HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 9, 2026

KUTOKA Wazo la COSTECH hadi Chakula cha Kuku Kinachopunguza Gharama za Ufugaji

 

Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
MWAKA 2018, Whitefrank Frank alikuwa mwanafunzi aliyemaliza kidato cha sita akiwa na wazo la kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wafugaji wa kuku nchini. Miaka minane baadaye, wazo hilo limezaa teknolojia ya chakula cha kuku inayolenga kupunguza gharama za uzalishaji kwa takribani asilimia 20 huku ikiongeza tija kwa wafugaji.

Kupitia kampuni yake ya Afrimix Animal Feeds, Dkt. Frank na timu yake wamebuni chakula cha kuku wa nyama kinachotumia malighafi zinazopatikana nchini na kinacholenga kuongeza uzito wa kuku kwa muda mfupi bila kutumia kemikali za kuchochea ukuaji.

Anasema safari hiyo ilianza baada ya kufanya tafiti kwa wafugaji wa kuku wa kisasa na wa kienyeji ili kubaini changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za kila siku.

Matokeo ya tafiti hizo yalionesha kuwa gharama za chakula na matibabu ni miongoni mwa vikwazo vikubwa vinavyopunguza faida kwa wafugaji wengi.

Dkt. Frank anasema wafugaji wengi hutumia fedha nyingi kuanzia kununua vifaranga, chakula, chanjo hadi dawa za kutibu magonjwa mbalimbali yanayoathiri mifugo yao.

"Nimekulia katika mazingira ya kifugaji, hivyo hali hii ilinifanya kuanza kutafuta njia ya kutengeneza chakula cha kuku chenye ubora unaohitajika lakini kwa gharama nafuu zaidi," anaeleza.

Anasema jitihada zake zilianza kuzaa matunda mwaka 2021 alipopata ufadhili wa awali kupitia programu ya MAKISATU inayoratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

"Nilipata ufadhili wa dola za Marekani 5,700 ambao uliniwezesha kuboresha ubunifu wangu na kuanza kufanya majaribio ya kisayansi," anasisitiza.

Dkt. Frank anasema kuwa kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), timu hiyo ilifanya majaribio kwa kutumia vifaranga 800 ili kupima ufanisi wa chakula hicho kwa kuku wa nyama.

"Matokeo ya majaribio yalionesha kuwa kuku waliolishwa chakula chetu waliweza kufikia uzito wa kati ya kilogramu 1.5 hadi mbili kwa muda unaokubalika kibiashara huku gharama za uzalishaji zikishuka kwa takribani asilimia 20 ikilinganishwa na baadhi ya mifumo inayotumika sasa," anafafanua.

Kwa mujibu wa Dkt. Frank, moja ya sababu zinazofanya chakula cha kuku wa nyama kuwa ghali ni mfumo wa lishe unaolazimika kuharakisha ukuaji wa kuku ili kufikia uzito wa soko ndani ya muda mfupi.

Hata hivyo, anasema utafiti wao umeonesha kuwa malighafi za ndani zinaweza kutumika kutengeneza chakula chenye matokeo mazuri bila kuongeza gharama kwa mfugaji.

Mbali na kuongeza uzito wa kuku, anasema chakula hicho kimeonesha uwezo wa kusaidia kuku kujenga kinga ya asili ya mwili, jambo linaloweza kupunguza gharama za matibabu na matumizi ya dawa.

“Hatuongezi kemikali za kukuza ukuaji. Tunachofanya ni kuhakikisha kuku wanapata lishe sahihi inayowawezesha kukua vizuri na kufikia uzito unaohitajika kwa muda mfupi,” anasema.

Anabainisha kuwa teknolojia hiyo inaweza kusaidia kupunguza muda ambao mfugaji anasubiri kabla ya kuuza kuku wake, jambo linaloongeza mzunguko wa uzalishaji na mapato.

Licha ya mafanikio hayo, Dkt. Frank anaamini bado kuna changamoto za kisera zinazohitaji kufanyiwa kazi ili kuongeza tija katika sekta ya ufugaji wa kuku.

Miongoni mwa changamoto hizo ni mfumo wa kuuza kuku kwa idadi badala ya uzito.
Anasema mfumo wa kuuza kuku kwa uzito ungeweza kuwapa motisha wafugaji na wabunifu kuwekeza zaidi katika teknolojia zinazoongeza ubora na uzito wa kuku.

Kwa kufanya hivyo, wafugaji wangepata thamani halisi ya uwekezaji wao na kuongeza tija katika sekta hiyo.

Wakati huo huo, anaeleza kuwa changamoto nyingine inayowakabili wafugaji wengi ni kutofuata kanuni bora za ufugaji, ikiwemo usafi wa mabanda, udhibiti wa magonjwa na upatikanaji wa elimu sahihi kuhusu lishe ya kuku.

“Wafugaji wengi wameaminishwa kuwa kuku lazima walishwe aina fulani ya chakula pekee. Ukweli ni kwamba jambo muhimu ni kuhakikisha wanapata virutubisho vinavyohitajika na kufuata kanuni bora za ufugaji,” anasema.

Anafafanua kwamba Afrimix Animal Feeds ipo katika hatua za kuanza uzalishaji wa kibiashara wa chakula hicho ili kuwafikia wafugaji wengi zaidi.

Mpango wa awali ni kuanza katika mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Morogoro kabla ya kupanua huduma katika Singida, Dodoma, Arusha na Kilimanjaro.

Dkt. Frank anaamini mahitaji ya chakula cha kuku nchini bado ni makubwa na yanatoa nafasi kwa wabunifu na wawekezaji kuingia katika sekta hiyo.

Anasema kuongeza uzalishaji wa chakula bora cha mifugo kutasaidia kuvutia watu wengi zaidi kuingia kwenye ufugaji wa kuku na kuongeza upatikanaji wa protini kwa wananchi.

Kwa mtazamo wake, ubunifu wa ndani una nafasi kubwa katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayosisitiza matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo za kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuimarisha usalama wa chakula.

“Tunataka kujenga kampuni inayotegemea tafiti na ubunifu katika kutatua changamoto za wafugaji. Tukiwasaidia wafugaji wadogo kuongeza faida, tutakuwa pia tunachangia ukuaji wa sekta binafsi na maendeleo ya taifa kwa ujumla,” anasema.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad