe.


 Picha mbalimbali za matukio katika mahafali ya Chuo cha VETA Chang'ombe.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad