MENEJA wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) Kitengo cha Bandari, Alfred Shungu amesema kuwa wafanyabiashara wanaobainika kuhujumu vipimo vya mafuta, hasa kwa kutumia vifaa visivyotimiza viwango, watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kifungo au faini isiyozidi Shilingi Milioni 20 kwa kosa la kwanza.
Kauli hiyo leo Julai 2, 2025 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba, yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Shungu ameeleza kuwa lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha uadilifu wa vipimo vya mafuta kwa faida ya serikali na walaji. Ameongeza kuwa WMA hufanya ukaguzi kuanzia meli zinapowasili na bidhaa hiyo hadi vituo vya mafuta, kwa lengo la kulinda haki ya mlaji na kuhakikisha kodi sahihi inalipwa.
Akitoa tahadhari kwa wananchi, Shungu amewahimiza wakague nembo ya WMA kwenye pampu za mafuta ili kuhakikisha kuwa vipimo vimehakikiwa rasmi.
“Unapopimiwa mafuta, hakikisha pampu inaanza kuhesabu kuanzia sifuri (0) na siyo namba yoyote nyingine kama mbili (2),” amesema
Aidha, Shungu ametoa rai kwa watumiaji wa mafuta kuwa waangalifu na kufuatilia usomaji wa kipimo kwa macho wakati wanapohudumiwa ili kuepuka kudhulumiwa.











No comments:
Post a Comment