Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager ambayo ni mdhamini mkuu wa timu za Simba na Yanga zinazoshiriki ligi kuu ya soka ya Vodacom premier league leo imekabidhi vifaa mbalimbali vya michezo kwa timu hizi mbili kwa ajili ya kuvitumia katika maandalizi ya ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara mzunguko wa kwanza.
Akikabidhi vifaa hivyo mbele ya waandishi wa Habari jijini Dar es salaam Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Bw. George Kavishe alisema bia ya Kilimanjaro imekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu nchini.
Bw. Kavishe alisema vifaa vilivyokabidhiwa leo vina thamani ya shilingi milioni sitini na nne (64,000,000/=) na vitatumiwa na timu hizo kwenye mazoezi na michezo ya ligi ya Vodacom .
Aidha alisema udhamini wa bia ya Kilimanjaro kwa timu za Simba na Yanga unahusisha kupatiwa vifaa vya michezo kwa awamu mbili za ligi, awamu ya kwanza ikiwa ni kipindi cha mzunguko wa kwanza na awamu ya pili ikiwa ni Mzunguko wa pili,udhamini huu unahusisha pia kulipa mishahara kwa wachezaji na mabenchi ya ufundi ya timu hizo, ikumbukwe pia kwamba Kilimanjaro Premium Lager tayari ilishazipatia magari mawili kwa kila timu kwa ajili ya safari za timu na viongozi.
Alisema udhamini wa Bia ya Kilimanjaro kwa timu za Simba na Yanga ni sehemu ya mkakati mkubwa wa Bia hiyo wa kuhakikisha inafanikisha Soka la Tanzania kufikia kilele cha mafanikio.
“Kampuni ya Bia Nchini TBL kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager, inafofuraha kubwa kutoa vifaa vya maandalizi kwa timu za Simba na Yanga ambazo tumekuwa tukizidhamini kwa muda sasa na hakika zimekuwa na maendeleo na mafanikio makubwa kwenye ligi kuu ya mpira wa miguu hapa nchini na hii inatupa matumaini makubwa na leo tunakabidhi vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni sitini na nne kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa kwanza wa ligi kuu hapa nchini Tanzania na hii ni sehemu ya mkakati wa bia ya Kilimanjaro kuhakikisha soka la Tanzania lina kuwa na kufika kwenye kilele cha mafanikio .”Alisema bwana Kavishe.
Kwa upande wao wawakilishi wa timu hizo waliishukuru bia ya Kilimanjaro kwa kuendelea kuvidhamini vilabu hinyo na kuahidi kuendeleza makali yao pindi mzunguko wa kwanza wa ligi kuu utakapoanza Aug 21,2010.
Timu za Simba na Yanga zimekuwa zikishiriki ligi kuu ya Tanzania Bara kwa muda mrefu ambapo kwa msimu uliopita timu ya Simba iliibuka kidedea huku timu ya Yanga ikishika nafasi ya pili ambapo Simba italiwakilisha Taifa katika mashindano ya club Bingwa barani Africa huku Yanga nao wakishiriki kwenye mashindano ya shirikisho barani Africa.
No comments:
Post a Comment