Thursday, March 19, 2015

Kuelekea Mpambano Ndondi kati ya Mohamed Matumla na Wang Xin Hua wa China

Mwandishi Wetu

Wakati bondia Mohamed Matumla Jr akiwa katika mazoezi ya mwisho mwisho kumkabili Wang Xin Hua wa China, wenzake Thomas Mashali na Karama Nyilawila wametoleana uvivu huku kila mmoja akijigamba kutwaa ubingwa watakapozichapa Machi 27 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

Matumla Jr atazichapa na Hua pambano la super bantam la ubingwa wa dunia wa (WBF World Eliminate) pambano maalumu kwa mabondia hao la kutafuta tiketi ya kucheza pambano la utangulizi kwenye lile la nguli wa masumbwi duniani, Manny Pacquiao na Floyd Mayweather la Mei 2. 

Kama Matumla atampiga Hua kwenye pambano lao la Machi 27 na kuonyesha kiwango kizuri atapata nafasi ya kucheza pambano la utangulizi kuwasindikiza nguli hao wa masumbwi duniani watakapovaana Mei 2 jijini Las Vegas.

Akizungumza katika mazoezi yake yanayoendelea kwenye gym ya Oil Com, Keko jijini Dar es Salaam chini ya kocha wake ambaye ni baba yake mzazi, Rashid 'Snake Man' Matumla, bondia huyo alisema hataki kupoteza nafasi ya kucheza kwenye pambano la Mayweather na Pacquiao.

"Najua ugumu wa pambano langu na Hua hivyo sitaki kufanya mzaha, niko fiti na sasa nafanya mazoezi mepesi ili kumkabili lakini pia sitaki kupoteza nafasi ya kuwasindikiza nguli wa masumbwi duniani kwani ni pambano ambalo 'litanitoa'," alisema Matumla Jr.

Kocha wake alisema, hivi sasa bondia huyo anajifua katika mazoezi ya mwisho mwisho ambayo ni ya wepesi na kumweka tayari kumkabili Hua. "Mudy yuko fiti, nimekuwa naye katika mazoezi, kiwango chake kinaridhisha na sasa yuko katika hatua ya mwisho kabisa ambayo ni ya mazoezi mepesi ya kumuweka tayari kwa pambano," alisema kocha wa bondia huyo.

Promota wa pambano hilo, Jay Msangi alisema ili Matumla Jr apate nafasi ya kuwasindikiza Pacquiao na Mayweather ni lazima aonyeshe kiwango kwenye pambano lake na Hua.

"Tayari tumemwambia Matumla Jr vigezo hivyo kwani si ili mradi kushinda bali aonyeshe kiwango kama ni ngumi ziwe ngumi kweli kwani hawezi akacheza kwa kukumbatia na kushinda kwa pointi alafu apewe nafasi ya kucheza Las Vegas, kule mashabiki wanataka waone ngumi hivyo Matumla Jr anapaswa kupambana Machi 27 ili apate nafasi hiyo," alisema.

Siku hiyo pia, Japhet Kaseba atazichapa na Mada Maugo wakati Karama Nyilawila akionyeshana ubabe na Thomas Mashali ambapo mabondia hao kila mmoja amejigamba kutwaa ubingwa.

"Sina hofu na mpinzani wangu kwani kiwango chake nakijua na amekuwa bondia wa kukimbia kimbia ulingoni hivyo ajiandae, cha msingi ni mashabiki wangu kujitokeza kwa wingi kunipa sapoti," alisema Nyilawila.

Wakati Mashali akijinadi kuwa yeye ataonyesha vitendo ulingoni siku hiyo kwani nafasi ya kupigwa na Nyilawila haipo kwake na kusisitiza kuwa yuko fiti na hatarajii kama mpinzani wake atamaliza raundi zote siku hiyo.

No comments:

Post a Comment