REKEBISHENI UTOAJI WA HUDUMA ZENU NDANI YA SIKU SABA. - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 3, 2023

REKEBISHENI UTOAJI WA HUDUMA ZENU NDANI YA SIKU SABA.

 

Na Janeth Raphael

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dkt.Selemani Jafo, ametoa siku 7 kwa wamiliki wa kumbi za Starehe na Taasisi za dini kurekebisha utoaji wa huduma zao, kutokana na kukithiri kwa uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele na mitetemo, ili ziendane na takwa la sheria ya mazingira na kanuni zake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 3,2023 Jijini Dodoma, kuhusu uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele na mitetemo Dkt.Jafo ameiagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufungia maeneo yote yatakayo kaidi kutekeleza sheria na kanuzi za mazingira kuhusu kelele na mitetemo baada ya siku 7 tangu agizo kutolewa.

"Kama mtakavyokumbuka, tarehe 29 Julai, 2019 nilitoa maelekezo ya kuwataka wadau wote wanaohusika kuhakikisha wanazingatia sheria na miongozo inayodhibiti uchafuzi wa Mazingira unaotokana na kelele na mitetemo na pia hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa wale ambao shughuli zao zinasababisha kelele kuzidi viwango vilivyoainishwa,"

Na kuongeza kuwa "hata hivyo, pamoja na kuchukua hatua hizi za kisheria, kumekuwa na ongezeko la malalamiko ya kelele na mitetemo. Kwa kipindi cha mwaka 2021/2022 asilimia 65 ya Malalamiko yaliyowasilishwa Baraza la Mazingira yanahusu kelele na mitetemo, hali inayoonesha adhabu za kutozwa faini kwa waokamatwa zimezoeleka na hazitoshi,"amesema Dkt.Jafo

Waziri huyo amewataka Wamiliki wa maeneo ya burdani, starehe na nyumba za ibada kuzingatia matumizi ya vipima kelele na vizuia sauti ili kuhakikisha jamii zinazozunguka maeneo hayo haziathiriwa na kelele wanazozisababisha.

"Wamiliki wa nyumba za ibada na kumbi za starehe hakikisheni sauti zitokanazo na shughuli zenu hazizidi viwango vinavyokubalika kwa mujibu wa sheria,"

Na kuongeza kuwa "Wananchi toeni taarifa kuhusu kelele na mitetemo kwenye ofisi za serikali za mitaa au ofisi za Baraza la Taifa la Mazingira na kuhakikisha kelele na mitetemo inakuwa agenda ya kudumu katika vikao vya wakaazi ili kulipatia ufumbuzi suala hili,"amesisitiza Dkt.Jafo

Pia amezitaka Wizara za kisekta, Taasisi za umma, Sekretarieti za mikoa, Mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha zinatekeleza majukumu yao yaliyoainishwa kwenye mwongozo wa udhibiti wa uchafuzi wa mazingira utokanao na kelele na mitetemo wa mwaka 2021.

Aidha, amelielekeza Baraza la Taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira katika kanda zote kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa kanuni za udhibiti wa kelele na mitetemo za mwaka 2015, hasa kwa kuhakikisha wazalishaji sugu wa uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele na mitetemo wanachukuliwa hatua kali hususan kufungiwa shughuli zao wanazozifanya.

Sheria ya Mazingira Sura ya 191, Kifungu cha 106 (5 na 6) kinakataza kupiga kelele kuzidi viwango vilivyoruhusiwa na vilevile ni kosa kupiga kelele kinyume na viwango vilivyoruhusiwa. Kanuni za udhibiti wa kelele na mitetemo za mwaka 2015, zimeainisha viwango vya sauti vinavyoruhusiwa kwenye maeneo ya makazi, biashara, viwanda na hospitali ili kulinda afya ya jamii.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Dkt Selemani Jafo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma.


 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad