Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba akiwa amembeba mtoto aliyezaliwa katika Hopsitali ya Wilaya (Dk. Jakaya Kikwete) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani kiwilaya.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Nyabaganga Talaba akimpa msaada mmoja wa mama anayeuguza mtoto katika hopsitali ya wilaya.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba akizungumza na wauguzi (hawapo pichani) katika sikukuu ya Wauguzi Duniani viwanja vya hospitali ya wilaya.
Katibu Tawala Wilaya ya Kishapu, Shadrack Kangese akitoa neno kumkaribisha mgeni rasmi mkuu wa wilaya
Wauguzi wakila kiapo cha utii wakati wa sikukuu hiyo.
Wauguzi wilayani Kishapu wamepongezwa kwa kazi nzuri na
kutakiwa kuendelea kuipenda kazi yao kuchapa kazi katika mazingira yoyote
waliopo kwani wao ni chachu ya afya katika jamii.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani
Shinyanga, Nyabaganga Talaba wakati kwenye kilele cha Siku ya Wauguzi Duniani
iliyofanyika katika viwanja vya Hospitali ya Wilaya ya DK. Jakaya Kikwete.
Talaba ambaye aliwaongoza wauguzi hao na watumishi wa
halmashauri kutoa misaada na kufariji wagonjwa hospitalini hapo aliwapongeza
kwa huduma nzuri kwa wagonjwa.
Alisema kuwa bila ya wauguzi afya haijakamilika na kuwa
uuguzi ni zaidi ya wito na ni huduma inayohitaji upendo na huruma kwa wale
unaowahudumia.
“Kama huna upendo na ukarimu basi wewe siyo muuguzi na
ukionesha ukarimu na upendo ndiyo mwanzo wa kupona kwa mgonjwa ukifika tu pale
mgonjwa anapona hata kabla hujampa dawa,” alisisitiza.
Aidha, aliwataka wauguzi waendelee kuwa na ushirikiano
baina yao huku akiwapongeza kwa mafanikio katika sekta ya afya pamoja na kuwa
wana changamoto ya mazingira ya kazi.
Mkuu huyo wa wilaya aliwaomba kuendelea kutimiza wajibu
na kuzingatia viapo vyao vya uuguzi na kanuni za utumishi huku akionya
kushindwa kufanya hivyo ni kukiuka taratibu za kazi na hivyo kutengeneza
migogoro isiyo ya lazima.
Kwa upande wake, Kaimu Muuguzi Mkuu Hospitali ya wilaya
hiyo ya Dk. Jakaya Kikwete, Rehema Jumanne akisoma risala alitaja mafanikio
yaliyopatikana kuwa ni mafunzo kazini.
Alisema mafunzo hayo yamesaidia wauguzi kuboresha
huduma za jamii zikiwemo uzazi wa mpango, huduma za dharura kwa wajawazito na
kusaidia wachanga kupumua.
Pia alitaja mafanikio mengine ni kuendeleza wauguzi katika
ngazi za juu za elimu na hivyo kutoa huduma kwa kiwango cha juu pamoja na kutoa
huduma bora tofauti na mazingira yao.
Hata hivyo alisema kuna changamoto ya uhaba wa
watumishi hiyo husababisha kutokuwepo kwa uwiano sawia wa watumishi katika
kutoa huduma katika vituo vya afya na zahanati mbalimbali katika wilaya hiyo.
Siku ya Wauguzi Duniani huadhimisha kila Mei 12 ikiwa
ni kumuenzi muuguzi mwanzilishi Florance
Nightingale aliyoanzisha mwaka 1844 ambapo kaulimbiu ni Wauguzi, mbiu ya
kuyafikia malengo endelevu ya millennia.
No comments:
Post a Comment