HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 20 June 2018

MBUNGE KUBENEA ATOA USHAURI KWA SERIKALI KUBORESHA MRADI WA MABASI YA MWENDO KASI

*Uchache wa mabasi wasababisha mlundikano wa abiria vituoni

Humphrey Shao, Globu ya Jamii
MBUNGE wa Ubungo jijini Dar es Salaam Saed Kubenea ameishauri Serikali kuifuta kodi kwa mabasi ya mwendokasi 70 yanayotarajiwa kuingia nchini kwa lengo la kurahisisha usafiri katika mradi huo ambao kwa sasa unasua kutokana na kuzidiwa na wingi wa abiria.

Kubenea ametoa ushauri huo leo baada ya kutembelea Kituo cha mabasi ya Mwendokasi cha Kimara Mwisho ili kuangalia changamoto zilizopo katika mradi wa mabasi yaendayo Haraka (Udart).

Akiwa katika kituo hicho Kubenea ameambiwa changamoto kubwa iliyopo ni uhaba wa wa mabasi hayo ukilinganisha na wingi wa abiria wanaotumia usafiri huo.

"Niishauri Serikali ifute kodi ili haya mabasi yaweze kuingia au itoe muda fulani wa kulipa kodi angalau miezi sita hivi huku usafiri ukiendelea kutumika.

"Inawezekana mabasi hayo yanashindwa kuingia kwasababu mhusika amekosa kodi ya kulipa ndio maana yanachelewa na matokeo yake kusababisha adha ya usafiri kwa abiria kurundikana kwenye vituo kutokana na uhaba wa mabasi hayo,"amesema Kubenea.

Kubenea amesema wao kama wabunge wa Dar es Salaam pamoja na madiwani watahakikisha wanaulinda mradi huo ili udumu kwa ajili ya kizazi kijacho.

"Dar es Salaam ni kitovu cha nchi kibiashara, hivyo usafiri unapokuwa wa shida unaathiri mambo mengine. Sisi kama wabunge tunaowajibu wa kuulinda mradi huu na tutahakikisha tunaulinda,".

Ameongeza atazungumza na wabunge pamoja na Waziri wa Tamisemi kujua wanafanyaje kuulinda mradi huo pamoja na kupata eneo kwa ajili ya karakana.

Aidha Kubenea amesema mfumo mpya wa kielektroniki wa malipo serikalini (GePG) ni mzuri na utasaidia katika kuokoa wanaokwepa kodi na upotevu wa fedha.

Kwa upande wa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano (UDART), Deus Bugaywa amesema ni kweli wanakabiliwa na changamoto hiyo kutokana na abiria kuwa wengi kuliko mabasi yaliyopo.

Aidha amesema mbali na changamoto hiyo mafuriko yaliyotokea hivi karibuni yamefanya kampuni hiyo kutikisika, hivyo wanaomba kama kuna uwezekano wapate eneo lingine kwaajili ya karakana.

" Wakati tunaanza tulianza vizuri....muundo wa mradi ulikuwa yaingie 305 lakini yakaingizwa 140 kwaajili ya majaribio ambapo mwanzo tulikuwa tunahudumia abiria 50,000 kwa siku.

"Sasa hivi abiria wameongezeka tunahudumia abiria kati ya 150,000 hadi 200,000 kwa siku, hivyo utaona abiria wameongezeka lakini mabasi machache," amesema Bugaywa.

Pia amesema muda si mrefu mabasi 70 yataingia ambapo wanaimani yatasaidia kuondoa changamoto hiyo.

"Changamoto ya abiria tunaimani yakija mabasi haya itapungua...lakini tunaomba tupate eneo la karakana ambapo mabasi yatakuwa yanahudumiwa kama kawaida tofauti na eneo hili ambalo tunapata changamoto wakati wa mvua," amesema.

Akizungumzia tatizo la tiketi kutafanya kazi kwenye mageti ya kuscan, Bugaywa amesema hiyo inatokana na mabadiliko ya mfumo mpya wa malipo ambapo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Juni.

"Mageti ya kuscan tiketi hayafanyi kazi kwasasa mpaka pale mfumo utakapokamilika na hiyo itakuwa ni mwishoni mwa Juni kwa mujibu wa wataalam," amesema Bugaywa.

Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea akizungumza na Maofisa wa kitengo cha habari cha mradi wa mabasi yaendayo kasi (UDART) mara baad ya kutembelea mradi wa huo na kujionea mapungufu yaliyojitokeza na kusisitiza kuwa kila mbia ahakikishe changamoto zilizopo zinamalizika haraka.
 Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea akimsikiliza mmoja wa Watendaji wa kitengo cha habari katika mradi wa UDART , Joel Beda wakati alipofika  makao makuu ya ofisi hizo Jangwani jijini Dar es Salaam.
Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea akiwa ndani ya moja ya mabasi yaendayo kasi mara kuchanganyika na wananchi.
Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea akisikiliza maelekezo kutoka kwa mmoja ya watendaji wa UDART Katika kituo cha Kimara ambapo alikwenda kujionea msongamano wa abiria katika eneo hilo.
Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea akipita katika eneo la kupita abira kuingia kituoni mara baada ya kukata tiketi na kujinea changamoto iliyopo katika mfumo wa ukataji tiketi katika kituo hicho kutokana  kuwepokwa msonagamano mkubwa.
Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea akiwa katika foleni ya ukataji wa tiketi kwa mabasi yaendayo haraka UDART


Mmoja ya wakazi wa Kimara akitoa maoni yake kwa Waandishi wa Habari akiomba mradi huo uboreshwe zaidi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad