HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, February 22, 2010

Miaka 45 Tangu Malcom X Kuondoka Duniani

Posti hii nilitakiwa kuipandisha jana lakini sikufanikiwa maana jana nilifunga kiroho na kifikra ili kumkumbuka Malcom X, mpigania haki za watu weusi kule Marikani. Malcom X alizaliwa na kupewa jina la Malcom Little kisha akaamua kubadili "Little" na kuweka "X" kwa kile alichodai kuwa jina la awali lilikuwa ni la kikoloni na lenye nia ya kuiba utu wake. "X" inasimama kama "Alieyepotea/Asiye na Jina" ikimaanisha Mwafrika aliyepoteza utambulisho wake baada ya kutekwa na kupelekwa utumwani kule Marikani.

Nimeona niweke posti hii ili tuelewe kwamba isingekuwa Malcom X na wengine waliotangulia kama Martin Luther King Jr., Mama Rosa Parks, au mapambano ya kuwakomboa watumwa ya "http://en.wikipedia.org/wiki/Underground_Railroad" target="_blank">Reli ya Ardhini" (Undeground Railroad) yaliyoongozwa na mwanamke mweusi Harieth Turbman, pengine Marekani ya leo isingekuwa na Rais Mweusi tunayemfahamu na kumshabikia, Barack Obama.

Malcom X alizaliwa katika familia yenye maisha duni na akiwa na umri wa miaka 13, baba yake ambaye alikuwa mpigania haki za watu weusi pia aliuawa na wazungu wabaguzi waliojulikana kama Ku Klux Klan (KKK), na mama yake alikuwa amefungiwa katika hospitali ya wagonjwa wa akili. Hivyo Malcom akaanza maisha ya kujitegemea akitumia wizi wa mifukoni kama njia ya kujipatia kipato.

Mwaka 1946 Malcom alifungwa jela kutokana na wizi. Akiwa Jela, Malcom ambaye hakuwahi kusoma vitabu akajikuta akiwa msomaji mkubwa wa vitabu ambavyo vilimwongezea maarifa aliyokuja kuyatumia baadae katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa watu weupe kwa watu weusi.

Malcom X aliwahi kusema, "Ukitaka kumshinda adui yako, jifunze lugha yake". Hivyo akiwa jela Malcom X mbali ya kusoma vitabu vingi changamoto aliyojiwekea ilikuwa ni kukariri Kamusi ya Kiingereza ya Oksfodi, changamoto ambayo aliweza kuivuka. Malcom aliweza kujieleza vyema katika mahakama na vyombo vya habari juu ya mapambano yake, kitu ambacho kiliwaudhi sana wazungu waliokuwa wakitaka kupindisha ujumbe wake.

Ukisoma kitabu chake cha "The Autobiography of Malcolm X" kuna wakati Maclom alikutana na dada wa kizungu aliyetamani kufanya kazi ya ukombozi na Malcom lakini Malcom akamwambia, "Mzungu ni mzungu tu hata kama roho yako ni nzuri lakini bado wewe ni mzungu, hatukuamini!" Dada yule akaondoka amefadhaika.

Lakini mwaka 1964 akapata bahati ya kwenda kuhiji Mecca, huko akakutana na Wazungu, Weusi, na Waasia ambao waliketi pamoja, wakila pamoja na kulala pamoja. Kufikia hatua hii Malcom X akagundua jambo moja na akasema katika barua yake iliyopewa jina la 'A Letter from Mecca', "Nimegundua kwamba tatizo sio wazungu (watu weupe) bali ni mfumo wa Kibepari wa Kimarekani". Baadae aliwahi kusema, alipokuwa akimzungumzia yule dada wa Kizungu, "Siku zote nimekuwa nikiomba Mungu anisaidie nikutane tena na dada yule ili nimwombe msamaha lakini sijafanikiwa, natumaini dada huyu asomapo kitabu changu (The Autobiography of Malcolm X) atanisamehe kwa ujinga wangu".

Ni mabadiliko ya falsafa ya Malcom X toka kwenye falsafa ya 'Jino kwa Jino' au Militant Philosophy kwenda falsafa ya 'Ukipigwa Shavu la Kulia Geuza na lile Lingine' ndio iliyomjengea uadui mkubwa zaidi na shirika la kijasusi la CIA na lile la kikachero la FBI ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakituhumiwa kuwa ndio waliopanga mauji ya Mtume huyu. Mashirika haya yaliogopa kwa sababu yaliona Malcom yuko njiani kuunganisha watu wa rangi zote kufikia lengo lake.

Februari 21, 1965 Malcom akihutubia mbele ya wafuasi wake 400, kati yao akiwemo mkewe na binti zake wanne, aliuawa kwa kupigwa risasi, mbaya zaidi ni kwamba waliofyatua risasi hizo walikuwa ni watu weusi wenzake. Zipo tetesi kwamba wauaji wake walikuwa ni wafuasi wa jumuiya ya Nation of Islam, ambao Maclom aliamua kuachana nao kutokana na kiongozi wa Jumuiya hiyo kwenda kinyume na mafundisho yake. Kila nikikumbuka mauaji haya ujumbe toka kwa Mtume mwingine, Bob Marley, huwa unarindima masikioni mwangu. Marley anauliza kwenye wimbo wake wa Redemption Song, "Mpaka lini wataendelea kuwaangamiza Mitume wetu nasi tukiwa tumesimama na kuangalia tu?/How long will they kill our prophets while we stand aside and look."

Tumia dakika tano kila unapoamka asubuhi kabla ya kupiga mswaki kufikiria mashujaa/manabii wako waliofanya uweze kuishi unavyoishi leo. Tumia dakika nyingine tano kufikiria ungependa watoto wako waishi vipi miaka michache tangu sasa.

Pia ukumbuke kwamba Mungu ametutumia Mitume mingi tu baada ya Yesu na Muhamad (Amani iwe juu yao), na bado anatutumia mitume mingi zaidi tatizo letu huwa hatuelewi wanachotufundisha, na tukielewa tunawaua ili kuwanyamazisha. Ukweli huu umefunikwa miaka mingi lakini sasa haufichiki tena.

Babukadja Sankofa
www.fotobaraza.ning.com

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad