HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 2, 2025

TIA YAANZISHA KAMPASI MPYA MKOANI TANGA

NA EMMANUEL MBATILO

TAASISI ya Uhasibu Tanzania (TIA) imeanzisha Kampasi mpya ya TIA mkoani Tanga, ambayo inalenga kuhudumia wanafunzi kutoka kanda ya Kaskazini. 

Kampasi hiyo inatajwa kuwa chachu ya kuongeza udahili wa wanafunzi kutokana na ongezeko la wahitimu katika maeneo hayo.

Akizungumza katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere, Mkuu wa Taasisi hiyo, Prof. William Palangyo, ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza wigo wa elimu na kukidhi mahitaji ya soko la ajira linalobadilika kwa kasi.

Aidha Prof. amesema wameanzisha pia kozi mpya katika ngazi mbalimbali ikiwemo Shahada ya kwanza na Shahada ya Pili katika fani za Biashara pamoja na kozi mpya ya Ufuatiliaji na Tathmini (Monitoring and Evaluation).

Katika hatua nyingine, Prof. Palangyo alieleza kuwa TIA inamiliki kampuni tanzu ya kitaalamu iitwayo Tanzania Institute of Accountancy Bureau (TIA Bure), ambayo imekuwa ikitoa huduma za ushauri katika masuala ya biashara, uhasibu na manunuzi kwa taasisi mbalimbali za umma na binafsi.

Kwa lengo la kuendelea kujenga mahusiano na jamii na kuonesha matokeo ya kitaaluma, TIA inatarajia kufanya Mkutano Mkubwa wa Kitaaluma mwezi Novemba 2025 mkoani Mwanza, ambapo wananchi watapata fursa ya kujifunza na kushiriki mijadala ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Prof. Palangyo, Taasisi hiyo kwa sasa ina jumla ya wanafunzi zaidi ya 30,000, na inalenga kuongeza idadi hiyo ili kuendana na dira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha elimu ya juu inawafikia wananchi wengi zaidi.







No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad