Monday, May 28, 2018

KIJANA WA MALI ALIYEMWOKOA MTOTO AKUTANA NA RAIS WA UFARANSA, APATA DONGE NONO

 Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii

KIJANA raia wa nchini Mali, Mamoudou Gassam (22) ambaye Jumamosi iliyopita amefanya kitendo cha kishujaa cha kumuokoa mtoto mdogo aliyetaka kudondoka kutoka jengo la ghorofa ya nne, amekutana na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron na kupatiwa zawadi nono.

Mamoudou amekutana na Rais Macron mapema leo kwenye Ikulu ya Elysee Palace kwa ajili ya kufanya mazungumzo pamoja na kupongezwa kwa msaada alioutoa.


Rais Macron amempatia cheti cha Uraia wa Ufaransa kijana huyo ambaye alihamia nchini hapo kwa njia zisizokuwa za kihalali takribani miezi miwili iliyopita kwa ajili ya kutafuta maisha. Lakini pia Rais Macron amempatia kazi Mamoudou katika jeshi la zima moto la Ufaransa.


Kupitia mtandao wa Twitter Rais Macron ameweka picha akiwa Ikulu na kijana Mamoudou na kuandika, “With Mr. GASSAMA who saved Saturday the life of a child climbing 4 floors with bare hands. I announced to him that in recognition of this heroic act he would be regularized as soon as possible, and that the brigade of the firemen of Paris was ready to receive it.”


Kijana huyo ameeleza kuwa alikuwa akipita tu mtaani ndipo alipoona umati wa watu umekusanyika mbele ya jengo.

"Nilijitolea kwa sababu alikuwa ni mtoto," gazeti la Le Parisien lilimnukuu akisema . "Nilikwea jengo... Namshukuru Mungu nilimuokoa." Mamoudou

Wahudumu wa kampuni ya zima moto jijini Paris walifika eneo la tukio na kupata tayari mtoto ameokolewa.

"Kwa bahati nzuri kulikuwa na mtu mwenye nguvu za mwili na mwenye ujasiri wa kwenda na kumchukua mtoto," waokozi wa zima moto walilieleza  shirika la habari la AFP.

Maofisa wa eneo hilo walionukuliwa na vyombo vya habari vya Ufaransa wakieleza kuwa wazazi wa mtoto huyo hawakuwa nyumbani wakati akiokolewa.

aidha baba yake amekuwa akihojiwa na polisi kwa  kushukiwa kumuacha mwanae bila mtu wa kumuangalia, zimeeleza taarifa za mahakama.

No comments:

Post a Comment