Friday, November 28, 2025

Benki ya I&M Yazindua Rasmi Huduma ya Asset Finance, Yakabidhi Magari 15 kwa Mteja

* Yafikia mafanikio ya TZS bilioni 508 katika ufadhili wa mali


BENKI I&M Tanzania leo imezindua rasmi huduma yake ya Ufadhili wa Mali (Asset Finance), inayolenga kuwezesha umiliki wa mali kwa urahisi na kwa gharama nafuu kwa Makampuni na Wateja wa Kipato cha Juu na kati kote nchini.

Hafla hiyo mahususi, iliyofanyika Mahindra Tanzania, ilishuhudia makabidhiano ya magari mapya 25 yaliyofadhiliwa na I&M Bank Tanzania kwa mmoja wa wateja wake wa kimkakati, ikiashiria manufaa ya haraka na ufanisi wa suluhisho hili jipya.

Kupitia huduma hii ya Ufadhili wa Mali, wateja wanaostahili wanaweza kupata magari mapya pamoja na vifaa vingine muhimu kwa ufadhili wa hadi asilimia 90 ya gharama, na masharti nafuu ya marejesho ya hadi miezi 60. Bidhaa hii pia imeambatanishwa na huduma za kuongeza thamani kama vile bima, ufadhili wa bima (premium financing), na usaidizi na usimamizi maalum kupitia maafisa mahususi wa mahusiano.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Bw. Simon Gachahi, Mkuu Kitengo cha Rejareja na Huduma za Kidijitali I&M Bank Tanzania, amesema:

“Hatujazindua tu huduma ya ufadhili wa mali pia tunatoa suluhisho jumuishi za bima, chaguo la ufadhili wa malipo ya bima, na usimamizi wa karibu wa maafisa wetu wa mahusiano. Ushirikiano wetu na Mahindra Tanzania unahakikisha wateja wanapata urahisi na suluhisho maalum kwa mahitaji yao ya kibiashara hususani zinazohusiana na magari kama usafirishaji.”

Kwa upande wake, Bw. Emmanuel Wilson, Mkuu wa Kitengo cha Mikopo I&M Bank Tanzania, ameongeza:

“Hatua hii inaonyesha imani yetu kubwa kwa soko la Tanzania na uimara wa mfumo wetu wa kutoa mikopo. Kwa kufadhili hadi asilimia 90 ya thamani ya mali kwa utaratibu thabiti, tunavunja vikwazo kwa biashara ndogo na kati ( SMEs ) na makampuni makubwa huku tukiendelee kutoa viwango vya juu vya usimamizi kwa wateja wetu. Makabidhiano ya leo ya magari 25 ni mwanzo tu. Tuko tayari kikamilifu kusaidia maelfu ya biashara kupata mali za uzalishaji wanazohitaji ili kustawi.”

Uzinduzi huu unaimarisha dhamira thabiti ya I&M Bank Tanzania kwa biashara ndogo na za kati (SMEs), ambazo ndizo uti wa mgongo wa uchumi wa taifa letu. Zikiwa zaidi ya biashara milioni 3 zinazochangia kati ya 27–35% ya Pato la Taifa na kuajiri zaidi ya watu milioni 5, SMEs zinabaki kuwa kipaumbele cha kimkakati kwa Benki.

Benki ya I&M Tanzania inapoharakisha safari yake kuelekea hadhi ya Tier 1 ifikapo mwaka 2026, inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika teknolojia ya kisasa, maendeleo ya jamii, na ubunifu unaomlenga mteja.

Naye Mkurugenzi wa mauzo kutoka kapuni ya GF Automobile Mujtaba Karmali ameishukuru serikali kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji nchini ambapo wanatarajia kuanzisha kuwanda cha kuunganisha magari na hivyo kuiomba serikali kutoa kipaumbele kwa makuampuni ya ndani ili kuongeza wigo wa ajira na kukuza mapato ya serikali.


Tumefurahi sana kushirikiana na Benki ya I&M pamoja na Synarete katika kufadhili mteja wetu mkubwa, ambaye amenunua magari 26 yanayoweza kufanya kazi katika mazingira yoyote.

Tunatarajia kuendeleza ushirikiano huu kwa manufaa ya wateja wetu na maendeleo ya sekta ya usafirishaji nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Synarete, Deep Joshi ameishukuru GF Automobile pamoja na Benki ya I&M kwa ushirikiano mzuri uliowezesha wadau wote kuweka malengo sawa katika kufanikisha upatikanaji wa magari maalum kwa ajili ya kuwawezesha mainjinia wa minara jijini Dar es Salaam.

Aidha, Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa magari hayo mapya yatawawezesha mainjinia kutoa huduma bora, za haraka na za uhakika kwa wakazi wa Dar es Salaam, hivyo kuunga mkono jitihada za kuboresha miundombinu ya mawasiliano na huduma muhimu kwa jamii.



Ametamatisha kwa kusisitiza kuwa Synarete itaendelea kushirikiana na wadau wake ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa za kiwango cha juu na zenye tija kwa wananchi.


No comments:

Post a Comment