Wednesday, March 9, 2016

DAWASCO YABAINI WIZI WA MAJI MANZESE

Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) limeendelea kufanya operesheni maalumu ya kubaini wezi wa Maji na waharibifu wa miundombinu kwenye maeneo tofauti ya jijini humo na kubaini wizi mkubwa wa Maji eneo la Manzese Uzuri.

Katika msako huo uliofanyika juzi katika mtaa wa Chakula bora ,Manzese Uzuri , Dawasco ilibaini kuwepo kwa pampu kubwa mbili za kuvuta Maji zilizofungwa kwenye mabomba ya kupeleka Maji kwa wateja kinyume cha sheria.

Akizungumza kwenye tukio hilo Meneja wa Dawasco Magomeni, Mhandisi Pascal Fumbuka alieleza kuwa walipata taarifa za wizi wa Maji kutoka kwa wasamaria wema jinsi Maji yanavyouzwa kiwizi nyuma ya baa inayoitwa Migombani ambapo mmiliki wa eneo hilo aitwaye Donald Shirima alikimbia baada mafundi kutoka Dawasco kufika kwenye tukio.

“Tulipata taarifa ya wizi wa Maji kutoka kwa msamaria mwema, alitupa taarifa kuwa mwenye eneo alikuwa akiuza Maji kwa muda mrefu sana bila kuwa na mita kutoka Dawasco hivyo tulifika eneo la tukio “alisema Fumbuka.

Ofisa Mtendaji wa kata ya Manzese, Bi Salome Chilumba aliwasihi wananchi kuendelea kuwafichua  wezi wa Maji kwani hao ndio wanaofanya waliounganishiwa kihalali na Dawasco kukosa huduma hiyo. 

“Watu wanaohujumu huduma ya Maji kwa kujiunganishia kiholela hawafai ni lazima wote tushirikiane kuwafichua”,alisema Chilumba.

No comments:

Post a Comment