HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 27, 2026

SERIKALI YAPANGA UJENZI WA BARABARA YA NJIA NANE KIBAHA–CHALINZE KUPITIA MRADI WA EXPRESSWAY

Na Janeth Raphael -MichuziTv - Dodoma


Serikali imesema ipo katika hatua za kuendelea na mpango wa ujenzi wa barabara ya kisasa ya Expressway kutoka Kibaha hadi Morogoro, huku kipande cha Kibaha hadi Chalinze kikitarajiwa kuwa sehemu ya mradi huo mkubwa wa miundombinu utakaotekelezwa kwa mfumo wa ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP).

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo na Naibu Waziri wa Ujenzi Godfrey  Kasekenya wakati akijibu swali la Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Francis Koka, ambaye alihoji ni lini Serikali itaendeleza mradi wa upanuzi wa barabara ya Dar es Salaam – Morogoro, hususan kipande cha Kibaha hadi Chalinze, kuwa na njia nane.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kasekenya amesema  Serikali kwa sasa imejikita katika mpango wa kujenga barabara mpya ya Expressway yenye urefu wa kilometa 163.8 kutoka Kibaha – Chalinze – Morogoro, mradi unaolenga kuongeza ufanisi wa usafirishaji na kupunguza msongamano mkubwa wa magari katika barabara hiyo muhimu ya kiuchumi.

Amesema utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kufanyika kwa utaratibu wa PPP, ambapo Serikali itaingia ubia na wawekezaji binafsi ili kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo ya kisasa inayotarajiwa kuwa mkombozi mkubwa kwa watumiaji wa njia hiyo.

Hata hivyo, Kasekenya  ameeleza kuwa mazungumzo yaliyokuwa yanaendelea kati ya Serikali na mwekezaji wa awali hayakufikia makubaliano, jambo lililosababisha Serikali kuanza upya mchakato wa kumpata mwekezaji mwingine atakayetekeleza mradi huo.

“Kwa sasa taratibu za kumpata mwekezaji mpya zinaendelea baada ya majadiliano na mwekezaji wa awali kushindikana,” alisema Waziri huyo bungeni.

Aidha, Serikali imewahakikishia wananchi na watumiaji wa barabara hiyo kuwa wakati taratibu za mradi mpya zikiendelea, itaendelea kufanya matengenezo mbalimbali katika barabara ya sasa ya Kibaha hadi Chalinze ili kuhakikisha inapitika vizuri katika kipindi chote cha mwaka.

Barabara ya Dar es Salaam – Morogoro ni moja ya njia kuu zinazobeba shughuli nyingi za uchumi nchini, ikitumika kusafirisha mizigo na abiria kutoka Bandari ya Dar es Salaam kuelekea mikoa ya ndani pamoja na nchi jirani. Kutokana na ongezeko kubwa la magari na shughuli za kiuchumi, barabara hiyo imekuwa ikikumbwa na changamoto ya msongamano wa magari, hasa katika maeneo ya Kibaha na Chalinze.

Ujenzi wa Expressway hiyo unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuboresha miundombinu ya usafiri nchini, kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma ndani na nje ya Tanzania.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad