Na Dac Popos.
Ligi kuu ya Uingereza almaarufu EPL inayotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao inatarajiwa kuwa yenye ushindani mkubwa sana hasa kutokana na usajili unaoendelea kufanywa na vilabu mbali mbali ili viweze kufanya vizuri na hatimaye kupata ubingwa wa ligi hiyo.
Sajili nyingi zinazoendelea zimewashitua wengi hasa sajili inayosemekena kufanyika usiku wa kuamkia leo Ijumaa, Julai 22, 2016 ni ya Paul Pogba kutoka Juventus kwenda Manchester United ambao utaweka rekodi ya dunia ya ada ya uhamisho, kiasi cha Pounds Milioni 120 kimetajwa kulipwa ili kufanikisha uhamisho huo.
Tukiacha mambo ya usajili tuangazie suala zima la makocha ambao wanatarajiwa kuviongoza vikosi vyao katika ligi hiyo ya nchini Uingereza, duru za kispoti zinasema kuwa ligi hiyo itakuwa na utamu wake ambao utachagizwa kwa kuwepo na makocha mbali mbali wenye sifa tofauti hasa wawapo kwenye mstari unaowatenganisha wao na uwanja.
Baadhi ya makochaa hao ni Jurgen Klopp wa Liverpool (Majogoo wa jiji), Jose Mourinho wa Manchester United (Mashetani wekundu), Pep Guardiola wa Manchester City (Matajiri wa mafuta), Antonio Conte wa Chelsea (The Blues) na Arsene Wenger wa Asernal (Washika mitutu). Makocha hawa wana sifa tofauti ndani na nje ya uwanja, lakini leo tutatazama sifa zao za ndani ya uwaja.
JURGEN KLOPP:
Anasifika zaidi kwa kuwahamasisha Wachezaji sambamba na Watazamaji, mara nyingi utakuta akiwakumbusha wachezaji wake wawapo uwanjani kujituma zaidi kukaba kuanzia (juu) yaani kwenye eneo la adui, na papo hapo yeye utamuona kana kwamba naye ni sehemu ya wachezaji kwa jinsi anavyokuwa na mdadi, jinsi anavyoshangilia pindi wanapopata goli na wakati fulani badala ya kutazama mpira huwa anawatazama watazamaji kuona namna gani wanawapa sapoti wachezaji wao.
JOSE MOURINHO:
Huyu anasifika sana kwa kuchonga sana (kuongea), mara kadhaa awapo uwanjani hupenda sana kuwapigia kelele wachezaji na waamuzi. Pia ni kocha mwenye dharau sana hata ambapo mchezo unaendelea yeye huweza kuonyesha dharau kwa wachezaji wa timu pinzani na kuweza kuwatoa mchezoni ili timu yake ipate matokeo mazuri. Lakini hiyo sifa yake ya kuwasemea hovyo waamuzi safari hii itaweza kumtokea puani kwani FA imepitisha sheria kuwa iwapo Mchezaji au Kocha yoyote atakayemkaripia mwamuzi basi atapewa kadi nyekundu na kuondolewa uwanjani.
PEP GUARDIOLA:
Watu hupenda kumuita Model kutokana na mavazi yake kuwa kama mwanamitindo. Yeye sifa yake ni kuona timu yake ikicheza soka la kuvutia, mara nyingi awapo uwanjani basi ni mtu wa kutao maelekezo kila dakika na kutazamia kile anachokitolea maelekezo kinafuatwa, na kama hakifuatwi basi si ajabu ukamuona kainama huku kashika kichwa chake ambacho huwa anakionyoa nywele (upara). Ni mpole kwa wachezaji wake.
ANTONIO CONTE:
Mzee wa suti, kocha huyu nadra sana kumuona amevaa mavazi tofauti na suti, muda wote wa mchezo huwa amesimama akitoa maelekezo ila ni vigumu kumgundua kuwa muda gani kafurahi au kachukia, furaha yake utaiona pale tu timu yake inapopata bao, afurahi na kushangilia lakini baada ya sekunde kadhaa anarudi katika hali yake ya utata.
ARSENE WENGER:
Huyu hutumia muda mrefu wa mchezo akiwa ameketi akibadilishana mawazo na msaidizi wake. Timu yake ikiwa inaongoza ndipo utamuona muda mrefu akiwa wima. Mzee huyu ni nadra sana kumuona akiwa anatoa maneno makali, na ukimkuta katika hali hiyo basi ujue maji yamezidi unga.
No comments:
Post a Comment