Thursday, September 6, 2012

Misitu Yetu Itaendelea Kuharibiwa Hivi Mpaka Lini?

 Haya ni magogo yaliyokuwa yamevunwa isivyo halali katika msitu wa Ngumburuni, Msitu huu upo wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani.
Miti hii ilikatwa kwa ajili ya uchomaji wa mkaa.

Msitu huu wa asili na misitu mingine mbalimbali nchini imekuwa ikivamiwa na kuvunwa isivyo halali kwa kiwango cha kutisha kwa faida ya watu wachache. Magogo haya yalikamatwa na wanavijiji wa kijiji cha MUYUYU moja ya vijiji vinavyozunguka  msitu huu baada ya juhudi zao za kuomba msaada wa kukomeshwa kwa uvunaji haramu kutoka ofisi ya wilaya kushindikana. 

Baada ya juhudi hizo kushindikana waliamua kutumia vyombo vya habari mbalimbali ili kufikisha malalamiko yao ngazi za juu zaidi.. 

Baada ya taarifa kutoka kwenye vyombo vya habari, wavunaji haramu ambao wanatumia vyombo vya kisasa kuchakata magogo walikimbia na kuacha magogo msituni. Wanakijiji walichangishana fedha na kuzomba magogo kutoka msituni na kuleta kijijini. LAKINI UHARIBIFU MKUBWA AMBAO UNGEWEZA KUDHIBITIWA TOKA AWALI ULIKWISHA TOKEA.

Tutambue kuwa misitu hii inaharibika huku tukiwa na taasisi mbalimbali ambazo zimepewa jukumu la kusimamia misitu yetu vizuri, taasisi hizi zinawafanyakazi ambao ndio wamepewa jukumu hilo. Changamoto kubwa ni kwamba kumekuwa na wafanyakazi wachache wasiokuwa  waaminifu na hivyo kushirikiana na wahalifu kuharibu misitu yetu huku nchi ikikosa pia mapato.. 
Hii haikubaliki, haikubaliki wananchi wanaojitolea bure bila malipo kuisaidia serekali kusimamia misitu yake wanatoa taarifa kwa mamlaka iliyopewa dhamana ya kusimamia mistu kisheria na mamlaka hizo kupuuza huku misitu yetu ikiendelea  kuharibiwa kila kukicha. 
Imefika wakati sasa kila afisa wa msitu/misitu kuwajibika kutokana na hali ya misitu wanayopewa kuisimamia. Kama hawatawajibishwa maana yake hawataweka juhudi zozote kuhakikisha wanailinda misitu yetu vizuri.. 
Afisa misitu anapopewa taarifa za uvunaji wa kutisha ndani ya msitu aliopewa jukumu la kuusimamia na kutochukua hatua stahiki kwa visingiziao visivyokuwa na mashiko tumuelwe vipi? 
Tukisema anashirikiana na wavunaji haramu kuhujumu misitu yetu tutakuwa tunakosea? Wakala wa misitu, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wasaidie kuhakikisha watumishi wao wanatenda kazi yao inavyostahili. 
Mkuu wa mkoa wa Tanga ametuonyesha mfano wa namna ya kuwawajibisha watendaji wake kwa kumshtaki mwenyekiti wa kijiji kwa kosa la kutochukua hatua zozote huku msitu uliopo kijijini kwake ukiteketea kwa uchomaji wa mkaa. Mamlaka nyingine zinaweza, Hii ndio tafsiri ya uwajibikaji kwa vitendo.

No comments:

Post a Comment