Tanesco imetangaza kumalizika kwa mgawo wa umeme baada ya mashine moja ya Songas kutengenezwa jana na mafundi kutoka Marekani.Tangu Alhamisi iliyopita,Watanzania walianza kuonja machungu ya mgawo wa umeme baada ya Shirika la Umeme(Tanesco)kutoa ratiba ya mgawo wa saa 10.Mgawo huo ulitokana na kuharibika kwa mashine tatu kati ya sita za Songas.
Mitambo hiyo inazalisha umeme kwa kutumia gesi asilia ya Songosongo.Meneja Mawasiliano wa Tanesco,Badra Masoud alisema jana kuwa mashine moja kati ya tatu zilizoharibika imetengemaa baada ya mtaalamu kutoka Kampuni ya General Electric Marekani kuongoza matengenezo.
Alisema baada ya matengenezo hayo kukamilika kwa mtambo mmoja wa Songas, sasa zinazalishwa megawati 110 na mashine mbili zikikamilika mitambo hiyo itarudia kiwango chake cha kuzalisha megawati 180.
“Mashine moja imetengemaa kwa hiyo mgawo umeondolewa rasmi kuanzia leo (jana) kwani tunapata megawati 110 kutoka Songas,”alisema Masoud ambaye ndiye aliyetangaza mgawo wa saa 10 katika baadhi ya miji ya Bara na Zanzibar.Mtaalamu huyo kutoka Kampuni ya General Electric (GE), aliwasili Jumamosi kwa ajili ya kutathmini ubovu wa mashine hizo na kutoa ushauri kwa Songas na kwa Tanesco.
Songas inazalisha megawati 180 za umeme na inauza wote kwa Tanesco, kuharibika kwa mashine hizo tatu kulichangia upungufu wa umeme hali iliyolazimu Tanesco kutangaza mgawo. Mgawo wa umeme ulikuwa unaanza saa sita mchana hadi saa 4.30 za usiku,hali ambayo iliathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kiuchumi na biashara za wajasiriamali.
Baada ya mgawo huo kuanza,Waziri wa Nishati William Ngeleja aliwaondoa hofu Watanzania kwa kusema tatizo la mashine hizo halikuwa kubwa na lingetengemaa katika kipindi kifupi.Mgawo huo haukuhusu maeneo nyeti kama Ikulu,maeneo ya jeshi,Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na maeneo ya viwanda ili kutoathiri shughuli za kiuchumi.
No comments:
Post a Comment