Friday, April 26, 2024

WALIOCHEPUSHA VYAKULA VYA WAATHIRIKA WA MAFURIKO RUFIJI,WAHOJIWA

 

Na Mwamvua Mwinyi, Rufiji
TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) inawahoji watu 11 akiwemo Mtendaji wa kata, kijiji pamoja na vijana Tisa ambao ni wabeba mizigo (makuli) kwa madai ya kuchepusha chakula cha waathirika wa mafuriko Wilayani Rufiji kwa utaratibu usio rasmi.

Mkuu wa wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowelle alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusikitika endapo watu hao watabainika kufanya kitendo hicho.

Alielezea,yupo Mtendaji mmoja wa kata na Mtendaji wa kijiji ambao wakibainika watachukuliwa hatua za kiutumishi.


"Ni taarifa za awali ila kwa haraka haraka kuna mifuko zaidi ya 20 ilidaiwa kufichwa, tulivyobaini tuliaagiza wahusika warejeshe vyakula walivyoficha kisha kuwaripoti katika vyombo vya kisheria ,moja wapo kuhojiwa na TAKUKURU na baada ya uchunguzi watatoa taarifa ya kina."

Gowelle alieleza ,wanatumia vijana mbalimbali kubeba mizigo inayofikishwa kama misaada Rufiji na wanalipwa fedha , Kwahiyo ikitokea vitendo vya aina hiyo ni kuondoa uaminifu.

Aliwatahadhalisha vijana hao makuli kufanya kazi yao kwa uaminifu badala ya kuweka tamaa.

"Wasigeuze kufa kufaana, wafanye kazi yao ya kubeba vifaa, Vyakula Kwa uaminifu badala ya kuficha ama kujichukulia kinyume na taratibu na waache kuanzia sasa watafuatiliwa wakigundulika watachukuliwa hatua kali " alieleza Gowelle.

Pamoja na hayo alieleza ,Rufiji ni miongoni mwa wilaya iliyoathirika na changamoto ya mafuriko,Kati ya wilaya zilizopo kwenye mikoa 14 iliyokumbwa na changamoto hiyo.

Gowelle aliwaasaa, ambao bado wapo kwenye maeneo ya bondeni na yasiyo salama wahame ili kuondokana na changamoto zisizo za lazima.

No comments:

Post a Comment