Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema
Serikali imejidhatiti kufanya maboresho makubwa ya kimiundombinu na rasilimali watu
katika sekta za uchukuzi ili kuiwezesha sekta hiyo kuongeza ajira na kukuza uchumi wa
nchi.
Prof. Mbarawa amesema hayo mara baada ya kukagua Chuo cha Taifa cha Usafirishaji
(NIT) na kusafiri wa boti kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar ikiwa ni mkakati wa
kupata taarifa sahihi kuhusu hali ilivyo sasa kutoka kwa abiria na waendeshaji wa
vyombo vya majini.
Amesema Serikali itaboresha Bandari ya Dar es Salaam ili kupunguza urasimu usio wa
lazima na kuwawezesha abiria na boti kukaguliwa kwa haraka na kuondoka kwa muda
unaotakiwa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akibadilishana
uzoefu na makapteni wa meli ya Azam aliposafiri na boti hiyo.
‘Tutahakikisha kuwa idadi ya manahodha na wahandisi wa vyombo vya majini
wazalendo inaongezeka ili mkakati wa kuboresha usafiri wa majini hapa nchini uwiane
na uwepo wa wataalam wa uhakika’ amesema Prof. Mbarawa.
Waziri huyo wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano amesema Serikali ina mpango wa
kujenga meli mpya za kisasa katika Ziwa Victoria ili kuhamasisha wasafirishaji katika
sekta ya usafiri majini kuwa na vyombo vya kisasa na hivyo kupunguza gharama za
usafiri.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT)
ambapo amesisitiza kuwa Serikali itaunga mkono juhudi zinazofanywa na Chuo hicho
katika kutoa mafunzo wa marubani wa ndege ili kuongeza idadi ya marubani
wazalendo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akikagua moja ya
darasa linalotumika kufundishia Marubani wa ndege alipokagua Chuo cha Taifa cha
Usafirishaji (NIT), jijini Dar es Salaam.
‘Mpango wetu wakukunua ndege mpya unaendana na kuwezesha Chuo hiki chenye
kufundisha marubani ili tuwe na marubani wazalendo wa kutosha’ amesisitiza Prof.
Mbarawa.
Amewataka wafanyakazi wa Chuo hicho kufanya kazi kwa uzalendo, ubunifu na
kuzingatia matokeo ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayokwenda
haraka.
Naye Mkuu wa Chuo hicho Profesa Zacharia Mganilwa amemhakikishia Waziri Prof.
Mbarawa kuwa chuo hicho kitashirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRL), Mamlaka ya
Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), Kampuni hodi ya Rasilimali za Reli (RAHCO)
katika kupata utaalam wa kisayansi katika mradi wa ujenzi wa reli ya kati ya Kisasa
kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Serikali imejipanga kujenga chuo cha kisasa cha Usafirishaji kwa kushirikiana na
Jamhuri ya Watu wa China ikiwa ni mkakati wa kukifanya chuo hicho kuwa chuo mahiri
katika upande wa Afrika Mashariki na Kati.
Zaidi ya Shilingi trilioni 4 zimetengwa na Serikali katika bajeti ya mwaka huu ili
kuimarisha miundombinu ya usafiri wa Angani, barabarani, relini na majini.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akipata maelezo
kuhusu uboreshwaji wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),kutoka kwa Mkuu wa
Chuo hicho Prof. Zacharia Mganilwa alipokagua chuo hicho jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akiongea na
wanafunzi wanaosoma kozi ya udereva alipotembelea Chuo cha Taifa cha Usafirishaji
(NIT), jijini Dar es Salaam. Kushoto (mwenye tai nyekundu) ni Mkuu wa Chuo hicho
Prof. Zacharia Mganilwa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akiongea na
mmoja wa abiria wanaotumia usafiri wa boti kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar,
na kujionea changamoto mbalimbali zinazowakabili abiria hao ambapo ameahidi
kuzipatia ufumbuzi hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment