Sunday, February 15, 2015

NHIF shikamaneni kwenye kazi - Humba

WATUMISHI wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, (NHIF) wametakiwa kushikamana kwa pamoja na kufanya kazi bila kujali muda wa kazi ili kuhakikisha shirika hilo linabaki na heshima yake huku wanachama wakihudumiwa kwa heshima.

Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bw. Emanuel Humba katika hafla ya kuaagwa wastaafu wa Mfuko huo.

Bw. Humba ambaye naye alikuwa ni miongoni mwa waagwa, alisema kuwa mbinu kubwa ya kushinda katika utenda kazi kushikamana na kufanya kazi kwa ushirikiano bila kujali hali ya aina yoyote.

“Nawaombeni wafanyeni kazi kwa ushirikiano, Menejimenti wajalini watumishi na ninyi kwa ninyi kuweni kitu kimoja, sisi tumeacha heshima kwa shirika kwa kuwa tulifanya kazi bila ubaguzi na tulishirikiana sana,”

 “Nitahudhunika sana nikiona au kusikia shirika hili likifa au kudorola, sisi wenzenu nikiwemo mimi ambaye ni mwanzilishi sitakubali kuona hali hii kwa kuwa nimewekeza nguvu kubwa sana ndani ya Mfuko huu, watumikieni Watanzania kwa heshima ili lengo la kuanzishwa kwa Mfuko huu lisipungue,” alisema Bw. Humba.

Aliwataka watumishi wa Mfuko huo kila mmoja kwa nafasi yake kutimiza wajibu wake bila ya kusukumwa na mwingine lakini pia kujenga mshikamano na ushirikiano katika kazi ili kuzidi kuboresha na kuliimarisha shirika hilo.

Bw. Humba alitumia fursa hiyo kuishukuru Bodi pamoja na Menejimenti na watumishi wote kwa ujumla kwa kuona umuhimu wa kuwaaga na kuonesha kuthamini mchango wake katika utendaji kazi wake wakati akiongoza shirika hilo. 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Balozi Alli Muchumo alimpongeza Bw. Humba kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi chake ambayo imezaa matunda makubwa kwa Taifa na kuleta heshima ya nchi hii Kimataifa.

“Sisi kama Bodi tunatambua mchango wako na tunajua nia nzuri uliyonayo katika shirika hili, tum efurahi kukuaga leo siku ambayo tuliingoja kwa hamu kubwa,” alisema Bw. Muchumo.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Bw. Michael Mhando alisema kuwa ataendeleza yote yaliyoachwa na Bw. Humba kwa maslahi ya Watanzania na akamuomba kuwa endapo Mfuko utahitaji busara zake asichoke kuusaidia.

No comments:

Post a Comment