Friday, February 6, 2026

CEOrt Yasaini Makubaliano na CBE, IAA Kuendeleza sekta ya elimu, viwanda na biashara

 

Mwenyekiti wa CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) David Tarimo akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusaini hati ya makubaliano kati  Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA)pamoja na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) katika hafla iliyofanyika katika Makao Mkuu ya CEOrt Masaki jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Profesa Eliamani Sedoyeka  akizungumza kuhusiana na hati ya makubaliano kati IAA na CEOrt katika kutoa elimu inayokidhi katika soko la ajira ambapo ajira hizo ziko CEOrt,Masaki jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) David Tarimo na Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha(IAA) Profesa Eliamani Sedoyeka  wakisaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika   hafla iliyofanyika Makao Mkuu ya CEOrt Masaki jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
JUKWAA la Watendaji Wakuu nchini (CEOrt- Roundtable of Tanzania) limesaini Hati za Makubaliano (MoU) na Vyuo Vikuu viwili nchini, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya elimu, viwanda/ biashara ili kuwaandaa wahitimu wenye ujuzi, maarifa na uwezo unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na ushindani .

Makubaliano hayo yanalenga kuunganisha uzoefu wa vitendo wa sekta ya viwanda/biashara  na programu za kitaaluma za vyuo hivyo, kujenga uwezo wa wanafunzi na wahadhiri, pamoja na kuweka mifumo endelevu ya kubadilishana maarifa na uzoefu kati ya viongozi wa biashara na taasisi za elimu ya juu.

Ushirikiano huu unatambua kuwa maendeleo ya Tanzania yanahitaji wahitimu wenye uwezo wa kutumia nadharia walizojifunza darasani katika mazingira halisi ya kazi, wakisaidiwa na viongozi wa biashara wanaoelewa mwelekeo wa uchumi unaokua, changamoto zake na fursa zinazojitokeza.

Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo katika ofisi za CEOrt zilizopo Masaki, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CEOrt, Bw. David Tarimo, alisema kuwa CEOrt kwa kushirikiana na IAA na CBE imeanzisha mfumo wa kimkakati wa kitaifa unaolenga kuimarisha uhusiano kati ya sekta ya elimu na sekta ya viwanda/ biashara, hususan katika maeneo ya utafiti, ushauri elekezi na maendeleo ya rasilimali watu.

Bw. Tarimo alisema kuwa kupitia ushirikiano huo, CEOrt yenye makampuni wanachama zaidi ya 235 kutoka sekta binafsi itatumia uzoefu wake wa kibiashara kuchangia katika kuchambua changamoto za mazingira ya biashara na uchumi zinazoikabili nchi, na kushiriki katika kubuni suluhisho la pamoja lenye matokeo chanya kwa maendeleo ya taifa.

Aliongeza kuwa ushirikiano huo pia utavijengea uwezo vyuo hivyo katika kufanya tafiti, sambamba na kuwapa wanafunzi wanaojifunza kwa vitendo fursa ya kukabiliana na changamoto halisi za soko la biashara la sasa.

“CEOrt kupitia makampuni wanachama wake ni miongoni mwa waajiri wakubwa katika sekta binafsi nchini, hivyo ushirikiano huu utatusaidia kwa pamoja kuandaa vijana waliopo vyuoni ili waendane na mahitaji halisi ya soko la ajira,” alisema Bw. Tarimo.

Alisema makubaliano hayo yamejengwa juu ya dira ya pamoja ya kuoanisha elimu na mahitaji ya ulimwengu wa biashara, kuendeleza taaluma, na kuchangia ukuaji endelevu wa uchumi kwa kuunganisha vyumba vya madarasa na bodi za wakurugenzi zenye uzoefu wa kibiashara.

Bw. Tarimo alifafanua kuwa makubaliano hayo na vyuo hivyo yanaongozwa na malengo ya msingi yanayofanana, yakiwemo kuingiza uzoefu wa sekta ya biashara katika mitaala ya vyuo, kujenga ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira kwa wanafunzi na wahadhiri, pamoja na kuimarisha mifumo rasmi ya kubadilishana maarifa kati ya viongozi wa biashara na taasisi za elimu ya juu.

Aliongeza kuwa nguzo kuu ya Hati za Makubaliano hayo ni ushirikiano katika utafiti na ushauri elekezi, ambapo wanachama wa CEOrt watatumia uzoefu wao wa kibiashara kuchangia katika kutatua changamoto muhimu za biashara na uchumi zinazoikabili Tanzania.

Kwa mujibu wa Bw. Tarimo, mfumo huo wa utafiti unaotokana na vitendo unalenga kuzalisha suluhisho zenye athari halisi kwa jamii na uchumi, huku ukiimarisha uwezo wa utafiti wa IAA na CBE, na kuwapa wanafunzi fursa ya kushiriki moja kwa moja katika utatuzi wa changamoto zinazoikabili sekta ya biashara na uongozi hapa nchini.

Aidha, alisema kuwa ushirikiano huo unaanzisha mifumo rasmi ya ushiriki kupitia mafunzo ya ziada na mihadhara ya wazi kwa umma, itakayowakutanisha wahadhiri, wanafunzi na wataalamu wa sekta za biashara, uongozi na uchumi. 

Katika mpango huo, wanachama wa CEOrt pamoja na wahitimu wa Mpango wa Mafunzo ya Uongozi kwa Wakurugenzi Wakuu (CEOrt Apprenticeship Programme – CAP) watashiriki kama wahadhiri wa ziada, wakileta uzoefu wa vitendo darasani.

Bw. Tarimo alisema makubaliano hayo pia yanalenga ujenzi wa uwezo wa muda mrefu kupitia programu za maendeleo ya uongozi, mafunzo ya uendelevu, kozi fupi na mafunzo ya vitendo.

Kwa upande wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), alisema mpango wa Mafunzo ya Uendelevu kwa Mameneja wa CEOrt utakuwa sehemu ya mitaala ya chuo hicho, huku pande zote zikitarajia kuendesha mafunzo ya viongozi waandamizi, programu za uongozi, ushauri elekezi na kambi za mafunzo ya uongozi.

Kwa upande wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), ushirikiano huo utajumuisha kozi fupi, mafunzo yanayoongozwa na sekta ya biashara, pamoja na mafunzo kwa vitendo kupitia viambatanisho vya kazi (field attachments) na mafunzo kwa vitendo (internships), ili kuhakikisha wahitimu wanahitimu wakiwa na ujuzi, uzoefu na mtazamo unaowawezesha kuchangia kikamilifu katika mageuzi ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania katika dunia ya sasa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Profesa Eliamani Sedoyeka, alisema ushirikiano huo una mchango mkubwa katika kuzalisha viongozi na wataalamu wenye ushindani katika sekta ya biashara nchini.

Naye Profesa Robert Mashenene,  Makamu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) anayesimamia taaluma, Ushauri na Utafiti, alisema makubaliano hayo yatasaidia kupunguza pengo la uzoefu wa vitendo lililopo kwa kuwapa wanafunzi fursa za kujifunza moja kwa moja kutoka kwa vinara wa biashara.

“CEOrt ina uzoefu mkubwa katika masuala ya uongozi na biashara, hivyo maarifa haya yatawasaidia sana wanafunzi wetu ambao kwa sasa wengi wao hujifunza kwa nadharia darasani.

“Ushirikiano huu utawaunganisha na viongozi wa sekta binafsi kutoka nyanja mbalimbali za biashara, jambo litakalosaidia kuongeza ushindani wao katika soko la ajira na mchango wao katika uchumi wa taifa,” alisema Profesa Mashenene.

Mwenyekiti wa CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) David Tarimo na Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha(IAA) Profesa Eliamani Sedoyeka  wakibadilishana hati ya  ya makubaliano ya Ushirikiano katika  hafla iliyofanyika  Makao Mkuu ya CEOrt Masaki jijini Dar es Salaam.
Makamu Mkuu wa Chuo,  Taaluma , Tafiti na Ushauri wa Chuo cha Elimu ya Buashara (CBE) Profesa Robert Mashenene akizungumza kuhusiana na hati ya makubaliano kati CBE na CEOrt katika kutoa elimu inayokidhi katika soko la ajira  ambapo ajira hizo ziko CEOrt,Masaki jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) David Tarimo na Makamu Mkuu wa Chuo,  Taaluma , Tafiti na Ushauri wa Chuo cha Elimu ya Buashara (CBE) Profesa Robert Mashenene wakisaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika   hafla iliyofanyika Makao Mkuu ya CEOrt Masaki jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) David Tarimo na Makamu Mkuu wa Chuo,  Taaluma , Tafiti na Ushauri wa Chuo cha Elimu ya Buashara (CBE) Profesa Robert Mashenene  wakibadilishana hati ya  ya makubaliano ya Ushirikiano katika  hafla iliyofanyika  Makao Mkuu ya CEOrt Masaki jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment