TSC, WORLD VISION WATOA MAFUNZO KUIMARISHA MAADILI YA WALIMU, KUMLINDA MTOTO - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, February 2, 2023

TSC, WORLD VISION WATOA MAFUNZO KUIMARISHA MAADILI YA WALIMU, KUMLINDA MTOTO

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya World Vision Tanzania wameandaa mafunzo kwa Wadau mbalimbali wa Elimu kuhusu Wajibu wa Mwalimu katika masuala ya Ajira, Maadili na Ushughulikiaji wa Mashauri ya Nidhamu, kwa ajili ya kuelimisha jamii juu ya haki, ustawi wa mtoto na wajibu wa mzazi/mlezi katika kumlea na kumlinda mtoto.

Mafunzo hayo ya siku tatu, Februari 1 – 3, 2023 yanayofanyikia mjini Shinyanga yamehusisha wadau wa Elimu kutoka Wilaya za Mikoa ya Shinyanga, Tabora na Simiyu ambapo washiriki ni Watumishi wa TSC, Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati za Nidhamu za TSC ngazi ya Wilaya, Wathibiti Ubora na Maafisa Ustawi wa Jamii ili kuwezesha washiriki hao kutoa elimu hiyo kwa walimu katika ngazi ya shule.

 

 Mafunzo hayo yamefunguliwa Februari 1, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambapo amesema mmomonyoko wa maadili katika jamii ni agenda ya Kitaifa inayohitaji nguvu ya pamoja ili kumlinda mtoto dhdi ya ukatili unaotokea mara kwa mara katika jamii. 

 Kiongozi huyo amefafanua kuwa inasikitisha kuona wapo baadhi ya walimu wanajihusisha na vitendo vya uvunjifu wa maadili hususan kwa watoto wakati jamii imewaamini na kuwakabidhi wanafunzi ili wawalee huku akisema kuwa ukiukwaji huo unasababisha baadhi ya wazazi kuanza kukata tamaa kuwapeleka watoto shule hususan wale waliotakiwa kujiunga kidato cha kwanza kwa kuona kuwa watoto hawapati kile wanachostahili.  

 “Mmomonyoko wa maadili ya watu wakiwemo walimu imekuwa ni tatizo kubwa. Agenda hii tunayo kama taifa na hata katika Mkoa wetu wa Shinyanga tunatambua na tupo kwenye mikakati ya kukabiliana nayo. Tunashukuru TSC pamoja na World Vision kwa kuja na wazo hili la kuwakusanya wadau hawa ambao kila mmoja anahusika kwa mwalimu na kwa mtoto.” 

 “Mambo haya tunayafanya sisi ambao tumekabidhiwa watoto, hatuwalei katika misingi inayotakiwa. Baadhi ya walimu hawana maadili, wanaanzisha mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi, wengine wanawapa mimba wanafunzi na wengine kutoa adhabu kupitiliza nk. Wakati mwingi haya yanapotokea baadhi ya wazazi wanakata tamaa kupeleka watoto shule kwa kuwa wanaona watoto hawaendi kupata kitu wanachotakiwa kupata,” amesema.

 Mkuu huyo wa Wilaya ameongeza kuwa wapo baadhi ya walimu ambao hawatimizi wajibu wao, hawafundishi, wanakuwa na dharura mara kwa mara za kuwa nje ya kituo cha kazi huku wakipokea mishahara ambayo hawaifanyii kazi, hivyo amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha wanakwenda kuwaelimisha walimu juu ya umuhimu wa kumpatia mtoto haki yake ya kufundishwa na kulindwa dhidi ya uovu wowote. 

 Ameongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kuimarisha miundombinu ya shule ikiwemo ujenzi wa madarasa, vyoo, madawati na sasa ujenzi wa nyumba za walimu akiwa na matarajio kwamba watoto wapate elimu bora.

 “Pamoja na juhudi hizi za Rais, bado unakuta mpaka leo Januari imekwisha tupo mwezi Februari lakini kuna wanafunzi wamefaulu kwenda kidato cha kwanza lakini hawajafika shuleni. Miaka michache iliyopita tulikuwa tunasema madarasa hayatoshi sasa hivi madarasa ni mengi tunatafuta watoto waje wasome. Lazima tuwaeleze walimu kuwa wana wajibu mkubwa kuwafanya watoto wapende na wafurahie kuwepo shuleni,” amesema. 

 Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ajira Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC, Fatuma Muya amesema kumekuwa na changamoto ya walimu wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa Maadili ya Kazi ya Ualimu na hivyo kuifanya kazi ya Ualimu ipoteze hadhi yake.

 “Ni jambo lililo dhahiri kuwa Mwalimu anayezingatia Maadili na Miiko ya kazi yake ana mchango mkubwa katika wa kukuza taaluma ya ualimu na kuifanya Shule iwe salama,” amesema.

 Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa pamoja na jitihada ambazo Tume hiyo inazichukuwa ikiwemo kutoa elimu kuhusu maadili ya kazi ya ualimu, baadhi ya walimu wamemeendela kukiuka maadili ya utumishi wao ambapo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2016/17 hadi 2021/22 jumla ya walimu 11,022 walipatikana na makosa mbalimbali na kuchukuliwa hatua za kinidhamu. 

 Kwa mujibu wa Muya, Makosa hayo yaliyofanyika ni pamoja na utoro, kughushi vyeti vya kitaaluma, mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi, ukaidi na ulevi wakati wa kazi.

 “Ni matumaini yangu kuwa kikao kazi hiki kitawawezesha washiriki wa mafunzo ya kujengeana uwezo kuyaelewa vyema Masuala ya Ajira, Wajibu wa Mwalimu na Kanuni za Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu ili hatimaye wakatoe mafunzo kwa Walimu waliopo shuleni,” amesema. 

 Naye Meneja Mradi wa Taasisi ya World Vision Tanzania Kanda ya Nzega, Jackine Kaihura amesema Taasisi hiyo inalenga kuhakikisha maisha ya mtoto yanakuwa mazuri na dunia inakuwa sehemu salama zaidi kwa mtoto kuishi.

 Ameongeza kuwa Taasisi hiyo imeamua kushirikiana na TSC kutoa mafunzo hayo kwa kuwa Tume hiyo ndiyo inayosimamia Maadili na Nidhamu ya walimu na kwa kuwa mtoto yupo na mwalimu kwa muda mrefu zaidi ni muhimu TSC ichukue jukumu la kuwaelimisha walimu ili waishi na watoto kwa usalama.

