Friday, January 23, 2026

TCAA YAIMARISHA USALAMA WA ANGA KWA MIFUMO YA KISASA

 


Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imesema imejizatiti kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani, ikiwemo matumizi ya Akili Mnemba (AI), ili kuendelea kuimarisha usalama na ufanisi wa usimamizi wa anga nchini. Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Bw. Salim Msangi, wakati akifungua Mkutano wa 45 wa Mwaka wa Chama cha Waongoza Ndege Tanzania (TATCA).

Akizungumza katika mkutano huo, Msangi alisema, “TCAA itaendelea kutenga bajeti ya kila mwaka kwa ajili ya mafunzo ya wataalam wa anga ili kuhakikisha wanaendana na mabadiliko ya teknolojia na kudumisha viwango vya juu vya usalama.”

Msangi ameongeza kuwa mamlaka hiyo tayari imefanikiwa kufunga mifumo ya kisasa ya mawasiliano katika viwanja 15 vya ndege nchini, hatua itakayoongeza ufanisi wa mawasiliano kati ya marubani na waongoza ndege.

Amesema anga la Tanzania limeendelea kuwa salama na la kuaminika, hali iliyochangia ongezeko la ndege zinazopita katika anga la nchi kutokana na uwepo wa mifumo imara ya mawasiliano na uongozaji ndege.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Waongoza Ndege Tanzania (TATCA), Merkiory Ndaboya, amesema mkutano wa 45 wa mwaka wa chama hicho ni jukwaa muhimu kwa wataalam wa anga kujadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo na kuweka mikakati ya kuimarisha ufanisi.

Ndaboya amepongeza hatua zinazochukuliwa na TCAA kuimarisha mifumo ya kisasa ya anga na kusema chama hicho kitaendelea kushirikiana na mamlaka hiyo kwa lengo la kuboresha usalama na huduma za anga nchini.

Mkutano wa 45 wa TATCA umefanyika chini ya kaulimbiu ya “Ajira na Mafunzo kwa Usimamizi Endelevu wa Anga”, ukikusanya wataalam wa anga kutoka ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi akizungumza na wataalam wa Chama cha Waongoza Ndege Tanzania (TATCA) kuhusu namna Mamlaka hiyo ilivyojipanga kuwawezesha waongozaji ndege kufanya kazi kwa weledi na ufanisi wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 45 wa mwaka uliofanyika Januari 23, 2026 jijini Dar es Salaam.
Rais wa Chama cha Waongozaji ndege Tanzania (TATCA), Merkiory Ndaboya akizungumza kuhusu namna chama hicho kilivyoweza kuwakusanya na kuwaratibu waongoza ndege nchini Tanzania wakati wa kufunguzi wa Mkutano wa 45 wa TATCA.
Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi wa Mitambo ya Kuogozea Ndege, Mhandisi Zawadi Maalimu aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Huduma za Uongozaji Ndege akitoa neno kwenye mkutano Mkutano wa 45 wa Chama cha Waongozaji ndege Tanzania (TATCA).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi akitoa zawadi kwa baadhi ya Waongoza Ndege wastaafu kwa kutambua mchango wao wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 45 wa mwaka uliofanyika Januari 23, 2026 jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wanachama wa Chama cha Waongoza ndege Tanzania (TATCA) pamoja na viongozi wa TCAA wakisikiliza hotuba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi alipokuwa anafungua mkutano mkuu wa 45 wa mwaka uliofanyika Januari 23, 2026 jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi akiwa kwenye picha ya pamoja na waongoza ndege Tanzania waliohudhuria mkutano wa 45 wa Chama cha Waongozaji ndege Tanzania (TATCA) uliofanyika Januari 23, 2026 jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment