Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Reuben Kwagilwa akizungumza waandishi wa Habari wakati akifungua mafunzo kuhusiana umuhinu wa waandishi wa habari kutoa uelewa wa Biashara ya kaboni kwa Wananchi.
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imeongeza juhudi za kuiwezesha Tanzania kushiriki kikamilifu katika masoko ya kimataifa ya kaboni ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Reuben Kwagilwa wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam yaliyoratibiwa na Kituo cha Kitaifa cha Kufuatilia Kaboni (NCMC).
Kwagilwa amesema waandishi wa habari ni nguzo muhimu katika kuelimisha wananchi kuhusu biashara ya kaboni na namna wanavyoweza kunufaika nayo kiuchumi pamoja na kusaidia uhifadhi wa mazingira.
Aidha, amesema masoko ya kaboni yana lengo la kuhamasisha shughuli za utunzaji mazingira ikiwemo upandaji miti na matumizi ya nishati mbadala isiyoharibu mazingira.
Amesema hali ya ukataji miti nchini bado ni changamoto kubwa huku takribani hekta 370 za misitu zikikatwa kila mwaka kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kibinadamu.
“Mafunzo haya yana lengo la kuongeza uelewa kuhusu biashara ya kaboni na namna Watanzania wanavyoweza kunufaika nayo kiuchumi na kimazingira,” amesema Kwagilwa.
Kwa upande wake, viongozi wa Kituo cha Kitaifa cha Kufuatilia Kaboni (NCMC) wamesema taasisi hiyo pamoja na bodi yake zinaendelea kuratibu biashara ya kaboni nchini ili kuhakikisha Tanzania inanufaika na masoko ya kimataifa ya biashara hiyo.
“Tunaomba vyombo vya habari muendelee kushika mkono taasisi hii ili wananchi waweze kuelewa fursa hii muhimu kwa taifa,” amesema mmoja wa viongozi wa kituo hicho.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Upimaji, Uhakiki, Usajili pamoja na Tathmini ya Gesijoto katika NCMC, Deo Shirima amesema biashara ya kaboni inahusisha shughuli zote zinazosaidia kupunguza, kuzuia au kuondoa gesijoto zinazosababisha mabadiliko ya tabianchi.
Shirima amesema biashara hiyo haihusiani na misitu pekee, bali pia inagusa sekta za taka, nishati, viwanda pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi zinazosaidia kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.
“Kila mtu anaweza kushiriki katika biashara hii, awe kampuni binafsi, mtu mmoja mmoja au jamii, mradi afuate taratibu na ithibati zilizowekwa na serikali,” amesema Shirima.
Amesema hadi sasa yapo makampuni takribani 99 yaliyopo katika hatua mbalimbali za usajili wa miradi ya kaboni nchini, huku makampuni manane tayari yakiwa yameanza utekelezaji wa miradi hiyo.
Katika mafanikio ya biashara hiyo, Shirima ametolea mfano wananchi wa Wilaya ya Tanganyika ambao walipokea takribani Sh bilioni 14 mwaka 2024 kutokana na juhudi za usimamizi wa misitu kupitia biashara ya kaboni.
Amesema Tanzania inashiriki katika masoko rasmi na yasiyo rasmi ya kaboni ambapo wanunuzi wake wanaweza kuwa mataifa, kampuni au watu binafsi wanaotaka kufidia uzalishaji wa gesijoto.
Kituo cha Kitaifa cha Kufuatilia Kaboni (NCMC), ambacho sasa kina makao makuu yake Dodoma baada ya kuhamishwa kutoka Morogoro na kupewa hadhi ya taasisi kamili ya serikali, kimesema kitaendelea kushirikiana na vyombo vya habari kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu biashara ya kaboni na fursa zake kwa maendeleo ya taifa.




No comments:
Post a Comment