HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 27 August 2018

Jukumu la kuendeleza Sanaa Nchini ni la Serikali ,Wadau wa Sanaa na Wananchi

Na Lorietha Laurence-WHUSM,Shinyanga.
Jukumu la kuendeleza sekta ya sanaa nchini ni la Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sanaa na wanachi ambao wako mstari wa mbele kuhakikisha sekta hiyo inaleta manufaa ndani na nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa Leah Kihimbi kwa niaba ya Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza katika halfa ya ufunguzi wa filamu ya Ruanda Mkoani Shinyanga.

Leah Kihimbi anaeleza kuwa Serikali kwa kuona umuhimu wa sekta ya sanaa nchini imeandaa Sera ya Maendeleo ya Sanaa itakayotoa muongozo kwa taifa kuhusu masuala yote ya sekta hiyo ikiwemo hakimiliki, urasimishaji wa kazi za sanaa na uendelezaji wa sekta hiyo nchini.

“Sera hii itakuwa dira na muongozo wa kazi zote za sanaa, hivyo kuwanufaisha wasanii pamoja na nchi” amesema Leah Kihimbi.

Aidha Leah Kihimbi amewapongeza wasanii kikundi cha Viwawada kwa kutoa filamu nzuri ya Ruanda ambayo inapinga na kukemea mimba na ndoa za utotoni, mauji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) na watu wenye umri mkubwa (Vikongwe).

Anazidi kueleza kuwa sanaa ni kioo cha jamii hivyo huangaza yale yote yanayotokea kupitia filamu ,muziki , ushairi na mengineyo ili kukemea, kuelimisha ,kuburudisha na kujenga jamii bora.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Mkoa wa Shinyanga (TDFAA) Mwl. John Tungu amemshukuru mgeni rasmi kwa kuweza kushirikiana nao katika ufunguziwa filamu hiyo,na kuahidi kuendelea kuwasimamia vyema wasanii hao ili kufikia lengo.

Kwa upande wake Afisa Utamaduni Mkoa wa Shinyanga Bi. Mariam Ally ameeleza kuwa wasanii wa Shinyanga, wako tayari kujifunza na kuhakikisha wanaipeleka sekta hiyo katika ngazi ya juu kwa kuzalisha waigizaji na filamu bora zaidi.

Filamu ya Ruanda imechezwa na wasanii wa Mkoa wa Shinyanga kwa kuhusisha madhari ya mkoa huo, lengo ikiwa ni kupinga na kukemea mimba na ndoa za utotoni, mauji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na watu wenye umri mkumbwa(vikongwe).
Afisa Utamaduni Mkoa wa Shinyanga Bi. Mariam Ally akiongea katika hafla ya ufunguzi wa filamu ya Ruanda iliyoigizwa na wasanii wa Viwawada wa Mkoa huo yenye maudhui ya kukemea na kupinga mimba na ndoa za utotoni, mauji ya watu wenye ulemevu wa ngozi (Albino) pamoja na watu wenye umri mkubwa (Vikongwe), jana Mkoani Shinyanga.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari ,Utamaduni,Sanaa na Michezo Leah Kihimbi akizungumza na wadau wa sanaa (hawapo katika picha) alipokuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Naibu Waziri wa Wizara hiyo katika halfa ya ufunguzi wa filamu ya Ruanda,jana Mkoani Shinyanga.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari ,Utamaduni,Sanaa na Michezo Leah Kihimbi (kushoto) akipokea risala kutoka kwa Bi. Elizabeth Vedastus (kulia) wakati ya halfa ya ufunguzi wa filamu ya Ruanda jana Mkoani Shinyanga.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari ,Utamaduni,Sanaa na Michezo Leah Kihimbi (kushoto) akisaidiana na Afisa Utamaduni wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Mariam Ally kufungua boski lilikuwa limewekwa CD ya filamu ya Ruanda ikiwa ni ishara ya kuizindua, jana Mkoani Shinyanga.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari ,Utamaduni,Sanaa na Michezo Leah Kihimbi akionyesha CD ya filamu ya Ruanda baada ya kuifungua rasmi wakati wa hafla hiyo jana Mkoani Shinyanga.

Wadau mbalimbali wa sanaa ambao walialikwa kuhudhuria halfa ya ufunguzi wa filamu ya Ruanda wakifuatilia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea katika halfa hiyo hapo Jana, Mkoani Shinyanga.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari ,Utamaduni,Sanaa na Michezo Leah Kihimbi (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na waigizaji wa filamu ya Ruanda mara baada ya kuifungua hapo jana Mkoani Shinyanga.
(Picha na Lorietha Laurence-WHUSM,Shinyanga)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad