CHAMA
cha Wakunga Tanzania (TAMA) Tawi la Hospitali ya Taifa Muhimbili chini
ya udhamini mkuu wa Benki ya NMB kimetoa huduma za afya mbalimbali bure
jijini Dar es Salaam, ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya siku ya
wakunga duniani.
Akizungumza leo na mwandishi wa habari hizi katika tukio hilo
linaloendelea Hospitali ya Taifa Muhimbili jirani na jengo la watoto,
Mwenyekiti Msaidizi wa Chama cha Wakunga Tanzania tawi la Hospitali ya
Taifa Muhimbili, Bi. Elizabeth Thawe aliwataka wananchi kujitokeza
katika eneo hilo ili kuweza kupata huduma hizo za afya bure.
Alisema
huduma wanazotoa bure siku nzima ya leo ni pamoja saratani ya shingo ya
kizazi, saratani ya matiti, elimu kuhusu lishe bora, shinikizo la damu
(BP), sukari mwilini na elimu ya unyonyeshaji watoto kwa akinamama.
"Kuelekea maadhimisho ya siku yetu, tumejitolea kupima afya bure kwa
wananchi wote watakaojitokeza katika eneo hili...huduma zinazotolewa
bure leo ni pamoja na saratani ya shingo ya kizazi, saratani ya matiti,
tunatoa elimu kuhusu lishe bora, tunapima shinikizo la damu (BP),
tunapima sukari mwilini na elimu ya unyonyeshaji,
"
alisema Bi. Elizabeth Thawe.
Aliongeza kuwa huduma hizo zinatolewa kwa wanachama wa Chama cha Wakunga
Tanzania (TAMA) tawi la Muhimbili kwa kushirikiana na wengine kutoka
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Mifupa Muhimbili
(MOI) pamoja na vyuo vyote vya afya vinavyozunguka Hospitali ya
Muhimbili.
Alisema mbali na kutoa huduma hizo bure siku ya pili ya maadhimisho
(yaani Agosti 7, 2017) watafanya kongamano la kisayansi katika Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH) ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya siku
hiyo muhimu kwa wakunga.
Aidha
aliishukuru Benki ya NMB ambayo ni wadhamini wa kuu wa maadhimisho hayo
pamoja na makampuni mengine yaliojitokeza kusaidia kufanikisha shughuli
hizo.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia misululu ya wananchi waliojitokeza
kupata huduma za afya bure eneo hilo na wengine kuvutiwa na huduma za
NMB zilizotolewa eneo hilo, kuwaunganisha wananchi na huduma za kibenki.
Maofisa kutoka Benki ya NMB (kushoto) wakimfungulia akaunti mmoja wa
wateja (kulia) aliyejitokeza kupata huduma hizo katika kongamano la
Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) Tawi la Hospitali ya Taifa Muhimbili
ambapo mbali na huduma hizo za kibenki toka NMB, wananchi walipata
huduma mbalimbali za afya bure, ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya
siku ya wakunga duniani.
Sehemu ya wananchi wakiwa katika foleni kupata huduma za afya bure
zilizokuwa zinatolewa na Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) Tawi la
Hospitali ya Taifa Muhimbili leo.
No comments:
Post a Comment