 “Kuna umuhimu mkubwa wa kuboresha tabia za walimu ili waendelee kuishi na watoto wetu vizuri wanapokuwa shuleni. Shuleni ni sehemu ambapo mtoto anakaa muda mwingi zaidi kuliko nyumbani na uhalifu dhidi ya watoto unaweza kutokea shuleni zaidi kuliko hata nyumbani. Hivyo, baada ya mafunzo haya washiriki watakwenda kuwaelimisha walimu ambao ndio walengwa. Tunaamini kwa kufanya hivyo vitendo vya uhalifu dhidi ya watoto vitapungua,” amesema Jacline. Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude (wa pili kutoka kulia) akikata utepe kuzindua vitini vitakavyotumika kutoa mafunzo kwa walimu katika ngazi ya shule juu ya Wajibu wa Mwalimu katika masuala ya Ajira, Maadili na Wajibu wa Jamii katika kumlinda Mtoto. Amezindua vitini hivyo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wadau wa elimu kutoka Wilaya za Mikoa ya Shinyanga, Tabora na Simiyu Februari 1, 2023 mjini Shinyanga.Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude akifungua mafunzo kuhusu Wajibu wa Mwalimu katika masuala ya Ajira, Maadili na Wajibu wa Jamii katika kumlinda Mtoto. Mafunzo hayo yamefanyika mjini Shinyanga Februari 1, 2023, yameandaliwa na TSC kwa kushirikiana na Taasisi ya World Vision Tanzania na yamehusisha wadau wa Elimu kutoka Wilaya za Mikoa ya Shinyanga, Tabora na Simiyu.Mkurugenzi wa Ajira Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC, Fatuma Muya akitoa neno la kumkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Kishapu (hayupo pichani) ili afungue mafunzo ya wadau wa Elimu kutoka Wilaya za Mikoa ya Shinyanga, Tabora na Simiyu. Mafunzo hayo yanafanyika Februari 1 – 3, 2023 mjini Shinyanga.Meneja Mradi wa Taasisi ya World Vision Tanzania Kanda ya Nzega, Jackine Kaihura akitoa neno la utangulizi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wadau wa elimu kutoka Wilaya za Mikoa ya Shinyanga, Tabora na Simiyu yanayofanyika Februari 1 – 3, mjini Shinyanga.Kiongozi wa Elimu wa Taasisi ya World Vision Tanzania, Jennifer Mhando akitoa neno la shukrani kwa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu (hayupo pichani) mara baada ya ufunguzi wa mafunzo ya wadau wa elimu kutoka Wilaya za Mikoa ya Shinyanga, Tabora na Simiyu Februari 1, 2023 mjini Shinyanga.


Washiriki wa Mafunzo wa mafunzo ya wadau wa elimu kutoka Wilaya za Mikoa ya Shinyanga, Tabora na Simiyu yanayofanyika Februari 1 – 3, 2023 mjini Shinyanga wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude (katikati kwa waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Elimu kutoka Wilaya za Mkoa wa Simiyu wakati wa mafuzo ya washiriki hao yanayofanyika Februari 1 – 3, 2023 mjini Shinyanga. Pichani, wa pili kutoka kushoto (waliokaa) ni Mkurugenzi wa Ajira Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC, Fatuma Muya na wa pili kutoka kulia (waliokaa) ni Meneja Mradi wa Taasisi ya World Vision Tanzania Kanda ya Nzega, Jackine Kaihura.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude (katikati kwa waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Elimu kutoka Wilaya za Mkoa wa Tabora wakati wa mafuzo ya washiriki hao yanayofanyika Februari 1 – 3, 2023 mjini Shinyanga. Pichani, wa pili kutoka kushoto (waliokaa) ni Mkurugenzi wa Ajira Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC, Fatuma Muya na wa pili kutoka kulia (waliokaa) ni Meneja Mradi wa Taasisi ya World Vision Tanzania Kanda ya Nzega, Jackine Kaihura.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude (katikati kwa waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa TSC pamoja na watumishi wa Taasisi ya World Vision Tanzania walioshiriki mafunzo ya wadau wa elimu kutoka Wilaya Mikoa ya Shinyanga, Tabora na Simiyu yanayofanyika Februari 1 – 3, 2023 mjini Shinyanga. Pichani, wa pili kutoka kushoto (waliokaa) ni Mkurugenzi wa Ajira Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC, Fatuma Muya na wa pili kutoka kulia (waliokaa) ni Meneja Mradi wa Taasisi ya World Vision Tanzania Kanda ya Nzega, Jackine Kaihura.Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude (katikati kwa waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Elimu kutoka Wilaya za Mkoa wa Shinyanga wakati wa mafuzo ya washiriki hao yanayofanyika Februari 1 – 3, 2023 mjini Shinyanga. Pichani, wa pili kutoka kushoto (waliokaa) ni Mkurugenzi wa Ajira Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC, Fatuma Muya na wa pili kutoka kulia (waliokaa) ni Meneja Mradi wa Taasisi ya World Vision Tanzania Kanda ya Nzega, Jackine Kaihura.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad