Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein,(wa tano kushoto) pamja na Viongozi wengine wa Serikali wakiungana na Waislamu katika Swala ya kuwaombea Dua Abiria waliofariki katika Ajali ya Meli Mv Skagit ya Kampuni ya Seagul,iliyozama hivikaribuni ikitokea Dar es Salaam kuelekea Zanzibar,swala hiyo ikiongozwa na Mufti wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi,katika Msikiti wa Mwembeshauri Mjini Zanzibar leo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein,(katikati) pamja na Viongozi wengine wa Serikali wakiungana na Waislamu katika Hitma ya kuwaombea Dua Abiria waliofariki katika Ajali ya Meli Mv Skagit ya Kampuni ya Seagul,iliyozama hivikaribuni ikitokea Dar es Salaam kuelekea Zanzibar, katika Msikiti wa Mwembeshauri Mjini Zanzibar leo.
Baadhi ya Waislamu waliohudhuria katika Hitma ya kuwaombea Dua Abiria waliofariki katika Ajali ya Meli Mv Skagit ya Kampuni ya Seagul,iliyozama hivikaribuni ikitokea Dar es Salaam kuelekea Zanzibar, katika Msikiti wa Mwembeshauri Mjini Zanzibar leo.Picha na Ramadhan Othman Ikulu.
Na Juma Mohammed,MAELEZO Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk Ali Mohammed Shein amewaongoza wananchi katika sala maalum ya maiti kuwaombea watu waliofariki katika maafa ya kuzama kwa Meli ya Mv. Skagit.
Sala maalum na dua ilifanyika katika Msikiti Mushawar, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ambapo pia katika sehemu mbalimbali dua na sala maalum za kuwaombea waliopoteza maisha kwenye maafa ya kuzama kwa Meli ya Mv. Skagit ilifanyika.
Mbali ya Rais kuhudhuria katika kuwaombea dua marehemu, pia viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muunganao wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar,Balozi Seif Ali Idd, Rais mstaafu wa Zanzibar,Dk.Amani Abeid Karume,Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho.
Viongozi wengine ni pamoja na Mawaziri, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wananchi mbalimbali. Serikali imeandaa Sala na dua hiyo ni maalum kwa ajili ya kuwaombea watu waliokufa katika maafa ya kuzama kwa meli ya Mv. Skagit iliyozama karibu na Kisiwa cha Chumbe Zanzibar.
Wakati huo huo, Maiti tano zimepatikana katika bahari ya Zanzibar na kufanya idadi ya maiti zilizopatikana hadi sasa kufikia 73.
Maiti hizo zimepatikana pembezoni mwa Kisiwa cha Chumbe zikiwa zinaelea saa 5: 30 asubuhi zikiwa zinaelea ikiwa maiti za wanaume wanne na mwanamke mmoja.
Maiti moja ya mwanaume mtu mzima imekutwa na kitambulisho katika mfuko wa suruali chenye jina la Philip John Busia mwenye umri wa miaka 35 mkazi wa Mkoa wa Mwanza.
Katika taarifa ya Serikali ilisema watu waliookolewa wakiwa hai ni 146. juhudi za utafutaji miili mengine inaendelea katika eneo ilipozama meli hiyo.
Meli ya Mv. Skagit ilizama Julai 18,2012 karibu na Kisiwa cha Chumbe umbali wa maili sita kuelekea Kusini mwa Kisiwa kidogo cha Yasin Zanzibar ikitokea Bandari ya Dar es Salaam ilikoanza safari saa 5:30 asubuhi.
Meli hiyo inamilikiwa na Kampuni ya Sea Guall Sea Transport Ltd, Kampuni ambayo Meli yake nyengine ya Mv. Fatih ilizama ikiwa Bandarini Malindi Zanzibar na kufariki watu sita mwaka 2009.



No comments:
Post a Comment