HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, May 24, 2025

Msimu wa Tano wa West Kili Forest Tour Challenge 2025 wazinduliwa rasmi

 

Na Mwandishi Wetu, West Kilimanjaro.

Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka amezindua rasmi msimu wa tano wa West Kili Forest Tour Challenge 2025, tukio la utalii na uhifadhi linalotarajiwa kufanyika Juni 21 na 22 mwaka huu katika misitu ya West Kilimanjaro, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza mbele ya wadau wa mazingira, wawakilishi wa sekta ya utalii, wananchi na waandishi wa habari waliohudhuria hafla hiyo Mei 23, 2025 Dkt. Timbuka alieleza kuwa lengo la tukio hilo ni kukuza utalii endelevu, kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na kuwakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali kwa lengo la kushirikiana katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“West Kili Forest Tour Challenge siyo tukio la kawaida. Ni jukwaa la kutangaza vivutio vya asili tulivyonavyo, kuhamasisha uwekezaji katika maeneo ya hifadhi na kuwaunganisha Watanzania kupitia michezo, utamaduni na elimu ya mazingira,” alisema Dkt. Timbuka.

Alisema kuwa tukio la mwaka huu linatarajiwa kuwavutia washiriki kutoka ndani na nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali zitakazofanyika ndani ya hifadhi, zikiwemo matembezi na mbio za umbali wa kilomita 21.1, 10.2 na 5 kwa ajili ya kujionea mandhari ya kipekee ya misitu ya West Kilimanjaro, mbio za baiskeli na Pikipiki, maonyesho ya mavazi ya asili, michezo ya watoto, pamoja na ngoma na sanaa za jadi.
Dkt. Timbuka aliwahimiza Watanzania na wageni kutoka mataifa mbalimbali kushiriki katika tukio hili maana lina manufaa ya moja kwa moja kwa jamii, siyo tu katika nyanja ya uchumi, bali pia kwa elimu na kuendeleza mshikamano wa kijamii.

Aliongeza kuwa usajili wa washiriki wa mwaka huu umerahisishwa kwa njia mbili kuu: moja ni kupitia mtandao kwa kutembelea tovuti rasmi ya www.westkili.co.tz au tickets.westkili.co.tz, na nyingine ni kwa kufanya malipo ya moja kwa moja kwa simu kupitia namba ya Tigo 7878284 kwa jina West Kili Run and Bike au M-Pesa 5362338 kwa jina Pedal Tz.
Akitoa salamu kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mhifadhi Mwandamizi, Tulizo Kilaga alisema kuwa West Kili Challenge inaakisi mkakati wa TFS wa kutumia misitu kama kichocheo cha uchumi wa kijani.

"Tunapotangaza ‘Explore Life in Nature,’ tunawaalika Watanzania kuiona misitu kama fursa si chanzo cha kuni tu, bali mazingira ya michezo, elimu, utalii na uwekezaji,” alisema Kilaga.

Aliongeza kuwa tukio hili linaendana na dira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kukuza uchumi wa kijani na kuhakikisha misitu inanufaisha kizazi cha sasa na kijacho.
Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti West Kilimanjaro, PCO. Robert Faida, alieleza kuwa maandalizi ya miundombinu ya tukio yanaendelea vizuri na kutoa wito kwa wadau wote wa utalii, biashara na uhifadhi kujitokeza kushiriki.

"West Kilimanjaro ina fursa nyingi kuanzia uwekezaji wa kijani hadi utalii wa kipekee. Tunakaribisha sekta binafsi kushirikiana nasi kuendeleza eneo hili,” alisema PCO. Faida.

Tukio la mwaka huu linatarajiwa kuvutia washiriki zaidi ya 2,000 na kuweka West Kilimanjaro kwenye ramani ya kimataifa ya utalii wa mazingira.
Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka akikagua uwanja utakapofanyikia mashindano hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka akifurahia jambo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad